UTHIBITISHO kwamba kampuni ya BAE Systems ya Uingereza imetembeza rushwa ili kupata kuiuzia Tanzania rada ya kijeshi (Plessey Commander Fighter Control System), unatupa changamoto kama taifa kuhusu uwajibikaji na utayari wetu kukomesha ufisadi.
Hiyo imetokana na ripoti ya Shirika la Uchunguzi wa Jinai la nchi hiyo, Serious Fraud Office (SFO) kuthibitisha BAE Systems ililipa pauni 30 milioni kwa baadhi ya vigogo wa Tanzania waliotajwa waziwazi.
Mauzo hayo ambayo aliyekuwa waziri wa ushirikiano wa Uingereza, Claire Short aliyaita kuwa ni uozo na harufu ya ufisadi, yalifanyika mwaka 2002.
Kati ya waliotajwa ni mwanasheria mkuu wa zamani wa Tanzania, Andrew Chenge na gavana wa zamani wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Dk. Idris Rashid wanaosemekana waliificha fedha waliyokatiwa kwenye benki nchini Uingereza.
Ajabu watuhumiwa hawa hawajawahi kukiri wala kukanusha ingawa ushahidi wote unaonyesha walitenda makosa na kuhujumu nchi.
Kibaya zaidi, mamlaka za uchunguzi za Tanzania zimekuwa nzito kuwashitaki kwa hofu ya kudhalilisha vigogo wengine wa serikali walioidhinisha ununuzi wa rada.
Taarifa mpya ni msumari wa mwisho kwenye jeneza kwa wale wanaosita kushitaki achilia mbali watuhumiwa wenyewe.
Watanzania na Waingereza wanangoja kuona mamlaka sasa zitatoa kisingizio gani mbele ya ufunuo huo.
Kwa kuthibitishwa kukosa, BAE Systems imepigwa bakora. Je, washirika wake watanusurika au kuendelea kulindwa na wakubwa wenzao? Na je, Watanzania walioibiwa wataendelea na ukondoo?
Kisheria, kama mamlaka zetu zisingekuwa na tabia ya kulindana, kesi yake ni rahisi; si BAE wamekiri kutoa? Iwapi nafasi ya kuendelea kugeuza Watanzania ni majuha?
Je, rais Jakaya Kikwete ambaye amekuwa akijenga imani watu kwamba anapambana vilivyo na ufisadi, naye atakubali kuendelea kuumbuka na serikali yake kuonekana kumbe ina ubia na watu tofauti na alivyowahi kukana?
Wakati muafaka wa kumshinikiza Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali (DPP) kuchukua hatua za kiutu uzima ndio huu.
Tunajua shahidi. Watuhumiwa ni vigogo wenye ushawishi katika ngazi za juu kutokana na kuwahi kushika nyadhifa nono walizozichafua na kuzitumia vibaya.
Lakini je, Watanzania wataendelea kufumbia macho uoza na dhulma hii? Vyama vya mageuzi vitanyamaza kama wananchi wataendelea na ukondoo? Tutarajie maandamano ya kushinikiza haki kutendeka kwa watuhumiwa kushitakiwa mahakamani.
Tuhuma za ubadhirifu kwenye tenda ya kijambazi waliyopewa BAE zilipofumuka, kwa makusudi watawala wetu walizikejeli. Sasa ukweli umedhihiri. Wanasemaje?
Uzuri wa tukio hili la kihistoria ni ukweli kwamba BAE hawakuzungusha kitu wala kushangaa. Wametaja wezi kweupeni.
Wakati tukisubiri hatua, vema kukumbuka kwamba kuadhiriwa kwa wakubwa kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi adilifu wa Uingereza.
Wangetaka wangenyamaza tu na fedha zetu zikawa zimeliwa na kampuni yao. Hawakufanya hivyo. Hawa kesho watatudharau na kutukejeli iwapo serikali yetu itashindwa kushughulikia vigogo waliolishwa asali.
Tunatakiwa kukua na viongozi wetu watie akili sawa na wafadhili wanaotusaidia. Walisita kwa kuwa uthibitisho haukuwepo, leo imeshathibitishwa hakuna cha kufanya wazubae. Ni kuchukua hatua na sasa siyo halafu.
Ningekuwa DPP ningeficha uso kusudi nyani wa kumuua asinilaghai. Ni kumuua tu maana muda wake umefika. Angeharakisha kupata ripoti kamili ya uchunguzi kutoka SFO ili kutumia taarifa hizo kufungulia watuhumiwa mashitaka.
Ajabu kusikia waziri anashinikiza fedha ziletwe haraka na kukabidhiwa serikali lakini haelezi ni lini watuhumiwa watashitakiwa.
Hakueleza ni vipi wanawasiliana na serikali kutaka fedha walizoficha watuhumiwa baada ya kuhongwa zirudishwe nchini.
Hivyo hatua ya BAE kukiri inajenga mazingira kwa serikali kurejesha heshima iliyokuwa imeipotea kutokana na kutowashughulikia wezi.
Miezi michache imebaki kabla ya uchaguzi. Kwa kuwa serikali inaogopa kushitaki watuhumiwa, upinzani uchangamke kwa kuzidi kuamsha umma maana yawezekana watuhumiwa wakalindwa hadi mwisho.
Kazi ya kuhamasisha wananchi kuitia adabu serikali ifanyike sasa. Hakuna sababu ya kutumia nguvu, wenyewe wanajua wapi pa kusemea.
Ndio wakati wa kuwaeleza kwamba ufisadi hauna nafasi Tanzania. Anayeutenda, asulubiwe badala ya kupokewa kwa shangwe.
Wananchi wasijali pilau wala pombe ya kienyeji au upande wa kitenge. Wajue wakichekelea takrima leo, ni majuto ya miaka mitano kwao.
Kwa vile watawala wanahubiri utawala wa sheria bila ya kuufuata, wanapokosea wao, bakora yao ni kuwanyima kura.
Hebu tuangalie fedha zile zingetumika kujenga shule na kuipatia vifaa vyote watoto wangapi wangenufaika?
Fedha zile zingenunuliwa dawa na vifaa tiba na kugawanywa kwenye zahanati za vijijini masikini wangapi wangenufaika?
Ni fedha kama hizo hutafunwa kila siku na watumishi wasiokuwa waaminifu na hakuna kinachofanyika kuzirudisha.
Bado utasikia rais wetu anashindwa kutoa jibu akiulizwa nini sababu ya Tanzania kuendelea kuwa masikini.
Nchi itaendeleaje wakati viongozi wanaibia wananchi na kutumia vibaya madaraka waliyopewa?
Nchi itapiga vipi hatua ya maendeleo wakati rais anaona fakhari kila siku kufanya ziara za nje na kuomba misaada?
Nini kama siyo upungufu kukubali kuomba huku rais akidiriki kuitwa ombaomba aliyevaa suti ya bei mbaya au mlafi anayetapika kwenye viatu vya wafadhili kama alivyowahi kusema balozi wa Uingereza.
Inataka mtu kuoba aibu na kutambua utu wake na maslahi ya watu wake. Vinginevyo serikali isingeshindwa kushitaki watu waliolamba asali.
Hivi kama matapeli wachache wanaweza kuiba kiasi kikubwa cha fedha tusishtuke si wakitaka hata kuangusha serikali wataweza?
Umma unataka walionufaika na ununuzi wa rada wakamatwe na kushitakiwa maana wakati wa kutafuta mchawi umepita.
Chanzo: MwanaHALISI Feb. 24, 2010.
1 comment:
GagisoloChals Anrielelin futtdevisee [url=http://napechke.com]Senanamaso[/url] Centumnimbele http://napechke.com
Post a Comment