Sunday, 23 April 2017

Barua kwa Ben Saanane

Image result for photos of ben saanane

Mpendwa Ben,
            Nakuandikia popote uliopo; uwe hai au marehemu, najua utasikia. Usiposikia wapendwa wako watasikia ukiachia mbali wanaochukia kile ulichofanyiwa. Sasa ni zaidi ya miezi mitatu tangu umepotea kimiujiza kwenye nchi yenye kila vyombo vya ulinzi vilivyoshindwa kukulinda wewe achia mbali kukutafuta kama siyo kukuhifadhi. Nikinukuu maneno ya Mbunge Zitto Kabwe kuwa ulitekwa na usalama wa taifa bila wao kukanusha, hali inatisha. Kwani tangu utekwe, wengine wametekwa. Hata hivyo, tofauti na wewe, wao walikuwa na bahati. Kwani waliteswa kidogo na kuachiwa. Kama huwajui, acha nikutajie. Waliotekwa ni Emanuel Elibariki aka Ney wa Mitego kwa kosa la kutunga wimbo wa "Wapo" ambao ulikuwa ukilaani jinai ya kughushi vyeti huku walioaminiwa na kutarajiwa kumtumbua wakimkingia kifua. Kama haitoshi, punde si punde mwingine aliyetekwa na utekaji huu kuendelea kuwa kizungumkuti ni Ibrahim Musa aka Roma Mkatoliki ambaye naye alitemwa na watekaji hawa baada ya umma kuja juu.
            Ukiachia watu waliotekwa, yametekwa hata maofisi. Kituo cha televisheni cha Clouds kilitekwa na mtu anayeitwa Bashite akiwa ameandamana na mapolisi. Ajabu ya maajabu, huyu mhuni na mhalifu aliyetenda jinai hii–huwezi kuamini–bado yuko kwenye ofisi ya umma akitanua tokana na kukingiwa kifua na mzito mmoja. Hii itakufanya uelewe ni kwanini suala lako halishughulikiwi. Ni kwa sababu sheria yetu siku hizi inafanya kazi kwa madaraja kulingana na nani yuko karibu au mbali na wakubwa. Kama alivyowahi kusema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ni kwamba wakati baba yako akisema Ben si mbuzi  wala ng'ombe wake bali mwanae aliyepotezwa, wenye madaraka hawakuangalii hivyo.
            Bwana mdogo Ben, hebu fikiria. Hivi kweli unaweza kutendewa haki wakati hata wakubwa waliojaribu kumchunguza, kwa mfano, mkubwa aliyetaka kufichua huu utekaji wa Clouds, aliishia kutimliwa ghafla bin vu kama mhalifu ili kumlinda mhalifu anayejulikana wazi wazi. Hata ndege wanamjua mhalifu huyu hata kama yuko juu.
            Bwana mdogo Ben, huko uliko, kama u mzima au mfu, nakuomba ujue kabisa kuwa kinachoendelea kuhusiana na utekaji nyara wa watu wasio na hatia unaanza kuzoeleka tokana na wanaopaswa kuushughulikia ima kuwa woga au kujidanganya kuwa hakuna mwisho wa uzandiki huu na unyama dhidi ya binadamu. Sijui kama Ben ungekuwa mtoto wa hao wanaowalinda wahalifu wanaoteka watu kutetea uchafu wao wangeweza kujiamini na kuendelea kutenda jinai na upuuzi kama huu. Sijui kama una uraia wa taifa lolote. Kama unajidanganya kuwa unao, jiulize. Kwanini nchi yako haikukutetea? Kwanini nchi yako imeshindwa kutoa maelezo. Kama hujui basi jua. Juzi aliuawa faru mmoja aitwaye John. Dogo, huwezi kuamini. Waziri wa wanyama na hata waziri mkuu hawakukaa ofisini. Ziliundwa kamati na mabilioni ya shilingi kutumika kujua nani au nini kilimuua hayawani huyu. Ajabu ya maajabu, hakuna anayetumia hata senti moja kutaka kujua nani walikuteka, kukuficha, kukuua na vyovyote ilivyo. Mpaka sasa, si wazazi wako, taifa wala yeyote anayejua hali yako zaidi ya waliokuteka na kukuonea tokana na itikadi na msimamo wako.
            Mpendwa Ben,
            Wazazi na wapenzi wako hawalali. Wana hasira na uchungu japo hawana namna tokana na kuogopa. Mimi ninayeandika siogopi kitu. Wapo wanaodhani naandika haya kutokana na kuishi mbali na watekaji. Wanakosea. Hata ningekuwa nchini ningeyaandika haya kutokana na imani yangu kuwa kufa si chaguo bali faradhi. Hivyo, ninapoandika haya, ujue fika ima ni mimi peke yangu niliyeona umuhimu wako au wachache. Najaribu kujiuliza. Ningekuwa wewe au baba na mama yako ningetaka nitendewe au utendewe vipi. Nimevumilia kuona maigizo na kujifanya hamnazo kuhusiana na kupotea kwako. Sasa nimefikia kikomo. Ndiyo maana nimeamua kukuandikia usome au usisome angalau moyo wangu utaridhika kuwa nimetenda haki ambayo nilipenda na nilipaswa kutendewa kama binadamu au kiumbe.
            Ben mpendwa,
            Ninapoandika, naamini haki itatendeka iwe kwa kutaka au kwa kulazimika, uwe hai au uwe marehemu, naamini kuwa ipo siku haki itatendeka. Kwani naamini hakuna lenye mwanzo lisilo na mwisho. Tuliwaona akina Idi Amin, Jean-Bedel Bokassa, Charles Taylor, Saddam Hussein na mahabithi wengine wengi. Je waliishia wapi? Binadamu ni nini hadi ajione wa maana wakati ni udongo tena wa daraja la chini? Binadamu ni nini zaidi ya mavumbi? Wako wapi watu watukufu kama akina Nelson Mandela, Julius Nyerere na wengine waliosifika kwa utauwa na usafi wao? Wamezikwa; na wameoza. Nani huyu atokaye kwenye tumbo na uchi wa mwanamke atakayeyashinda mauti? Nani mpumbavu huyu asiyepoteza muda kupinga na ukweli na kanuni za maumbile? Hata hayawani wasio na akili wanalijua na kulikubali hili.
            Ben Mpendwa,
            Hata kama binafsi sikujui, niruhusu nikuomboleze kwa kukuahidi kuwa haki kwa ajili yako itatendeka siku moja hata kama ni kwa kuchelewa. Damu ya binadamu si maji yamwagwe bila sababu. Uwe unanisikia au la, nasema iko siku milima na mabonde vitaongea kueleza nini kilikupata baada ya vyombo husika kushindwa kutupa jibu la nini kilikupata.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: