Wednesday, 19 April 2017

Punguezeni mikoa na wilaya vilivyoanzishwa kisiasa

       Image result for the map of tanzania
  Hivi karibuni Mbunge wa Nkasi Kaskazini Ally Kessy akichangia kwenye kikao cha bunge la 11 huko Dodoma alitaka rais John Magufuli aangalie uwezekano wa kupunguza utitiri wa wilaya ili kuleta mendeleo katika maeneo mengi ya taifa letu ambayo yako nyuma kimaendeleo. Pia kesi alikwenda mbali kudai kuwa kuna mikoa inayopendelewa kwa kupewa majimbo na fedha nyingine kulinganisha na mengine. Tokana na siasa za majitaka, tanzania kwa sasa inaweza kusemekana kuwa na mikoa na hata wilaya nyingi visivyolingana na uwezo wake kiuchumi. Yote hii ilitokana na baadhi ya viongozi waliopita kuangalia masuala ya kisiasa katika uanzishaji au upanuzi wa mikoa na wilaya. Mfano mdogo, Benjamin Mkapa alianzisha Mkoa mpya wa Manyara ambako anatoka waziri wake mkuu Fredrick Sumaye kwa tangazo la Serikali Na. 367 lililotolewa tarehe 27 Julai, 2002.
            Kikwete ndiye alivunja rekodi kwa kuunda mikoa mingi. Kwani hapo Machi 2, 2012, alianzisha mikoa ya Geita anakotoka rais Magufuli, Katavi anakotoka waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda, Njombe na Simiyu na wilaya Buhigwe, Busega,Butiama, Chemba, Gairo, Ikungi, Itilima, Kakonko, Kalambo na Kaliua. Nyingine ni Kyerwa, Mbogwe, Mkalama, Mlele, Momba, Nyang’hwale, Nyasa, Uvinza na Igwachanya.
            Kama alivyodai mbunge Kessy, ukiangalia ukubwa wa baadhi ya mikoa hata wilaya unashangaa ugawanywaji wake. Nini mantiki ya Mwanza na Shinyanga yenye jumla ya ukubwa wa kilometa za mraba70,876 kugawanywa kuunda mkoa wa tatu wa Geita wakati ukubwa wake ni chini ya ukubwa wa mkoa mfano, mkoa wa Tabora wenye ukubwa wa kilometa za mraba 76,15 au Rukwa wenye ukubwa wa kilometa za mraba75,240 kama si Morogoro wenye ukubwa wa kilometa za mraba72, 939? Kwanini Mkoa wa Geita wenye ukubwa wa kilometa za mraba 21,729 usiunganishwe na Kagera wenye ukubwa wa kilometa za mraba 40,838 Jiulize na kuunda mkoa mdogo kuliko Tabora?  Mkapa alifuata kigezo gani kama siyo kumzawadia rafiki yake na waziri mkuu wake mkoa iwapo mkoa wa kabla ya kugawanywa katika mikoa miwili ulikuwa na ukubwa wa kilometa za mraba
            Kwa mtu anayejua gharama za uendeshaji mkoa na wilaya, asingekubaliana na ushauri wowote wa kuanzisha mikoa minne ndani ya utawala mmoja ukiachia mbali wilaya nyingi. Hata hivyo, kwa wanaojua utawala wa Kikwete ulivyokuwa wa kisanii hawashangai hili kufanyika kiasi cha kuacha wenye kujua mambo wakishangaa.
            Kwa vile, tuna serikali inayotaka kubadili mambo, tungeshauri iangalie umuhimu au ulazima wa utitiri huu wa mikoa. Je wingi wa mikoa na wilaya hizi umeongeza ubora wa maisha ya wananchi au kuwaongezea mzigo wa kulisha wakubwa wachache wanaoteuliwa na rais kuwa wakuu wa mikoa na wilaya?
            Ni bahati mbaya kuwa wahusika walipoanzisha mikoa mipya, walifanya maamuzi ya kiuchumi bila kuzingatia uhalisia wa kiuchumi. Hata bila kuwa mchumi, akili ya kawaida haikubali kuanzishwa kwa mikoa minne kwa mpigo kwa nchi ambayo bado bajeti yake inategemea wafadhili ukiachia mbali kutotekelezwa hata kwa asilimia 50. Hadi sasa ni vigumu kujua mantiki, ujuzi, utaalamu, hata sababu vilivyotumika kuanzisha mikoa na wilaya hivi ndani ya utawala mmoja.
            Pesa zinazopoteza kuwalisha wateule hawa wachache zingeweza kuleta nafuu hata maendeleo kiasi gani kwa sehemu zilizomo hizi wilaya mpya kama zingetumia kwenye mambo ya msingi kama vile miundombinu, huduma za kijamii na maendeleo? Unashangaa utitiri wa wilaya ambazo tena ni majimbo ya uchaguzi. Kwanini zisibaki kuwa majimbo na wabunge wakazihudumia badala ya kujaza utitiri wa wakuu wa wilaya ambao umuhimu wao unazidi kupotea kadri miaka inavyopita?
            Kama tunataka kutenda haki basi mikoa inayopaswa kugawanywa tena si kwa kuungaunga ni kama vile Tabora, Rukwa, Morogoro na Lindi. Hakuna kinachokera kama kugundua kuwa mikoa hii mikubwa si kwa ardhi tu bali hata uzalishaji. Hebu fikiri mkoa kama Lindi na utajiri wake wa gesi asilia, korosho na mambo mengine unaachwa vinagawanywa vipande vya mikoa. Tunajenga picha gani hapa kisiasa? Je hili nalo linangoja upinzani uchukue dola ulirekebishe?
            Hata ukija kwenye ugawaji wa wilaya unashangaa kuona wilaya kama Siha kwenye mkoa ambao ni sawa na baadhi za wilaya za mikoa mikubwa tajwa. Kuna haja ya wabunge na wataalamu wanaotoka kwenye mikoa inayopunjwa kufanya upembuzi na kuja na mapendekezo kwa serikali ili kuhakikisha ima upanuaji wa wilaya na mikoa unafuata ukubwa wa eneo vinginevyo hii mikoa na wilaya vilivyoundwa kisiasa vibatilishwe na fedha ambazo zinapotea kule ziende kuwahudumia wananchi badala ya kikundi kidogo cha wamangi meza.
            Hata kama tutatumia kigezo cha idadi ya wakazi, bado  kuna ushahidi wa kisayansi kuwa mikoa mikubwa tajwa hapo juu ukiondoa mkoa wa Lindi ni miongoni na inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wakazi.
            Tumalizie kwa kushauri serikali ya awamu ya tano iangalie mapungufu haya kwenye kuunda mikoa mipya. Pia iangalie namna ya kuivunja au kuipunguza mikoa mipya. Sipendekezi upanuaji mwingine. Vinginevyo tutaendelea kumtwisha mzigo mlipa kodi maskini ambaye mzigo alio nao unakaribia kumtoa roho.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: