Saturday, 31 May 2014

Mlevi amshangaa mheshimiwa bwege

Mbunge wa Kilwa Kusini Selemani Ally Bungara aka Bwege
         Hivi karibuni mlevi ataingia kwenye majarida ya uvumbuzi ya kaya kwa kuwa msomi wa kwanza kugundua chanzo cha mipasho mjengoni. Nisingekuwa nimeishapata PhDs zangu ningefanya uvumbuzi huu kuwa thesis au tasnifa ya andiko langu.
Jamani sizushi. Msidhani hangovers za gongo na “hangunders” za bangi vinanisumbua hadi kuwakosea hishima waishiwa wahishimiwa wasio na hishima. Hakuna kitu kilikuwa kinanisumbua kama kitendo cha kutamalaki mipasho matusi hata vijembe na taarabu mjengoni kuanzia mjengo mkuu hadi ule wa Katiba na constitution ya constipation.
Katika utafiti wangu niligundua kuwa kumbe nilikuwa nakosea katika kuangalia watafitiwa wangu vizuri kwa kuogopa kuvunja kile ambacho watafiti huita Nuremberg Code ambapo mfanya utafiti anabanwa asimfiche wala kumfanyia upepelezi mtafitiwa au kumtenza kama kitu au mnyama. Mambo ya kitafiti na kisomi tuyaache. Maana huwa yaboa tu.
 Hivyo, juhudi zangu za kujua ni kwanini mijengo yetu imegeuka vijiwe vya mipasho na upuuzi mwingine ziligonga mwamba hasa kuogopa kuwapeleleza waishiwa wahishimiwa.  Hata hivyo, bwege mmoja alinisaidia kugundua kuwa kumbe ubwege ni sababu mojawapo. Kwa lugha ya kawaida ni kwamba kuna mabwege wengi mijengoni kiasi cha kutamalaki mambo ya hovyo ambavyo, mara nyingi, huthibitisha ubwege wa wahusika. Msidhani natukana. Ninachofanya hapa ni kutoa uchambuzi wa kitaalamu na kilevi ili waathirika wagundue chanzo cha masahibu yao kiasi cha kuishia kushuhudia maigizo runingani huku waigizaji wakiwa mabwege mjengoni.
Punde si punde nilipata clue nyingine toka kwa naibu microphone Jobless Nduguy alipodai kuwa mjengoni kuna waishiwa wanavuta mibangi na kubwia mibwimbwi. Hiyo ni clue ya kwanza tena toka kwa mwenzao na kiongozi wao.
Juzi nilipata lead nyingine toka mjengoni kwenye kile ambacho wamasai huita from the horse’s mouth. Nilimsikia mwenyewe mjengoni muishiwa mhishimiwa mmoja kutoka kusi tena kisiwani akimtishia waziri maji. Du nimesahau! Naibu kipaza sauti si alimuuliza jina lake. Naye akaijibu, “Mimi naitwa Sele Seydou Ali Bunga’ Bwegee!” Alijibu hivyo mara tatu kuonyesha kuwa hatanii.  Baada ya kusikia hivyo nilisikia mkota mmoja akisema, “La haula wala quwata illa billah! Si heri mngejaza walevi na wavuta bangi mjengoni kuliko mabwege.”
Baada ya bwege kukiri kuwa ni bwege tena maarufu, Mlevi niligundua kuwa kumbe kuna mabwege wengi. Wapo mabwege wanaotishia kwenda mwituni wakati wanasifika kwa kuuchapa usingizi mjengoni tena kibwegebwege huku midomo ikiwa wazi na udenda ukiwatoka. Wapo tena mabwege wanaotishia walevi kuwa wasipokubaliana na upuuzi wao ndutu zitachukua kaya.
Pia wapo mabwege wanaosifika kutoroka vikao mjengoni huku wakijidai wanawawakilisha walevi. Kama si ubwege nini kwa mwakilishi kukosekana pale anapopaswa kuwa kuwawakilisha anaodai kuwawawakilisha? Mabwege wengine ni wale wanaounga mkono kila upuuzi simply because sirikali inayotawala ni ya chata lao. Mabwege wa namna hii wanashindwa kuchagua baina ya wale waliowapa kura ya kula na hicho kijichama.
Orodha ya mabwege ni kubwa tu. Wapo mabwege wanaolilia kuitwa wahishimiwa hata kama wanayofanya hayastahili hishima.  Mkinichagua mie kwenda kuwawakilisha mjengoni kitu cha kwanza nitakataa kuitwa mhishimiwa. Nitapenda niitwe ndugu kwa vile mimi ni ndugu yenu wala si mkoloni wala mpenda sifa wala bwege. Mie ni mlevi, finish. Mabwege wengine ni wale wanaocheza makidamakida mjengoni kwa kuwaita wenzao Boko Haram. Sijui wanafanya hivyo kwa sababu wanaongozwa na makidamakida au wasanii?
Mabwege wengine ni wale waliostukiwa hivi juzi kuwa wameghushi vyeti vya kitaaluma. Ni ubwege kiasi gani kwa mtu kuogopa umande halafu akajiita msomi wakati usomi wenyewe ni wa kughushi. Mabwege hawa wana bahati. Kwani kuna mabwege wakubwa wanaowakingia kifua pamoja na kutuhumiwa miaka mingi iliyopita.
Aina nyingine ya mabwege ni ile iliyoingia mjengoni kwa njia haramu kama vile kupata umaarufu kutokana na ukoo au madhehebu yake ya mfukoni. Ni ubwege kiasi gani, kwa mfano, kuchanganya dini na siasa au udugu na kazi za umma? Je hatunao mabwege waliomo mjengoni simply because ni watoto wa wakubwa fulani au waliongia kwa mchongo fulani?
Mabwege wengine ni wale waliosimikwa pale kufanya kazi moja tu, kutetea fisadi kama dada yangu Annae cheza Makidamakida aliyesimikwa na mafisadi baada ya kumwengua rafiki yangu Sam Sixx baada ya kumsulubu Eddie Luwasha na Richmonduli yake.
Mabwege wengine ni wale wanaokaa upande mwingine wakatoa majibu ya kipuuzi kwa maswali muhimu ya waishiwa mjengoni. Bwege mmojawapo ni Sossie Muongo aliyelipuliwa na David Kafulia kuwa yeye na wenzake waliiba njuluku za walevi halafu badala ya kujibu tuhuma akaanza kudai eti wabaya wake wanazua ili kumng’oa. Prof mzima anakuwa muongo kiasi cha kujikuta kwenye kundi la mabwege mjengoni!
Makala hii haiwezi kuisha bila kuwataja mabwege wanaoongea kiswangilish mjengoni wakati hawajui chochote si kitasha wala kiswazi bali usanii mtupu. Hivi ni ubwege kiasi gani kwa mtu anayedai kuwawakilisha awawakilishao kutumia lugha wasiyoelewa? Anadhani nao ni mabwege kama yeye washobokee lugha za watu?
 Napiga picha nikiitwa na kipaza sauti au naibu wake akiuliza jina langu nami najibu profesa Mlevi mkuu kutoka Ukanadani. Naona yule anatikisa kichwa kudhani kuwa sifai kuwa mjengoni kwa vile ninaishi kwa mibangi gongo na madude mengine yanayowanyotoa roho walevi. Heri walevi wanaolewa kama komba kuliko mabwegwe wanaobwabwaja na kufanya mambo kibwegebwege kama kupashana na kutukanana au kuuchapa usingizi.
Sikuamini mjengoni kunaweza kuwa na bwege hata mabwege wengi tu. Sijui mna mabwege wangapi mjengoni hasa nikiangalia mambo ya kibwegebwege yanayoendelea humo?
Tumalizie kwa kuwasihi mabwege wanaochagua mabwege kuacha ubwege wa kuchagua mabwege ili wakafanye mambo ya kibwege kiasi cha kaya yetu kuonekana kaya ya mabwege au kila mwandishi mmoja aliita pepo ya mabwege.
CHANZO: NIPASHE 

No comments: