The Chant of Savant

Saturday 20 October 2012

Serikali inamdanganya nani kuhusu mihadhara

    
   Hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Saidi Meck Sadiki alikaririwa akisema kuwa serikali imepiga marufuku mihadhara ya kidini inayokashfu dini nyingine hadi hali itakapotulia. Mihadhara hii imekuwa ikiendeshwa na kushabikiwa na waislam hasa wa kada ya chini hasa wasio na elimu ukiachia mbali kudhaminiwa na wafanya biashara wengi wenye asili ya kiarabu. Huu ni upuuzi. Kwanini kuipigia mihadhara marufuku hadi hali itakapokuwa shwari wakati wameishakiri kuwa inakashfu dini za wengine? Kinachokera ni kwamba hawa wanaojifanya wahubiri hawana elimu si ya Ukristo wala Uislam bali njaa na kutafuta sifa. Kuna haja ya kufanya mihadhara kuwa kosa la jinai hasa wahusika wanaposhambulia dini nyingine au kutokuwa na elimu juu ya kile wanachohubiri.
        Hii imekuwa staili ya serikali yetu ya nguvu ya soda katika kupambana na matatizo. Leo tunaambiwa hata Serikali ya  Mapinduzi Zanzibar (SMZ) nayo imepiga marufuku mihadhara ya wana Uamsho. Too late. Mwanzoni chini ya kihoro cha kutaka muungano SMZ iliridhia na hata kushirikiana na Uamsho kuhubiri chuki na dhihaka dhidi ya muungano ikidhani ingeweza kuwatumia kufikia ajenda zake bila kujua kuwa nao walikuwa na ajenda zao fichi. Maalim Seif Shariff Hamad alipigia upatu hili . Kwani hii imekuwa ajenda yake tangu akiwa CCM hata baada ya kufukuzwa CCM na kurejea kwa mlango wa nyuma chini ya kisingizio cha serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) ambayo hata hivyo inamhusu yeye na si chama chake. Leo wamegundua janja ya kutumiana wanaamka na kuanza kupiga mihadhara marufuku. Yote hii ni matokeo ya kuwa na watawala wasioona mbali.
           Hakuna anayehitaji mihadhara katika maisha. Mbona mihadhara imeanza juzi juzi miaka ya 90? Mbona kabla ya hapo tulikuwa tunaheshimiana na kupendana. Kesho wataibuka wahubiri wa mihadhara wa Kikristo waanze kuonyesha udhaifu wa Uislamu na waislamu wataanza kuja juu na kuchoma makanisa kutokana na kutokuwa na subira. Je namna hii tutafika? Maana kila dini ina udhaifu wake. Ndiyo maana dini zote hupenda kuwaaminisha watu badala ya kuwaelimisha. Hivi kwa mfano mtu leo akija anaongelea maisha ya Khadija mke wa kwanza wa Mtume aliyemwamuru Mtume amuoe si watu mtakatana shingo bure?
            Wengi wa waendesha mihadhara ni watu wasio na kazi ambao kimsingi ni wanyonyaji. Hata Uislam kama utatafsiriwa vizuri unazuia ujinga huu. Sayydina Omar ibn Al- Khatab Khalifa wa pili alipiga marufuku watu kumaliza salat na kuendelea kupiga mdomo wakiswali taraweh badala ya kwenda kufanya kazi.
Ila baada ya Tanzania kuruhusu utapeli wa kutumia majoho ya dini, tumeshuhudia kuibuka utitiri wa mihadhara na madhehebu ya kikristo mengi yakiendeshwa na matapeli wanaotaka utajiri wa haraka.
Je serikali inamdanganya nani zaidi ya kujidanganya na kulea huu uhuni usio na faida kwa watanzania?

No comments: