Wednesday, 26 April 2017

Barua ya wazi kwa rais Magufuli


       Mhesimiwa rais John Pombe Joseph Magufuli,
            Naandika waraka huu wa wazi kwako kwa kusukumwa na uzalendo na usongo kwa nchi yangu. Hivyo, sitapindisha wala kuzua jambo zaidi ya kusema ukweli. Nimekusikia siku zote ukisema; Msemakweli ni mpenzi wa Mungu. Pia naandika kutokana na kujitenga na woga na unafiki wa kusema; kila kitu kiko sawa wakati si kweli. Hivyo, nitadurusu yafuatayo.
            Kwanza, nakupongeza; kumteua mpinzani japo mmoja kwenye serikali yako ingawa haitoshi.
            Pili, nakupongeza kwa dhati kwa kuwa na uthubutu wa kubadili mfumo mchafu na wa kijinai ingawa bado kuna mengi yanalalamikiwa kama vile kuchelea kufukua makaburi na kushindwa kuyafukia.
            Tatu, baada ya kukupongeza, nitoe machache yanayokufanya ulaumiwe kwa sababu za msingi kabisa.
            Mosi, ni ile hali ya kutoa amri kwa serikali kufanya biashara na vyombo vya habari vya serikali huku vya binafsi vikiachwa vife kifo cha taratibu. Hii si sawa.  Madhara yake ni kama ifuatavyo:
            a) kuvinyima vyombo vya habari binafsi matangazo ni kuviua hasa ikizingatiwa, vyombo vingi vya habari huendeshwa kwa fedha ya matangazo zaidi ya habari.
            b) ni kuwanyima riziki waandishi, wachangiaji na wafanyakazi wengine wa vyombo husika. Mfano, tangu utoe amri yako, vyombo vingi vya habari vinasuasua kiasi cha kuwakopa ima wafanyakazi wake ukiachia mbali wachangiaji. Je madhara ya hii ni nini? Licha ya kufanya wahusika waishi maisha magumu, itawashawishi kama si kuwalazimisha kuomba rushwa mbali na kuwa na chuki na utawala wako.
            c) huu ni ubaguzi. Sina namna ya kuueleza. Vyombo vya habari vipo kisheria na si matakwa ya mtu au taasisi yoyote zaidi ya dola; na pia ni mojawapo ya shuruti ya utawala bora na wa sheria.
            Tatu, nitagusia chanzo cha sintofahamu hii baina yako na vyombo binafsi vya habari. Japo zipo sababu nyingi, kubwa inaweza kuwa kuibua baadhi ya mambo ambayo hayakukufurahisha. Mfano mzuri, ni ile hali ya kuvamiwa kituo cha runinga cha Clouds kinachodaiwa kunakodaiwa kufanywa na mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda.  Sijui vyombo vya habari vinajisikiaje vinapoona mwenzao ametendewa jinai na mhusika kuendelea kukingiwa kifua?  Hapa hatujaongelea wabunge wanaotekwa na kufunguliwa kesi za kubambikwa. Rejea walivyoonyesha chuki kwa kumshangilia mtangulizi wako; haijawahi kutokea. Japo wasaidizi na washauri wako wanaoogopa kukupa ukweli, kimsingi, kashfa hii ni yako. Kwani anayeshutumiwa ni mteule na mwakilishi wako. Hivi huyu bwana ana nini kiasi cha kufanya hata waheshimiwa wabunge wahoji na kulalamika na wasisikilizwe? Je hii inajenga picha na uhusiano wa aina gani baina ya serikali yako na mhimili huu wa dola?
Kadhia hii imekuchafua kama rais. Kwani, vyombo vya habari viliamua kugomea kuandika habari za mteule wako huyu mwenye ushawishi mkubwa kwako. Nijuacho, mkuu wa mkoa ni mwakilishi wa rais. Anapogomewa, anagomewa rais. Je nini kifanyike? Ondoa katazo kwa taasisi za umma kutotoa matangazo kwa vyombo vinafsi. Kwani, malipo ya matangazo hayo hutokana na kodi za wananchi bila kujali itikadi.
            Kumbuka, Tanzania imejengwa kwenye misingi ya haki na usawa. Hivyo, anapobaguliwa mtu au taasisi kwa itikadi au mawazo yake ni uvunjaji mkubwa wa katiba. Nimekusikia mara nyingi ukisema; wewe si mnafiki na unachukia unafiki. Zaidi umekuwa ukisema wewe ni wa wote bila kujali dini, itikadi wala rangi. Sijui kama kubagua vyombo binafsi ndiyo huku kuwafanya na kuwaonyesha kuwa wote ni wako? Vipi?
            Wana tasnia ya habari wanaishi kwa mateso makubwa baada ya wewe kuondoa haki ya kupata matangazo toka kwenye asasi za umma. Ikumbukwe. Tanzania ni mali ya watanzania kwa sawa. Haiwezi kuendeshwa kwa matakwa ya mtu mmoja au kundi moja hata liwe na madaraka kiasi gani. Hivi ikitokea vyombo vya habari binafsi vikafunga shughuli zake hata kwa mwezi mmoja, serikali, licha ya kujenga picha mbaya, itawasiliana na watanzania vipi?
            Nimalizie kwa kugusia madhara yatokanayo na niliyosema hapo juu kama ifuatavyo:
            Mosi, inajengeka chuki dhidi yako na serikali bila sababu za msingi. Hili si jema. Si matarajio ya watanzania.
            Pili, ikishajengeka chuki, ushirikiano baina ya raia na serikali unatoweka kiasi cha kuweza kuhujumu juhudi zako mahsusi na adhimu.
            Tatu, hasira zitokanazo na chuki hii zinaweza kuipasua nchi na kuingia vurugu. Hata Rwanda ambako hupenda kutolea mfano, walianza hivi tokana na baadhi ya watu kuwa juu ya sheria kinyume cha sheria.
            Nne, inapotokea kutoaminiana au kuchukiana, uwezekano wa kulipiza visasi unakuwa mkubwa hasa kwa mipango na miradi ya umma. Sitaki hili litokee.
            Je nini kifanyike kuondokana na kadhia hii?
            Napendekeza kufuata katiba ya nchi na si ilani ya chama tawala tu. Hapa lazima tukubali kushindwa na kujadiliana. Mfano, watuhumiwa wa uchafu mbali mbali washughulikiwe bila kujali ukaribu wao kwako.
            Pili, dhana ya usawa itekelezwe kwa vitendo na si maneno. 
            Tatu, utende sawa na maneno yako. Mfano, dhana za usemakweli, kuchukia unafiki na kuwajali watanzania bila kujali dini, itikadi za kisiasa, rangi au watokako zitekelezwe kwa vitendo badala ya kuwa maneno matamu ya majukwaani.
            Japo yapo mengi, nakushauri  mheshimiwa rais upate nakala ya kitabu changu cha Africa’s Best and Worst Presidents: How Neocolonialism and Imperialism Maintained Venal Rules in Africa ambapo nimekuweka kwenye kundi la viongozi bora kama hutabadilika tokana na spidi na staili uliyoanza nayo kabla ya kujitokeza niliyosema hapo juu.
            Kwa heshima na taadhima, ndugu rais, acha niishie hapa.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: