The Chant of Savant

Wednesday 21 May 2014

Nape: Nyani haoni nonihino lake


           Kwa wanaomjua Nape Nnauye licha ya kuwa mtoto wa kada wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Musa Nnauye, Nape amerithi kiti baba cha yake cha ukatibu uenezi wa taifa wa CCM sawa na wateule wengine waliorithi viti vya baba zao vya ubunge kama Ridhiwan Kikwete, Adam Malima, Godfrey Mgimwa, Hussein Mwinyi na January Makamba na Emaunel Nchimbi ambao walitumia umaarufu wa baba zao kufikia walipo na warithi wengine wengi. Pia Nape ni mtoto aliyezaliwa ndani ya ulaji wa kujuana wa CCM sawa na watajwa wenzake. Ni bahati mbaya kuwa ulaji huu umemlevya kiasi cha kujiona bora asijue kuwa anatumiwa tena vibaya. Inshangaza kuona kijana kama huyu ambaye anapaswa kuangalia mbele, kuishi kwa bora liende kwa siasa za maji taka.
Yote tisa. Nape amejipatia umaarufu tokana na wepesi kubwata kila anapotumiwa. Waingereza humuita a lap-turned-toothless-barking dog yaani mbwa mpakatwa aliyegeuka mbwekaji lakini asiyeuma anayetumiwa na top dog kwa tafsiri isiyo rasmi. Pamoja na kujinadi kuwa ana shahada ya uzamili, maneno na matendo yake yanajenga shaka juu ya ithibati na ukweli wa elimu yake.
Nape alijizolea umaarufu pale alipotumwa na kutumiwa na rais Jakaya Kikwete kuwatolea uvivu akina Edward Lowassa na Andrew Chenge tokana na kutuhumiwa ufisadi kabla hajachomoa na kunywea baada ya wahusika kujibu mapigo pale alipowaita magamba. Pigo la mwisho la mbwa mbwekaji aliyegeuka kibogoyo tena akaufyata ni pale Chenge alipodai kuwa gamba lilikuwa limekatalia kiunoni. Hivyo, aliyetaka kulivua shurti aje na shoka. Wengi walidhani Nape na waliomtuma wangechukua mashoka na kuyatandika magamba. Lakini wapi! Waligwaya na kufyata mikia huku wakidandia hoja nyingine ili kuficha aibu na unguliko lao.
Baada ya hapo, Nape hakuchoka, alitafuta ulaji mwingine kwa kuwaita baadhi ya mawaziri mizigo katika serikali ya bosi wake. Wengi walidhani kuwa wakati huu lau Nape angefanikiwa na kurejesha heshima yake. Hakufanikiwa tokana na bosi wake kujua ubovu na uhovyo wake kama kifaa kitumikacho hasa kusafisha uchafu. Badala ya kuwawajibisha mawaziri mizigo, Kikwete aliwapandisha vyeo kiasi cha Nape na bosi wake Katibu mkuu wa CCM Abdulrahaman Kinana kuzodolewa na kuonekana mizigo. Wengi walihoji consciousness ya Nape na Kinana kwa kushindwa kujiuzulu baada ya kudhalilishwa wazi wazi na yule aliyewatuma na kuwatumia.
Baada ya aibu na udhalilishaji huu wengi walikosea kudhani Nape angejifunza na kufunga domo lake au kuacha kutumiwa lakini wapi. Hivi majuzi alikaririwa akisema, “Salamu kwa wazee walio katika muda wa jioni na ambao wamekengeuka, hawa wamekula maisha katika muundo wa serikali mbili, sasa wanapoona wanaenda ukingoni ndiyo wanaanza kupiga kelele juu ya serikali tatu. Wamefilisika,” hata kuku pamoja na kujaliwa ubongo mdogo anajua kuwa aliyelengwa hapa ni mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) Jaji Joseph Warioba. Wenye akili wameshangaa kitoto hiki kinapata wapi mshipa wa kutukana watu wenye heshima kuliko hata baba yake. Bila shaka, kama mbwa yeyote bweka, kuna mwenyewe ememwamrisha abweke. Naye kwa kutaka kumridhisha bwana wake inabidi abweke na kubweka lau aonekane anaiweza kazi. Ni utovu wa nidhani usio kifani kwa CCM kuendeleza siasa za visasi, mipasho na matusi tena ya nguoni. Hivi kama ni kuuangalia ukweli na kuusema vilivyo, nani aliyefilisika kati ya Warioba na wale wanaotumia vitoto ambavyo havikupata malezi mazuri kumtukana?
Bahati mbaya wanaomfundisha Nape kutukana wenzake wanasahau kuwa kesho watafunga virago na kuondoka kwenye ulaji ndipo aanze kuwaporomoshea mitusi waliyomfundisha hasa ikizingatiwa kuwa mchumia tumbo huwa hana rafiki bali maslahi. Kuonyesha Nape asivyo na breki alikaririwa akimrushia kijembe bosi wake aliposema, “Watalipwa fidia sawa, ila wamepoteza muda na sijui mawaziri wanaohusika wamefanya nini. Sisi chama tunapowaita kuwa ni mizigo wanatuchukia, lakini katika mazingira kama haya utawezaje kukwepa kuitwa mzigo?” Ni uhondo ulioje mzigo kuita mzigo mwenzake mzigo au ngamia kumcheka nundu ng’ombe? Hivi kama si CCM kuishiwa uongozi, busara na maarifa kuna mizigo mizito na michafu kama Nape na Kinana? Rejea Kinana alivyotuhumiwa kusafirisha nyara za taifa na akajikausha kana kwamba hakusikia. Nape anajulikana alivyo mzigo si kwa CCM tu bali hata kwake binafsi. Maana kwa umri na usomi wake   (kama anao kweli) alipaswa kuwa na angalau common sense kusoma alama za nyakati na kufanya maamuzi mazito kwa kuheshimu ukweli usiofichika kuwa hata hao anaowatukana kwa kuja na katiba kielelezo ya wananchi hawana makosa bali waliwasilisha mawazo ya umma, walatini walisema Vox Populi Vox Dei yaani sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Bila shaka Nape na wenzake wangeliona hili lisilohitaji kuwa na shahada lukuki za sayansi ya siasa kulienga.
Inashangaza kuona Nape akiwatupia vijembe na mipasho akina Warioba kuwa walifaidi vinono vya serikali mbili na sasa wamekengeuka. Heri yao walitoa jasho wakala walivyokula kuliko Nape anayevuna ambapo hakupanda. Kama si ukubwa wa jina la baba yake na mfumo mfu na mchafu wa kujuana nani angejua kuwa kuna kiumbe duniani anaitwa Nape au wale tuliowataja hapo juu? Ama kweli wahenga walisema: Nyani haioni Nonihino lake. Wote wangesema lakini si Nape wala wale walio kwenye ulaji kutokana na kubebwa na majina ya wazazi wao. Kama kuna mizigo basi ni hii ambayo umma unaibeba kama makandokando na mabaki ya wazazi wao.
Tumalizie kwa kulaani kitendo cha Nape na wale wanaomtuka kumkosea heshima mzee Warioba. Wanapaswa kushambulia hoja zake na si yeye binafsi kama mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba. Hakika alijisemea Eleanor Roosevelt,“Great minds discuss ideas; Average minds discuss events; Small minds discuss people.”
Chanzo: Tanzania Daima Mei 21, 2014.

1 comment:

Anonymous said...

Nape ana nini
Futari ya bwana huyo