Wednesday, 19 April 2017

Kijiwe Chamtaka Makonda Aonyeshe Vyeti

Image result for katuni za bashite
       Baada ya kugundua kuwa kaya ina mkwamo utakanao na sekeseke la Daudi Bashite aka Makonda, kimeamua kuokoa jahazi kwa kuhakikisha kila mmoja anatendewa haki bila ubaguzi wala upendeleo. Hii inshu imeletwa na Msomi Mkatatamaa tokana na ubobezi wake kwenye mambo ya Utatuzi wa Migogoro kimataifa yaani International Conflict Resolution.
            Msomi akiwa leo amekula suti ya bei mbaya na tai nyekundu kama ya dokta Kanywaji anatia timu na kufunguka “wazee, nionavyo mimi ni kwamba kaya imekwama kama siyo kukwamishwa. Maana, nikiangalia kulia na kushoto naona mkwamo ukiachia mbali sanaa za akina Bashit kutaka wanusurike na kashfa zao lukuki wasijue hawa wanaowahadaa wataishiwa ganzi yao na kuwatumbua. Hamkumsikia dingi akisema anao vihiyo 9,000 sirikalini anaongoja kuwatumbua? Hakuna kilichonisikitisha kama vita dhidi ya mihadarati kuzikwa kwa haki huku uwajibikaji na usawa vikipaa bila kusahau vita dhidi ya miharati kugeuka kuwa adimu kama vyeti vya Bashite.”
            Kabla ya kuendelea Kanji anamchomekea “sasa kama veve naona kaya iko kwama sasa nini napendekeza vatu ifanye ondokana na kwamo hii au nataka ilielie kama Basite kwa kanisani? Mimi toa sauri moja kuba. Kama Konda iko na weti si itoe mambo yote nakwisha na nakata zizi ya fitna. Kama baba yake napenda kaya sauri yeye toa weti ili mambo ikiwise.”
            Msomi anajibu “kama usingedakia, ungejua ninachomaanisha. Nakuja huko Kanji wala huna haja ya kuhofia. Ninachomaanisha na kupanga ni kwamba sisi kama kijiwe chenye hekima kuliko wote duniani siyo kuishia kulalamika bali twende kwa Bashite na kumwomba jambo moja dogo tu, kuonyesha vyeti vyake ili mambo yaishe na maisha yaendelee au vipi? Akiendelea kuzungusha kama ambavyo amekuwa akifanya basi twende kwa baba yake tumpe ishu nzima lau ajue tunavyoichukulia bila kujali ukaribu wala sanaa za Konda. Tena tusishikwe na kigugumizi kama hawa wanaomkingia kifua wakati wakijua kuwa lisemwalo lipo; na kama halipo laja. Kwanini tugombanie kitu kidogo kama vyeti? Kama anavyo si atoe na kuonyesha; na kama hana si aseme tu; kwani yeye wa kwanza?”
            Mgoshi Machungi anakula mic “hapa Msomi umemigusa pabaya. Ukimwambia kitu kama hiki atakupiga mingumi kama siyo mingwaa. Jamaa hataki kusikia juu ya kutoa vyeti.  Amesindwa hata kutoa cheti cha kuzaiwa. Maana, wapo wanaosema kuwa huyu jamaa anaweza kuwa muundi. Vinginevyo isingekuwa noma waa soo kama angekubai kuonyesha vyeti ii mambo yawe shwai.”
            “Yakhe nkubaliana nawe. Kwanini kusimamisha maisha ya kaya kwa vitu vya kidohodoho kama vyeti? Kama anavyo au hana si aseme lau tujue ukweli ili tuzodolewe au tuwazodoe wale wanonkingia kifua?” anachomekea Mpemba.
            “Kwa ninavyomjua jamaa, kama angekuwa na vyeti jenuine angekuwa ameishamwaga. Hakuna kinachonishangaza kama daktari wa kutibu majipu naye kushikwa na kigugumizi utadhani lao moja. Kwa namna jamaa alivyokuwa na kasi na usongo wa kutumbua majipu, sikutegemea hili wallahi,” anachomekea Mijjinga huku akibwia kahawa yake.
            Sofia Lion aka Kanungaemba anakatua mic “hata mimi nashangaa. Nakumbuka hata baba yake kipenzi aliwahi kusema si lazima wachovu wasingizie wana masters au PhD. Alisema kama wana vyeti vya darasa la saba waseme tu kwa vile si lazima kila mchovu awe na shahada hizo kubwakubwa. Sijui  nini kimemkumba akajipiga mtama kwenye sakata hili au ni yale ya mwenye mapenzi  haoni?”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu “jamani, tumelalamika sana. Sasa inatosha. Nadhani, kama warume, tunapaswa kuionyesha dunia hii kaya ni ya nani kati ya sisi na akina Bashite. Maana naona tunapoteza muda kwenye mambo ya hovyo huku mambo ya maana yakizidi kuharibika. Acheni ubwege pande zote. Hapa lazima, kama alivyosema rahis, lazima tuweke uzalendo mbele badala ya ubashite, ukondakonda na ugufuligufuli. Lazima kaya kwanza. Mengine baadaye. Hapa lazima tuepuka kuhubiri maji na kunywa mvinyo. Tuache unafiki na ubwege. Badala yake tuite koleo koleo bila kujali hadhi ya mchovu awe mzito au mwepesi. Enough is enough. Bashite must pack and hit the road vinginevyo tuchenchiane. Au vipi? Naungana na wale wanaotaka  twende kwa Bashite na kumtaka aondoke kwenye ofisi yetu. Akigoma twende kwa baba yake lau wajue kaya hii si mali binafsi bali mali ya wachovu au vipi?”
            Mipawa anakula mic “mheshimiwa Bwege nakuunga mkono  na mguu. Huu upuuzi na urushi vinavyoendelea ingekuwa majuu mambo kwisha zamani gani! Hapa ndipo tunapojivua nguo kama kaya. Inakuwa vigumu kushuhudia hata wale ambao hukuwatarajia wakijivua nguo kiasi cha kusaliti viapo vyao. Nadhani dingi aliapa peke yake na si pamoja na Bashite. Sijui kwanini anamg’ang’gania kiasi cha kutelekeza viapo vyake na kaya.”
            Wakati kijiwe kinaanza kunoga si likapita shumbwengu la Bashit. Wacha tulitoe mkuku kujua lau nani atatekwa usawa huu. Kama siyo ndata kutuzuia, huenda tungentumbua jamaa sisi wenyewe!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
Image result for katuni za bashite

No comments: