Sunday, 16 April 2017

Kushamiri utekaji: Barua kwa wahini na wahiniwa

Tanzania imekuwa na mambo ya maudhi hivi karibuni; si kwa watu binafsi bali kama jamii na taifa. Nimesikia wabunge wakiungana wa chama tawala upinzani kutaka kadhia ya utekaji ulioanza kuzoeleka kuchunguzwa. Hii ni baada ya kutekwa wanamuziki wawili na baadaye waheshimiwa wahiniwa watarajiwa wapatao 11 kutishiwa kutekwa. Wapo waliotaja waziwazi waliowatishia kuwateka kutokana na kutopendezwa na mambo au matendo yao. Mtajwa mkuu ni mkuu mmoja wa Mkoa ambaye anaonekana kuwa kipenzi cha mkubwa mmoja nchini kiasi cha kutoguswa; na kama akiguswa, anayefanya hivyo hata awe waziri atakiona cha mtema kuni. Hivyo, huyu ndiye mhini wetu na wote waliotishiwa au kuchukizwa na matendo yake ni wahiniwa. Nisema wazi, nami ni mhiniwa kama mwanajamii anayeshuhudia upendeleo wa wazi ukiachia mbali ulimbukeni na matumizi mabaya ya madaraka. Kinachogomba hapa ni mtu ambaye hakupigiwa kura hata moja kuwa na nguvu kuliko hata wahishimiwa waliotumwa na wananchi kuwawakilisha katika kuongoza taifa lao linalohinika kirahisirahisi kwa sasa.
            Historia ya utekaji hata hivyo, haikuanza jana. Wanaokumbuka namna Dokta Stephen Ulimboka aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha madaktari na Absalom Kibanda aliyekuwa mwenyekiti wa jukwaa la wahariri, watakumbuka wawili hawa walivyotekwa tokana na msimamo wao dhidi ya utawala uliopita. Hata hivyo, tokana na tabia ya jamii ya wahiniwa yenye kufanya vitu vya hovyo kuwa vya maana na vya maana kuwa vya hovyo, wahanga hawa wa kwanza, hawakutangazwa wala kuzua gumzo na hofu kama ya hawa wahiniwa wa pili. Hawakuwa maarufu kama hawa wa pili ingawa kama tunatoa umaarufu tokana na mchango na stahiki ya mtu, wahiniwa wa kwanza walipaswa kuwa maarufu kuliko wahiniwa wa pili. Hilo tuliache. Unategemea nini kwenye jamii ambayo baa inaheshimika kuliko shule? Hii nayo, kwa wenye akili, inahini na kuchefua.
Je nini chanzo cha kadhia hii? Majibu ni mengi kuliko majibu; nami nitapapasa na kutongoa machache kati yake kama ifuatavyo:
            Mosi, ni kutokana na woga wa wale wanaowahini wenzao unaosababisha wawaone hawa wanaowadhania kuwa wabaya wao hadi wakawahini hata kuwateka kama tishio kwa madaraka yao.
            Pili, ni ukosefu wa utawala bora na wa sheria. Maana kama ungekuwapo, haiwezekani wahini wakaendelea kuwahini wahiniwa nao wasishughulikiwe lau kwa kuhiniwa kidogo. Japo baadhi yao walishahiniwa na maadui zao, wana rungu la kuwapondea.
            Tatu, ni ulimbukeni na ulevi wa madaraka. Kila palipo ombwe la utawala bora basi kuna ulimbukeni na ulevi wa madaraka. Heri ulevi wa pombe kuliko wa madaraka.
            Nne, mfumo mbovu wa utawala ambao kimsingi ni ule tuliorithi toka kwa wakoloni ambapo wakati mwingine unashindwa kubaini tofauti kati ya gavana generali wa kikoloni na maaskari wake na watawala waliochukua ofisi na mamlaka yake wakaendelea kutawala kutoka kwenye jumba lile lile kwa staili ile ile na falsafa na saikolojia ile ile.
            Tano, ni woga wa wahiniwa ambao hawataki kuungana na kuwakabili wahini lau kieleweke.  Na hii pia inatokana na kuendelea kujengeka hofu na woga kijamii bila msingi. Wakati mwingine unajiuliza: inakuwaje wahini wachache wawahini wahiniwa wengi kiasi hiki wasiwapatilize lau kuwafunza adabu?
            Sita, kusambazwa kwa hofu kwa kimombo fearmongering ambayo mara nyingi ni nyenzo kuu ya maimla wote duniani. Maimla wote licha ya kueneza hofu, nao wana hofu kadhalika. Wana hofu kiasi cha kuogopa hata vivuli vyao. Tuliona mifano kwenye nchi kama DRC wakati wa imla Joseph Mobutu mwizi mkubwa kuwahi kutokea barani. Tuliyaona Uganda chini ya mumiani na chinjachinja Idi Amin. Tuliyashuhudia Libya na Misri pale wahiniwa walipoamua kusema: “Sasa yatosha.” Tuombe Mungu na tuyasikie kwa  wenzetu. Tutolee mifano kwa wenzetu. Tusiombe wahiniwa wafikie kusema “inatosha.”  Siku zote punda anaonekana mnyama mpole na hodari wa kubeba mizigo. Ila anapofikia kusema “inatosha” huwa hapatoshi wala kukalika.
            Tumalizie kwa kuwaasa wahini na wahiniwa waangalie mienendo yao hasa wakijua kuwa binadamu ni viumbe ambao hawatabiriki na ni rahisi kubadilika. Japo wahini wetu wamekuwa wakitolea mifano ya Rwanda, husahau kitu kimoja; au tuseme huangalia upande mmoja, ya huko yalianza na viumbe kama Bashite. Yalianza na kutekwa kwa haki za kidemokrasia. Yalianza na kutekwa kwa wahiniwa. Yalianza na kutotenda haki. Yalianza na matumizi mabaya ya vyombo vya dola. Yalianza tokana na siasa za kujuana. Yalianza na siasa za kuburuzana, kujuajua ukiachia mbali kuangalia upande mmoja wa sarafu. Yote katika yote, hakuna  kitu kibaya kama wahini kuwateka wahiniwa wasijue wajibu wao ni kuwalinda na kuwahakikisha amani na usalama kwa njia zinazokubalika kisheria.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: