How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 31 October 2012

Mpayukaji ajiteka ili kuwapakazia ndata

BAADA ya kuona kundi la Uangusho kule Zaainzibaa likimwaga cheche na kupata maujiko huku SZM ikiwafumbia macho ikidhani wataufumuua muunganiko, mzee mzima Alhaji, Dk., Professa, Lt Col. Father, mtaalamu wa kuongea na majini, Mpayukaji Msemahovyo Waambie niliamua kujiteka ili kuanzisha vurugu ambazo nilidhani ni ukombozi wa walevi.
Nilipoona wabangaizaji kama Ismi Juha, Shehena Fuad na Tapeli Pondwa wakipata ujiko hata ulaji nami nikaona nitie guu. Ningeachaje kufanya hivyo wakati nina usongo na nambari kwani ukiachia mbali kuweza kupata wachukuaji waitwao wawekezaji wanaoweza kudhamini fujo zangu ili walevi wapigane nao wavune mali zao? Kwa wasiojua gemu zima wajiulize kwanini DRC imo msambweni? Madini wanangu. Kwanini Mashariki ya Kati imo motoni? Wese wanangu.
Kwa vile na kaya yetu ina madini na imegundua miwese mingi, lazima tulianzishe ili tupate washitili wa kula nao kwa ulaini. Unadhani ulaji mchezo?
Pia kufeli na uroho wa wanasiasia kula peke yao kumetufanya nasi kuona tunaweza kutumia nyenzo yoyote kuanzia bangi, kahawa, dini, hata jinsia kupata ulaji.
Hivyo kesho mkiona bi mkubwa wangu akiingia na chama chake cha Wanawake na Maulaji (WEMA) au Equal Oportunities for First Ladies (EOFL) msishangae, ni mambo ya ulaji.
Twende kwenye dili. Baada ya kuona napiga mikelele kwenye kijiwe na walevi hawapati somo, niliamua kujiteka na kutangaza kuwa nimetekwa na ndata ili walevi waamke na kupambana na ndata hata kuwanyotoa roho kama yule wa kule Zenj alivyofanyiwa na wahuni wa Shehena Fuadi.
Ili kuwapata walevi waliochoshwa na kutolewa chochote na ndata, niliwaambia kuwa badala ya kupigana na ufisadi huu wa ndata, tuanzishe vurugu kudai kuwa mfumo wa maisha wa walevi ndiyo unaopaswa kuendesha kaya. Kama Shehena wa Kupondwa Pondwa nilikuja na mkakati wa kudai kuwa walevi tunaonewa. Badala ya kulaumu ulevi na bangi zetu, nilitupia kila lawama kwa ndata na lisirikali.
Na walevi nao kutokana na ulevi na bangi zao si walikubaliana na mahubiri yangu ya ngoa na usongo. Ila kwa vile walevi ni walevi na hawawezi kuwavaa ndata, niliona nibuni njia nyingine ya kuwaamsha wapambane na ndata. Siku ya siku niliondoka zangu home na mshirika wangu wa bedroom tukiwa tunaendesha baiskeli yetu.
Nikiwa naendesha tulijadili mpango mzima na bi mkubwa wangu. Tulikubaliana kuwa baada ya kujiteka na kwenda kujificha kwenye kijiwe cha Uswekeni, baada ya siku tatu nijitokeze kama aliyeachiwa. Uongo tuliotunga ulisema hivi: Tulipofika mitaa ya Usiniulize, nikamwambia bibi mkubwa aondoke zake. Kwani nilikuwa na miadi na Mgoshi Machungi na maongezi yetu yangechukua muda mrefu.
Hivyo, bi mkubwa alipaswa kuondoka ili awahi naye kwenye miadi yake na shoga yake Salmi Kikwekwe ili ampe mbinu ya jinsi ya kutumia NGO yake kutengeneza ulaji hapo baadaye. Baada ya bi mkubwa kuondoa baiskeli niliingia zangu kichakani kuchimba na kupanda dawa. Wakati narudi si ndata wakaniteka kwa siku tatu!
Ilibidi nifanye haraka kujiteka na kujitokeza hasa baada ya kugundua kuwa kumbe na Shehena Pondwa naye alikuwa amelianzisha ili apate ujiko. Hivyo sikutaka amalize ujiko peke yake. Ilibidi nijiteke ili ukombozi upatikane ingawa niliishia kukumbwa na kesi ya jinai.
Baada ya kujiteka si mambo yalitibuka baada ya walevi kuingia mitaani na kuzidiwa nguvu na ndata. Isitoshe kuna walevi wenzetu waliostukia mpango mzima na hivyo kuupinga wazi wazi jambo ambalo lilinimaliza nguvu nikaamua kutoka nilikokuwa nimejificha kwa aibu.
Pamoja na dili langu kubuma nimejifunza mambo mawili matatu. Ukitaka kujulikana kwenye kaya yetu fanya fujo ukamatwe na ndata. Amini usiamini utapata majuha wengi wa kukuunga mkono kwenye kila bangi utakayokuwa ukiipigia debe.
Pia nimegundua kuwa walevi wengi wana hasira hasa baada ya kunyonywa sana na mafisadi. Ingawa wameshindwa kupambana na mafisadi mmoja mmoja au wote kwa pamoja kutokana na woga, wakipata mtu wa kuwachochea kumbe wanaweza kuwa vifaa huko tuendako!
Pamoja na kuwa na hasira, walevi pia wana kisasi na mafisadi, sema hawajui kupambanua nani wa kushughulika nao kwanza. Mfano mzuri ni juzi tu walipoamua kutaka kupambana na ndata wakati adui wao mkubwa ni mafisadi. Mara hii mmesahau mafisi kama Eddie Ewassa wanavyogawa mifweza ya wizi kwa vijiwe mbalimbali! Hawa ndio wa kufa nao badala ya ndata wasio na tofauti na mbwa na amfugaye.
Pia nimejifunza kuwa hata mafisadi nao hawana mikakati ya kuona mbali. Wakibanwa mbavu wanahaha na kuparaganyikiwa kama jamaa zangu waliofungulia masoja kwenda kufanya kazi ya ndata. Kwanini nasema hivi? Hebu angalia jinsi ambavyo akina Shehena Fuadi na Pondwa Pondwa walivyowajambisha ndipo wakakumbuka kufunga eti vyombo vya umbea vilivyokuwa vikitumika kuhubiri chuki na ngoa.
Kwani hawakujua kuwa vyombo hivi vya udaku havikuanzishwa kuelimisha na kuiburudisha jamii zaidi ya kuichafua, kuijaza ujinga na kuihuzunisha. Hawa jamaa nao wamezidi kwa ujuha na kujisahau.
Unakumbuka wakati wa Ben Tunituni bin Makapu alisemaje vyombo vya umbea vilipombana kuwa alikuwa fisi na fisadi? Aliviambia kuwa kama navyo si fisadi vieleze vilipokuwa vimepata mitaji ya kuanzishwa.
Sasa hawa jamaa walipoona vyombo hivi vya umbea vinahubiri maangamizi, wao wakatumia vyao kuhubiri chuki dhidi ya vyama vya upingaji.
Ngoja nirejee kwenye kisa changu cha kujiteka na kudai nimetekwa. Kwa ufupi ni kwamba nimejilaumu baada ya kugundua kuwa kumbe mambo si rahisi kama nilivyodhania. Pia niligundua kuwa kumbe si walevi wote wanaoniunga mkono. Hata hivyo, sitachoka.
Kama watafanya mchezo kama walivyofanya kwa kufanya mambo kwa nguvu ya soda, nitakuja na mikakati mikubwa ya kuchukua kaya kwa njia yoyote bila kujali kama ni halali, haramu, salama ama hatari. Walevi kaeni mkao wa kuliwa kama hamtajifunza kutokana na haya yaliyopita.
Naona gari la Jei Wii. Acha niishie wasije kunikamata kwa uzushi wangu! Hivi kunguru na mwewe nani kiboko ati? Acha nijikate kabla ya kunikamata na kuninyoa madevu yangu kama yule jamaa!
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 31, 2012.

No comments: