Wednesday, 5 April 2017

Laiti wakuu wa mikoa na wilaya wangeiga mfano wa Mjema

  Image result for photos of sophia mjema
 
            Hatua ya mkuu wa wilaya Ilala,  mheshimiwa Sophia Mjema, ya kuuzindua umma kwa kuukataa mwiko wa kuwa shuhuda wa uhujumu wa taifa letu ni ya kupigiwa mfano. Tokana na ushupavu wake,  uzalendo na ujasiri aliweza kuvamia kiwanda feki na cha kitapeli cha toys za kuchezea watoto huko Mabibo jijini Dar Es Salaam. Kiwanda hiki kinachomilkiwa na matapeli wa kihindi, licha ya kutolipa kodi tangu kianzishwe mwaka 2006, kinawalisha wateja bidhaa bandia na zisizo na viwango. Kwani, ilibainika kuwa kinatengeneza toys kwenye mazingira hatarishi  na kuweka lebo za China wakati bidhaa husika hazitoki huko. Je mamlaka za viwango zilikuwa wapi wakati upuuzi huu ukifanyika kama kweli wanafanya kazi zao vizuri na kitaalamu? Je kiwanda hiki kimeishambaza bidhaa hizi haramu kiasi gani nchini? Je kuna viwanda bubu kama hivi vingapi nchini? Je wakubwa wetu wanaohusika hawajui au kuna namna wanavyonufaika na hujuma hii kwa taifa?
            Tokana na hatua hii ya kipekee na kizalendo, tungeshauri serikali kuwakamata wahusika na kuvifungia viwanda hivi ili liwe somo kwa wengine wanaodhani Tanzania ni shamba la bibi ambapo matapeli toka nje wanaweza kuja na kuchuma utajiri kwa njia haramu na kuhujumu taifa. Hawa wanapaswa kukamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya kuhujumu uchumi, kudanganya na kulisha watu wetu bidhaa feki na zisizo na viwango. Itakuwa ni ajabu kama wahusika watatozwa faini huku wazawa waliobainika kuingiza magari kwa kuyaficha kwenye mitumba wakionzea ndani chini ya kosa la kuhujumu uchumi. Tungeshauri viwanda kama hivi vitaifishwe huku wahalifu husika wakibanwa na kulipa kodi ambayo wamekwepa kwa muda wote waliofanya biashara kabla ya kuwatupa gerezani. Pia kiwanda husika kichunguzwe kuhusiana na kadhia ya kuajiri wafanyakazi wa kigeni bila kufuata utaratibu. Mbali na hilo, mamlaka zinazohusika na kusajili biashara na viwanda ziwajibishwe kwa ima uzembe au kushirikiana na wahusika kuhujumu taifa. Maana haiwezekani kiwanda kama hiki kifanye kazi zake kwa miaka yote hii kikiwa bubu na bila kulipa kodi. Je ilikuwaje mamlaka za maji na umeme zikakipa huduma kiwanda hiki bila kujiridhisha kuwa kimefuata taratibu zote za kufanya biashara nchini? Je kuna uwezekano kuwa kiwanda hiki kinaweza kuwa kimekwepa kulipia umeme na maji?
            Pia tungeshauri wakuu wa mikoa na wilaya kuiga mfano huu na kuhakikisha shughuli zote haramu zinamulikwa na wahusika kuchukuliwa hatua. Kwani, ukiachia mbali kutolipa kodi ya mapato, kuuuza bidhaa feki na jinai nyingine, kiwanda husika kilibainika kuwanyonya wafanyakazi wake ambao wengi ni wazawa. Kama haitoshi, kiwanda husika kiliwalazimisha wafanyakazi kufanya kazi kwenye mazingira hatarishi na magumu huku wakilipwa malipo kidogo kulingana na kazi wanazofanya.
            Hakuna ubishi; wakuu wengi wa mikoa na wilaya wanapoteza muda mwingi kuwadhibiti wapinzani wakati wakiachia jinai hii ya kuhujumu uchumi ikiendelea kuudhoofisha uchumi wetu na hali za maisha ya watu wetu. Je taifa limeishapoteza fedha kiasi gani ukiachia kunyonywa na kudhalilishwa kwa raia wake? Je kweli Tanzania inahitaji uwekezaji huu wa kijambazi? Japo kweli tuna shida ya uwekezaji nchini, uwekezaji wa namna hii ni hatari kuliko kutokuwa na uwekezaji kabisa.
            Katika kukagua nyaraka za kiwanda husika, Mjema aligundua kuwa kina namba za kodi (TIN) wakati hakilipi kodi. Je hapa hakuna jinai nyingine ya kughushi nyaraka za umma au kuzipata kwa mlango wa nyuma kinyume cha sheria? Je hawa wamilki wa kiwanda husika wanaishi nchini kihalali na wana vibali vya kufanya na kuishi nchini kama wanavyopaswa? Je ni wafanyakazi wangapi wa mamlaka zinazohusika wanaowasaidia wahalifu hawa kiasi cha kula nao? Hapa lazima kuwa na mkono wa watu wenye mamlaka si bure.
            Tumalizie kwa kumpongeza Mjema kwa kuwataka wakuu wengine wa mikoa na wilaya kuiga mfano wake katika kupambana na wahalifu wanaohujumu nchi na uchumi wetu. Waache kukaa maofisini na kutoa maagizo wakati mambo yakiharibika. Wakati wa Tanzania kuondokana na ujinga na uhayawani wa kutumiwa na wahalifu wachache wa ndani na nje ni sasa. Tunashauri wahusika wazisake bidhaa zote ambazo ziko kwenye soko na kuzikamata na kuziteketeza ili liwe somo kwa wahalifu wengine. Pia huu uwe mwanzo wa kubaini viwanda vingine kama hivi nchi ambavyo bila shaka viko vingi tu. Hii maana yake ni kwamba taasisi husika na watendaji wanapaswa kuacha mazoea ya kukaa maofisini wakisubiri kuletewa kila kitu. Mambo ya kuwaamini wafanyabiashara yalishapitwa na wakati. Biashara haina kuaminiana tokana na ukweli kuwa lengo kubwa la wafanyabiashara karibu wote ni kupata faida hata kama ni kwa njia ya kuvunja sheria au kuwanyonya watanzania kama ilivyobainika kwenye kiwanda hiki feki.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatan leo.

No comments: