The Chant of Savant

Tuesday 22 July 2014

Kijiwe chajadili ubaguzi juu ya urais

BAADA ya vitimbakwiri kujitokeza bila aibu na kutaka kuwania urais, Kijiwe kimeona kisiachwe nyuma. Maana bila ya ushauri wake rais ajae anaweza kuwa rahisi tena na kaya ikaingia kwenye hasara zaidi ya hii tunayoshuhudia.
Mpemba anaingia akiwa na gazeti la Danganyika Always. Baada ya kuamkia anamtania Mgosi Machungi akisema; “Mgosi naona sasa mwapania kuchukua hata sirikali.”
Mgosi Machungi anajibu; “Wamaanishani mbona hatikueewi yakhe?”
Mpemba anakula mic tena. “Namaanisha huyu mwana wa Mgosi mwenzio atakaye kuwania urahisi. Hii maana yake ni kwamba ataka kuchukua sirikali huku babake akiwa ndiyo ameachia chama.”
Mgosi anajibu; “Alaa kumbe! Unamaanisha huyu kifaanga anayejifanya jogoo hata kabla hajabaehe siyo? Atawezaje kuwa mkuu wakati ni mbaguzi hivi?”
Mipawa anachomekea; “Hata mie namshangaa huyu kifaranga ambaye tunaambiwa amesoma majuu, lakini asionyeshe usomi wake. Haiwezekani mtu mwenye elimu tosha ya kweli akaongea upupu na utumbo kama huyu kifaranga ambaye anaturejesha kwenye ukaburu wa ubaguzi. Anadhani ubaguzi wa umri si ukaburi siyo? Huyu hafai hata kuwachunga mbuzi achia mbali kuongoza watu.”
Msomi aliyekuwa akisoma jarida la The Mail on Wednesday analiweka kando na kupoka mic. “Sidhani kama huyu dogo amesoma kweli. Maana nasikia alighushi hata kuingia kidato cha tano na sita na baada ya kumaliza baba yake alimkimbizia kwa Joji Kichaka akaja na shahada za urongo na ukweli. Kimsingi, huyu ni bomu. Hivi ukiondoa jina la baba yake ana sifa gani nyingine ya kustahili hata kuwa balozi wa nyumba kumi? The boy is a wino who’s drunk a lot from the cup of power. Now he’s vomiting on us to prove how drunkard the simian is.”
“Msomi punguza kikameruni hicho. Najua ukikasirika huwa kinatoka chenyewe.” Anaonya mzee Maneno ambaye kimombo huwa hakipandi.
Sofi Lion aka Kanugaembe anaamua kutia guu; “Hivi nyie watu mna matatizo gani?”
Kabla ya kuendelea Kapende anamjibu kwa dharau; “Kwani wewe huna matatizo? Ungekuwa huna ungekuwa kanunga dada yangu?”
Sofi kashikwa pabaya! Anaamua kupayuka; “Kuishiwa hoja ni kujadili mambo ya mtu binafsi badala ya masuala. Sasa ununga na urais vinaingilianaje?”
“Ahaa, kumbe hujui! Hivi huyu kifaranga anayekuja na gea kuwa rais ajaye awe kijana anajadili nini kama si watu binafsi? Nani anahitaji ujana au uzee zaidi ya uadilifu, uzoefu, hoja, sera na mipango madhubuti ya kukomboa kaya?”
Bwege hangoji wamalize utamu. Anakula mic; “Huyu dogo bomu kweli kweli. Kama ni ujana mbona yeye bado mtoto? Maana tuliambiwa kwenye uchakachuaji uliopita kuwa Njaa Kaya alikuwa kijana akiwa na umri wa miaka 55. Hivyo basi mwenye miaka chini ya hapo ni mtoto na hafai kuwa rais.”
Msomi anarejea; “Tuache utani. Mie nilishangaa usomi wa huyu kifaranga pale nilipogundua kuwa anataka kutumia turufu ya ujana bila kuangalia uzee wa chama chake. Huyu kweli ni msomi asiyeweza kufanya analysis ndogo kiasi hiki? Nadhani waliomtuma wanapoteza muda kwa vile tunajua kuwa huyu dogo hana lolote zaidi ya kusukumwa na ukubwa wa jina na mitandao ya baba yake ya kifisadi.
Hivi ukimvua jina la baba yake anabakia nini? Nilicheka nilipomsikia RizOne eti naye anataka atupangie sifa za nani anafaa kuwa rais. Yeye kama mfugo anawezaje kujua anayetufaa wakati amebebwa na jina kama Jan Makambae?”
“Nyie hamjui. Huyu dogo kimsingi hadhamirii kuwa rais. Anachofanya ni kutaka akae pale kama kikaragosi halafu baba yake, Njaa Kaya na mafisadi wengine wawe wamamchezesha kama Joyce Wowowo. Nani anataka rais kama huyu asiyeweza kujisimamia? Ajabu eti anajilinganisha na Obamiza ambaye kabla ya kuchaguliwa alishafanya makuu mengi.” Anazoza Kapende.
Mijjinga anamnyang’anya mic; “Huyu ndama haishii hapo. Eti anajilinganisha na mzee Mchonga kwa vile alipata uwaziri mkuu akiwa kijana. Ila anasahau kuwa mzee Mchonga alikuwa ameiva kutokana na kupigania uhuru wa kaya tofauti na yeye aliyelelewa na kupendelewa na mfumo wa kifisadi hadi akapanda haraka na kujikuta hapo alipo bila kujifanyia lolote.
Huyu dogo anadhani watu wote ni wajinga na wasahaulifu kama yeye? Hili la RizOne wala sitaki kuliongelea. Kama alivyosema mheshimiwa hapo, huyu ni mfugo sawa na huyu ndama. Ndama ni ndama tu.”
Kanji aliyekuwa kimya anaamua kukatua mic; “Hata mimi ona kweli. Hii toto hapana faa kuwa rais. Kwanini rais jana chama zee?”
“Du kweli wakati mwingine haramu haijifichi. Hata Kanji umeliona hili ambalo dada yako Sofi hataki kuliona!” anachonga Kapende.
Mgosi Machungi naye anakatua mic; “Mwenzenu kwetu Mashindei kwenye jimbo la Bumbui. Tina shida Mungu anajua. Tangu tikosee na kumpa kula huyu ndama, tinajuta.
Ameshindwa kutatua matatizo yetu ataweza ya kaya huyu au ametumwa na baba yake tinayemjua aivo bingwa wa kutetea mafisadi kama yue aliyetaka awe mbunge wa Kigaamboniii?”
Kijiwe kikiwa kinanoga si mvua ikanyesha. Kila mmoja alitimka kivyake kwenda kujikinga mvua. By the way, yale maskandali ya UDAA na ESIKROO yameishia wapi?
Chanzo: Tanzania Daima Julai 23, 2014.

5 comments:

Anonymous said...

Maneno haya nimependa sana mwandishi funguka tujuwe mengi
Tumechoshwa na kanga, fulana ,vitenge na kofia na kilo tano za sembe na mchele Nape domo kaya tukusikii NGO mmezoea kununua Watu mkutano yenu tuna kuja sana kwa vile kuna mshiko

Anonymous said...

Jamani mbona mnataka kuziba liziki zetu si madalali wa mikutano ya CCM
Tunavuta milioni kwa siku kwa kuitisha Watu kwenye mikutano ya CCM
Na wanapata mshiko
Jamani si ndo Ali mpya kasi mpya kwa maendeleo ya Tanzania

Anonymous said...

Tunasubiri ya Lowassa na wengine wengi wenye nia ya urais 2015 mambo yote mtaando ni Siri zote tutaanika mtaandoni Watanzania wajue mapema
Na wapiga kura vijana wapo mtandaoni na mtandao ulivyokuwa 2005 Mwakani kazi ipo

Anonymous said...

Leo tutakunywa bure hapa kijiweni kwetu kwa walevi wa busara, wale walevi wa dhuluma, kufikiria kutoka tumboni na mazoea ya uongozi hawana nafasi hapa kwetu.

Haya walevi wote wa busara na maarifa shusheni na kulete vitu vya maarifa ya kilevi kutona kichwani bila kikomo.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon hapo juu nawashukuruni kwa changamoto mlizotoa pamoja na hongera kwa kupitia uzi huu na kuacha nyayo zehu. Mbarikwe sana na karibu sana.