Saturday, 29 April 2017

Kaya ya madaktari wengi na madudu kibao

          Karibu katika kila uteuzi hukosi kusikia dokta so and so ameteuliwa na dingi kuula somewhere. Hapa siongelei akina Bashiteshite wala Makorongo Muhanga. Naongelea wateule wanaoitwa madaktari wa kweli. Sijagusia maprofesa kibao waliojaa kwenye ofisi za umma wakitafuna kaya.  Tena hawa ni madaktari wa kweli na siyo kama wale aliowahi kuwashukia mwanaharakati Msemakweli Keinerugaba aliyefikia kuwatungia kitabu cha Mafisi na Mafwisadi wa Elimu Danganyika huku wengine wakifungua kesi na kubwagwa kiasi cha kushindwa kulipa hata gharama. Tukirejea kwa madaktari orijino, je huu ubobezi wao umeisaidiaje kaya hasa walevi kule madongo poromoka kama sisi tuishio kwa Mfuga Dog  na kumalizia maisha yetu kwenye kanywaji pale Uwanja wa Hyena?
            Kwanini nahoji usomi wa wateuzi na wateule wetu? Siachi kushangaa namna wanavyoshindwa kuutumia udaktari wao kujua kuwa matumizi yao ya hovyo yanafanya kaya yetu iwe kapuku na apechealolo. Kwani, bado wanatumia mashangingi ya bei mbaya wakati kaya yao ni ombaomba na kapuku wa kunuka. Je hili nalo linahitaji udaktari kulideku au ni ujinga tu wa kawaida utokanao na elimu? Leo nitauliza maswali bila kutoa majibu ili wao wanijibu kwa ufasaha kama wanaweza.
            Pili, kama haitoshi, bado  wanaolialia kuzuiwa kwenda kuzurura ughaibuni. Hamkuona wengi walivyonuna waliposikia kuwa Bashite na bi Nkubwa wake walikwenda kutanua majuu huku wao wakipigwa stop? Ajabu ya maajabu, tokana na sijui ujinga sijui uchizi juzi niliona wengi wakimshangilia Vasco da Gama kiasi cha wengine kusema bila aibu kuwa wanammiss! Si mlikuwa mkimalalamikia alipotumia ngwe yake yote akizurura. Leo kaja banabana mnakumbuka blanketi kumeishakucha. Ngoja nitakwenda kumpa orodha ya wote walioshangilia upuuzi ili awashughulikie kama alivyomfanyie Nipe Mapepe pale alipotaka kumgusa mwanae kipenzi aliyependezwanaye.
            Kaya inapojaa madaktari wengi wa politiki ni matatizo matupu. Juzi nilimsikia mduwanzi mmoja mpingaji akisema eti nabii Joshwa amemtabiria ushindi kwenye uchakachuaji ujao. Hivi kweli mlevi mwenye akili timamu anawaweza kumwamini tapeli huyu wa Kinigerieni kweli wakati alishawaliza wengi mmojawapo akiwamo dada yangu Joisi Banda? Ama kweli mtumu Paulo aliona mbali alipowauliza Wagalatia nani alikuwa amewaroga. Acha nami ntume Mlevi niwaulize wabongolalalanders, nani nyie aliyewaroga kiasi cha kuanza kuvamiwa na matapeli wanaokimbia njaa na kesi kwao eti kuja kuwalisha neno? Nani nyinyi aliyewaroga mnaoabudia kusaliwa kana kwamba mu maiti?
            Pamoja na kuwa na PhD kama kumi kubwa zikiwa za ulevi na uchomaji majani huwa siachi kushangaa mantwiki ya kuwa na wasomi karibu kila idara lakini bado kaya ikaishia kuombaomba tokana na kukosa vipaumbele. Hebu niulize tena kilevi. Ilikuwaje kaya nzima yenye wasomi kila ngeli kuruhusu mfano nchanga uliojaa madini kusafirishwa ughaibuni kwa miaka 20 bila kustuka? Ilikuwaje kaya yenye kujaa wasomi, kama ni wasomi kweli, iliingia mikataba ya kipumbavu kama Richmonduli aka Symbiosis ambayo hivi karibuni ilishinda kesi ya kufilisi kaya, IPtL, Kagoda, UDa na mingine mingi ambayo imegeuka kile watasha huita albatross around neck? Sitatafsiri ili wasomi ninaowalenga watafsiri.
            Ukiachia hayo niliyotongoa hapo juu, inakuwaje kaya yenye wingi wa wasomi inajaa woga kiasi cha watu wawili kuiteka huku wasomi wetu wakiendelea kuchelekea jinai hii kana kwamba hawakusoma vitabu vya magwiji kama Karl Marx, Nelson Mandela, Fredrick Engels, Socrates, Plato, Nkwazi Nkuzi Mhango Willa Ngwenyama aka Sibusiso Sibulele na wengine wengi? Naona yule anatikisa kichwa kana kwamba huyu mwanafalasa wa mwisho si gwiji. Nenda kasome tabu lake la Africa Reunite or Perish au lile la Africa’s Best and Worst Presidents; How Imperialism Maintained Venal Rules in Africa. Kama haitoshi kasome Born with Voice, Souls On Sale au Psalms of the Oppressed. Kama huupati umombo basi kasome Nyuma ya Pazia au Saa ya Ukombozi huku ukingojea Perpetual Search ambayo iko jikoni kabla ya Is it Global War on Terror or Global War over Terra Africana? How Global War is Used to Occupy Africa Militarily.  Pamoja na ulevi wangu, huwa naongea kwa ushahidi ili nisijeitwa au kudhaniwa kihiyo au msomi wa hovyo asiyezalisha chochote. Mimi sikwenda shule kujifunza woga na ujinga.
            Kwa vile nahisi kiu, ngoja nimalizie hapa kwa kuwaasa wasomi wa kweli waje tupige kanywaji pamoja niwatoe woga. Guys, Guess what. Fear nothing except fear itself. Tuonane wiki ijayo nikirejea toka Koromije kukoroma. Message sent and delivered.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: