The Chant of Savant

Thursday 11 August 2011

Wizi UDA tutaendelea kuwa shamba la bibi hadi lini?




Taarifa kuhusu ufisadi na utata wa ubinafsishaji lililokuwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) zinatia kinyaa ukiachia mbali kuwa onyo kwa serikali kuwa wakati wa kuwashughulikia wezi ni huu. Habari toka bungeni ni kwamba UDA iliuzwa kwa shilingi 1, 200,000,000 wakati thamani yake ni mara kumi ya hii yaani shillingi 12, 000,000,000.

Utata ulizidi kuongezeka baada ya kugundulika kuwa kigogo mmoja ambaye ni mmojawapo wa viongozi wa wazee wa Dar es Salaam alikutwa akiwa amepewa shilingi 250,000,000 kwenye akaunti yake. Huu jamani ni ujambazi wa mchana hata kama unafanywa na watu wakubwa kwa kutumia kalamu. Je hawa wezi wanapata wapi hii jeuri ya kututenda hivi wakati mamlaka zikipata kigugumizi kuwashughulikia? Kazi ya mamlaka ni nini kama mali za umma zinaibiwa na fedha kuchotwa kila uchao?

Mbunge wa Mafia (CCM), Abdulkarim Shah alisema haiwezekani UDA yenye rasilimali za sh bilioni 12 ziuzwe kwa sh bilioni 1.2 kwa Kampuni ya Simon Group ambayo ununuzi wake wa hisa umegubikwa na mizengwe.

Shah alikaririwa akisema: “Mheshimiwa Mwenyekiti ni aibu kusikia shirika hili linauzwa ni aibu, kamata wote waliohusika kuliuza, Meya, Mkurugenzi wa Jiji, bodi yote kamata halafu Takukuru wafanye kazi yao.

Shah aliongeza: “Unakwenda kuuza terminal ya Kurasini, ni aibu, nasema Wallahi Wabilahi na Ramadhani hii, sintokubali, nasema watu hawa wawekwe ndani na wachunguzwe.

Je ushauri wa mbunge utafanyiwa kazi? Je ni wabunge wangapi wana mawazo kama haya ukiachia mbali wananchi wanaowawakilisha? Je tutaendelea kuwa shamba la bibi hadi linin a kwanini? Je wahusika kipindi hiki watafanya mambo tofauti au ni yale yale ya business as usual katika kulindana na kuokoana kwenye ufisadi na dhuluma kwa taifa?

Nchi yetu imegeuka shamba la bibi na wananchi wanaendelea kugeuzwa mataahira kila uchao. Nani mara hii kasahau kashfa ya Kiwira kuuzwa kwa shilingi 70, 000,000 kwa rais mstaafu Benjamin Mkapa, familia yake na marafiki zake ilhali thamani yake halisi ni bilioni 4,000,000,000? Tuliambiwa tumuache mzee Mkapa apumzike baada ya kuambiwa ana kinga kisheria. Je huyo mkewe, watoto wake na marafiki zake nao wana kinga ya urais ule ule wa Mkapa? Kwanini hatukuelezwa mapema kuwa kinga ya urais ni suala la kifamilia na marafiki? Kwanini hatuambiwi kuwa siku hizi urais wa Tanzania ni wa ushirika na si suala mtu mmoja tuliyemchagua na kumlisha kiapo kama inavyosema katiba? Wengi watajiuliza maswali yote haya ni ya nini.

Baada ya Mkapa kubainika kuwa alijitwalia Kiwira kinyume cha sheria nini kilifanyika zaidi ya kupigwa siasa na wananchi kusahau wakaendelea kusota kwa kulanguliwa umeme na mgao wa umeme? Nani mara hii kasahau kadhia iliyouawa kimya kimya ya Katibu Tawala zamani wa Mkoa kilimanjoro, Hilda Gondwe, kujiuzia gari aina ya Toyota Land Cruiser VX lililokuwa limenunuliwa miaka mitatu iliyopita kwa sh 155,000,000 kwa shilingi milioni kumi? Je mhusika alifanywa nini zaidi ya wahusika kutopoteza hata muda kujibu achia mbali kumchukulia mtuhumiwa hatua? Je ni magari au mali kiasi gani vya umma vimeishapotea kwenye mazingira kama haya nchi nzima na kwa muda wote tangu ufisadi uanze kuwa order of the day?

Nani kasahau ujenzi wa nyumba za TANESCO kwa mabilioni na hakuna ambaye amewaki kukamatwa wala kuhojiwa ukiachia mbali kupiga kelele na hatimaye kunyamaza? Nani mara hii haoni madudu ya waziri wa sasa wa Nishati na naibu wake walivyotaka kujipatia pesa kwa kisingizio cha kuwahonga wabunge wapitishe bajeti yao ya kimazabe? Na tunaambiwa wamekuwa wakifanya hivyo kwa muda mrefu. Nani kasahau utengaji wa mabilioni ya shilingi kila mwaka kukarabati ikulu? Je ni ikulu gani hii inayokarabatiwa kila uchao utadhani tunaishi mwisho wa dunia kwenye mabarafu? Hapa hatujaongelea nyumba za umma zilizonyakuliwa na wakubwa.

Ajabu katika bajeti ya bajeti ya wizara ya Ujenzi ya 2011/2012 huu shilingi 1,899,600,000 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi za majaji wakati shilling 949,800,000 zikitengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za OCD, DSO, DAS na DMO kwnye wilaya sita! Je kwa uhaba wa namna hii wa nyumba nini mantiki ya wakubwa kugawana nyumba za umma?!

Ajabu ya maajabu hakuna anayeulizia mantiki ya kujenga nyumba nyingine wakati zile za umma ziliishia kugawanwa na wezi fulani wenye madaraka! Hapa hatujaongelea wizi wa iliyokuwa benki ya taifa ya NBC au wale majambazi wa Net Group Solution walioshirikiana na wezi wetu kufilisi TANESCO. Badala yake tunaendelea kuugeuza mgao na kulanguliwa umeme na mafuta vitu vya kawaida ambavyo hatuna budi kuishi navyo na kuvizoea! Shamba la bibi bila shaka. Nani kamroga nani na lini na hadi lini? I have no idea.

Kwa ufupi, ukiamua kuorodhesha wizi uliofanyika nchini kwa miaka kumi, unaweza kujaza msahafu. Pia utagundua kuwa nchi yetu ni tajiri wa kutupwa yenye kutawaliwa na wezi wa kutupwa kwa kutengeneza maskini wa kutupwa wanaounga mkono wizi huu wa kutupwa.

Turejee kwenye kashfa na ujambazi wa UDA. ATC imechezewa, TRC kadhalika. Je wabunge wataishia kupiga kelele na kujinyazia au kunyamazishwa au watafanya kweli kama walivyofanya kwenye kashfa ya Richmond? Je spika wa sasa ambaye ameonyesha anaegemea upande gani atawawezesha kushughulikia uchafu huu? Je watuhumiwa ambao ni wazito watatimuliwa maofisini na kuchunguzwa mara moja? Maana wanajulikana na majina yao yametajwa wazi wazi ingawa baadhi yao wameishaanza kuzusha tuhuma kwa waliowatuhumu ili kupoteza muda na kuuchanganya umma usiwashughulikie.

Kama tulivyoanza, swali kuu bado halijajibiwa. Je nchi yetu itaendelea kugeuzwa shamba la bibi wakati waathirika tukiangalia hadi lini? Nani wa kulaumiwa kati ya wananchi wasiochukua hatua na baadhi ya watawala wao wezi? Je uwajibikaji wa wahusika ni kurusha tuhuma kwa wenzao au kujiweka kando ili uchunguzi huru ufanyike? Ni vizuri watuhumiwa wakaanza kujiwajibisha ndipo wanaowatuhuma baada ya kuwatuhumu wao nao wafuatie. Je mamlaka zitaendelea kufumba macho na kuziba masikio kana kwamba hii hujuma haiwahusu? Kazi yao ni ipi kama hatawachukulia hatua watuhumiwa? Tuguswe wapi ndipo tustuke jamani?

Chanzo: Dira ya Mtanzania Agosti 11, 2011.

No comments: