Tuesday, 27 May 2014

Kikwete ananufaikaje na walioghushi?JAPO vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele kuwaumbua na kuwashupalia wazito walioghushi, serikali imekuwa mstari wa mbele kuwakingia kifua kwa sababu izijuazo.Baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu wamefikia hata kuandika vitabu kuwafichua wakubwa walioghushi vyeti vya kitaaluma. Mmoja wa wanaharakati aliyeweka uovu huu wa kiakili kwenye maandishi ni Keinerugaba Msemakweli ambaye ameishaandika vitabu viwili kuhusiana na kadhia hii akiwataja mawaziri William Lukuvu, Mary Nagu, Makongoro Mahanga na Mathayo Mathayo.
Wengine waliotajwa ni mawaziri wa zamani Emmanuel Nchimbi na Deodorus Kamala ambaye baada ya hapo aliteuliwa Balozi nchini Ubelgiji anakoendelea kufanya kazi licha ya kutuhumiwa kutenda kosa la jinai.
Pia wamo wabunge Victor Mwambalaswa, Samuel Chitalilo, Raphael Chegeni kutaja kwa uchache.
Mbunge wa Ole, Rajabu Mohamed Mbarouk (CUF) ndiye aliyemtoa paka kwenye fuko alipoliambia Bunge, “Suala la vyeti feki ambalo Baraza la Mitihani la Taifa ndilo lenye dhamana na jukumu la kuhakikisha halitokei katika taifa limeonekana kama suala la kawaida. Vyeti feki ni vingi kiasi kwamba linasababisha kuajiriwa kwa watendaji ambao ni feki na mawaziri mizigo.”
Japo alichosema mbunge si kipya, inafurahisha kuona kuwa hata wabunge japo si wote wameanza kukerwa na kadhia hii.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (CHADEMA) aliyejipatia umaarufu kwa kuukabili uoza vilivyo alikuwa na haya ya kusema, “Hawa watu tuko nao humu ndani hawajakanusha, ndiyo maana tuna mawaziri mizigo kwa sababu wana vyeti feki. Serikali isiwe na kigugumizi hawa watu waonekane hapa hadharani.”
Msigwa licha ya kuwashukia walioghushi, anafahamika jinsi alivyomshukia hata anayewalinda, yaani Rais Jakaya Kikwete, ambaye kimsingi amewakingia kifua kwa kuendelea kuwa nao kwenye baraza lake la mawaziri licha ya kutuhumiwa kughushi.
Hivi karibuni Msigwa alikaririwa akiliambia Bunge kuwa wengi wa majangili ni marafiki wa Kikwete. Sasa ameongeza na majangili wengine wa kielimu.
Kama haitoshi, mbunge mwingine, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) Kasulu, aliongeza moto kwenye sakata hili la wale wanaoitwa waheshimiwa kufanya mambo yasiyostahili heshima aliposema, “Kama inafika wakati watu wanataja ni mawaziri na wabunge wana vyeti feki halafu Bunge lako bado linakaa kimya tutegemee watu wataenda kupiga dili huko la vyeti feki.”
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimsingi ndicho chenye watuhumiwa wengi hakikukaa kimya. Kada wake ambaye pia ni waziri wa wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia aliamua kutetea uoza huu kwa sababu anazojua mwenye.
Alikaririwa akisema, “Baadhi yetu si ajabu mnatengeneza vyeti feki. Hata wabunge wapo. Na kambi ya CHADEMA mnaye mbunge ambaye ana cheti feki cha kidato cha nne.”
Ni aibu na hatari kiasi gani kwa waziri mkubwa kama Ghasia kutetea uoza kwa sababu tu unatendwa na wote, yaani chama tawala na wapinzani?
Kwa vile ufisadi na jinai vinaanza kuhalalishwa nchini, waziri hana haja ya kuona aibu. Maana kama kungekuwa na serikali inayowajibika vilivyo Ghasia sawa na wale anaowatetea walipaswa kuwa nje ya Bunge na baraza la mawaziri huku wakikabiliwa na kesi mahakamani.
Lakini hili haliwezekani, hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ya Kikwete imejizoelea umaarufu kwa kuwalinda wahalifu kama hawa walioghushi vyeti ambao wamekuwa wakirejeshwa kwenye baraza la mawaziri na wengine kuzawadiwa uwaziri.
Kimsingi, maneno ya waheshimiwa wabunge ni ushahidi kuwa serikali inajua kila kitu haitaki kuwajibika. Je, serikali inanufaika vipi na jinai hii? Ushahidi kuwa serikali haishughulikii kadhia ya kughushi ni kuwepo kwa mawaziri na wabunge wanaojulikana wazi kughushi.
Pia kitendo cha polisi kubaini watu 212 walioghushi vyeti na kuwaachia kwa kuwafukuza badala ya kuwafikisha mahakamani ni ushahidi tosha kuwa wanaoghushi wako kitanda kimoja na serikali. Je, uzembe huu unalisaidia nini taifa?
Ukiachia mbali mawaziri waliotajwa na Msemakweli, wapo wengine ambao hakuwataja. Hawa ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum ambaye maelezo yake kwenye sifa za kuwa mbunge yana mushikeli.
Pia Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, naye kama bosi wake, maelezo yake yanatia shaka sana.
Mfano, wasifu wa Mkuya unasomeka hivi: Alisomea Shahada ya Master of Finance kuanzia mwaka 2008 hadi 2010 bila kutaja chuo alikosomea.
Alisomea Business Study ngazi ya Advanced Diploma mwaka 1997 hadi 1999, kama ada hataji chuo alikosomea.
Unaendelea kudai kuwa Mkuya alisomea shahada nyingine ya biashara yaani Master mwaka 2000 hadi 2000 bila kutaja chuo. Si hilo tu. Wasifu unasema kuwa badala ya kupata shahada alipata cheti! Pia wasifu wa Mkuya hauonyeshi kama ana shahada yoyote ya kwanza.
Wasifu wa Malima nao ni mauzauza matupu kama bosi wake. Unasema, alimaliza kidato cha nne mwaka 1982. Baada ya hapo yaani mwaka 1983 alikwenda Cuba kusomea shahada ya pili bila kuwa na hata cheti cha High School au shahada ya kwanza. Vipi?
Hakuna nchi duniani inaweza kuruhusu mtu aliyemaliza kidato cha nne kusomea shahada ya pili hasa nchi yenyewe inapokuwa na utaratibu wa kusoma kidato cha tano na sita. Hata kwenye nchi ambapo mtu humaliza kidato cha nne na kuingia chuo hazina utaratibu wa kuruhusu wanaomaliza kidato cha nne kusomea shahada ya pili.
Je, Malima alitumia miujiza au mbinu gani kuvunja kanuni hii? Anatokea Tanzania nchi ambayo elimu yake iko ICU kama walivyosema waheshimiwa wabunge hivi karibuni.
Wakati umefika wa kumwambia Rais Kikwete aache kuigeuza nchi yetu chaka la uovu. Awawajibishe watu wake wanaotuhumiwa kughushi hata kama ni marafiki na washirika au watoto wa rafiki zake.
Kwanini rais amejiruhusu kuwa mhimili wa maovu kuanzia ujangili, kughushi, ufisadi, mihadarati, ujambazi na mengine mengi?
Chanzo: Tanzania Daima Mei 28, 2014.

No comments: