Thursday, 23 September 2010

'Dodoma Locuta Est Causa Finita Est' mwisho wa CCM

KWA wanaokumbuka majivuno, kiburi, mitandao, usanii, uzembe na manjonjo ya utawala wa zamani wa Kirumi, bado wanakumbuka ujanja ujanja ulivyojiangamiza baadaye na ikabakia historia.

Himaya hii iliyoishi zaidi ya miaka 500 ilianza kusambaratika baada ya kugawanyika katika vipande wiwili- mashariki na magharibi, baada ya kifo cha Theodosius mwaka 395.

Mwaka 476 upande wa Magharibi, ulianguka chini ya utawala wa Romulus Augustus ambaye alilazimishwa kuikimbia Odoacer.

Upande wa mashariki ambao kwa kiasi fulani ulihimili mikiki na kufanya marekebisho mbalimbali ulisambaratika baada ya kifo cha Constatine IX. Trajan aliyechukua madaraka baadaye alishtukia akitekwa na Waturuki chini ya kiongozi wao Mehmed II huku akiwa amejigeuza mungu mtu juu ya ardhi.

Alilewa madaraka huku wasasi wa ngawira wakimramba miguu hadi kujisahau asijue wanafiki watupu ambao wangemkimbia baada ya taji kumtoka!

Chanzo kikuu cha kudhoofika hadi kutekwa na kutoweka ni ufisadi uliokuwa ukiendeshwa na wapambe wa mfalme (Praetorian Guards) na migongano baina ya seneti na mfalme huku Roma ikishikilia usanii wake wa Roma Locuta Est Causa Finita Est yaani ‘Roma Ikiishasema, Kesi Imefungwa’.

Hapa hatujagusia ukosefu wa kazi na maisha duni kwa wafanyakazi, kuporomoka kwa uchumi, matumizi makubwa, kutoweka kwa maadili, utumikishaji au unyonyaji wa umma na mengine mengi hadi ikavamiwa na kuangushwa kirahisi.

Histori ya Roma ni ndefu sana kiasi cha kuhitaji vitabu si makala. Nimeanza nayo kuonyesha ni jinsi gani kila kitu, hasa tawala, huwa ni cha msimu.

Nataka kuwapiga kijembe wajinga na wahuni wanaosema eti Chama cha Mapinduzi (CCM) kitatawala milele. Pia napenda kupiga upatu kuwa hata huu Muungano unaweza kufa tukawa na nchi mbili huru yaani Zanzibar na Tanganyika na maisha yakaendelea kama hautaboreshwa kwa matakwa ya umma badala ya watawala.

Kitu kingine ni kutaka kuonyesha kuwa ufanisi wa kupita kiasi huzaa maanguko. Karibu himaya zote zilizopita zilipanuka hadi kupasuka sawa na CCM ambayo imefanikiwa kutandawaa nchi nzima kiasi cha kujenga vijimitandao vya kimaslahi vinavyoanza kuipasua kidogo kidogo huku ikishikilia kuwa iko imara wakati siyo.

CCM imekuwa kama yule mama wa Kigiriki wa kutisha Medusa ambaye macho yake yakikulenga ilitosha kukugeuza jiwe.

Tumeona wengi waliogeuka mawe baada ya macho ya CCM kuwalenga kwa hasira. Tunawakumbuka kina Edward Sokoine na Horace Kolimba waliogeuzwa mawe waliposema CCM imekosa mwelekeo au kutaka kuirekebisha. Kosa lao kubwa kwa CCM ilikuwa ni kusema ukweli huu au kutaka kutenda haki. Na kwa wao binafsi ni kuendelea kubaki ndani ya CCM ilhali wa kijua hasira za Medusa binti Pholcys na mkedada Ceto na matokeo yake.

Siri mojawapo ya ufanisi wa himaya ya Roma iliyokuwa imetawala yapata eneo la ukubwa wa kilometa 6,5000,000 ilikuwa ni kauli mbiu yake ya Roma Locuta est causa finita est yaani kilichoamriwa Roma huwa hakina mjadala tena. Kilichofunguliwa au kufungwa Roma ndiyo kimefungwa au kufunguliwa hakuna wa kufunga au kufungua.

Ukiangalia mazingaombwe na usanii wa hivi karibuni huko Dodoma, utakubaliana nami kuwa kilichofungwa Dodoma, hakiwezi kufunguliwa na yeyote.

Sitapenda kuongelea vituko, kuzushiana, kumalizana na kuoneana kulikoripotiwa ambapo kada mmojawapo Hussein Bashe alipigwa kibuti kwa madai kuwa si raia. Maswali mengi yameishaulizwa na hayajajibiwa ni kwa nini sasa na si juzi kabla ya kutaka kugombea ulaji mkuu?

Awe raia au vinginevyo, Dodoma Locuta est causa finita est, Bashe kama rafiki yake Yusuf Masauni anayoyoma. Bahati mbaya kwa vijana hawa wote wameangushwa na sumu ile ile. Maana wengi wa wachambuzi wanasema eti walikosana na mtoto wa Rais Jakaya Kikwete yaani Ridhiwani ambaye ametokea kuwa King Maker kwenye Umoja wa Vijana wa CCM.

Roma kama himaya iliaminika kwa maajabu yake ambayo kimsingi hayakuwa maajabu kitu bali usanii ambao hatima yake uliisambaratisha Roma yenyewe.

Ni maajabu haya haya tumeyashuhudia juzi kule Dodoma yakiwapitisha watuhumiwa (Praetorian Guards) wa kashfa mbali mbali na kuwakata wapambanaji dhidi ya ufisadi mmojawapo akiwa Lucas Selelii mbunge wa Nzega anayemaliza muda wake ambaye nafasi yake baada ya kumtosa Bashe ilikwenda kwa Hamis Anderea Kigwangala ambaye naye anadaiwa kuwa Mrundi.

Maajabu ya Roma yanaendelea. Huko Kigoma kuna minong'ono kuwa mgombea aliyepewa baraka za CCM aliwahi kutajwa kwenye kura zilizoendeshwa na serikali ya CCM yenyewe dhidi ya wauaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi, kuwa ananunua viungo vya watu. Lakini kwa vile ni mwenzao, nani atamgusa? Dodoma locuta est causa finita est.

Na haya ndiyo maajabu ya watu kama Basil Mramba na Andrew Chenge wenye tuhuma na kesi mbichi kupindishiwa sheria na kupeta. Ni maajabu haya haya yaliyowawezesha waliotuhumiwa kughushi vyeti vya kitaaluma kama Emanuel Nchimbi, William Lukuvi, Mary Nagu, Victor Mwambalaswa na Makongoro Mahanga kupeta kana kwamba madai yao ni ya kutenda mema si kuvunja sheria.

Ni miujiza hii hii iliyowawezesha watu kama Rostam Aziz aliyedaiwa kuwa mmilki wa kampuni iliyodaiwa kuiba mabilioni ya EPA, Kagoda na Edward Lowassa aliyeachia ngazi kama ishara ya kukiri alishiriki uchafu wa Richmond kupeta. Ajabu maajabu haya haya yamemtupa nje Fredrick Mwakalebela kwa kutoa rushwa mbuzi siyo kuuza nchi!

Hata kina Diodorus Kamala na Samuel Chitalilo kama siyo kuasiwa na wapiga kura wangepeta.

Ni miujiza hii hii iliyowezesha watu kama Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, pamoja na kuvuruga chama na kuwa na mashikamano yenye kutia shaka, kuendelea kupeta.

Watu wengi wenye akili wanajiuliza. Nini mantiki ya serikali na TAKUKURU, kwa mfano, kukamata baadhi ya wana CCM na kuwaacha wengine? Vyombo vya habari viliwahi kuripoti kisa cha mgombea mmoja mwenye jina kubwa aliyewahi kushika nyadhifa za juu na baadaye kuchafuka na kutimka alivyokuwa akigawa simu tena miezi zaidi ya miwili hata kabla ya kura za maoni na TAKUKURU hawakufanya lolote!

Jambo muhimu la kuikumbusha Roma- CCM- ni ukweli kuwa mwenzake alitekwa na Waturuki kama ambayo siku moja CCM itajikuta imepinduliwa na mafisadi ambao tayari wameishaiteka na kuanza kuipeleka kuzimu taratibu.

Kwa ufupi ni kwamba kama ilivyokuwa Roma, kwa Tanzania, kila kilichofungwa au kufunguliwa Dodoma hakiwezi tena kufungwa au kufunguliwa na mtu. Ila Zanzibar wameanza kukifungua.

Uzuri wa ubabe na sanaa hii ni kuwa mbwembwe, manjonjo, kiburi, uzembe, usanii, ushufaa hujenga mbegu za uharibifu ambazo hatimaye husambaratisha genge zima kama tulivyoona kwenye himaya ya Roma.

Tuthibitishe kuwa wale wanaosema na kuamini kuwa CCM itatawala milele, licha ya kuwa hakifai, wanapaswa kusoma historia upya kama wanataka kuishi kwa usalama na ufanisi na vizazi vyao.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 22, 2010.

2 comments:

Anonymous said...

kuna fununu serikali inataka kuwalipa haki zao wastaafu wa iliyokuwa jumuhiya ya afrika mashariki kabla ya uchaguzi. lengo ni kupata kura za wazee hawa na ushawishi wao ili ccm ipate kura zao na za wategemezi wao na wale wote watakaoshawishika na kitendo hiki cha rushwa. tuwajulishe makamamda wa chadema wachunguze vema na wakemee rushwa hii ya wazi

Anonymous said...

Kama watalipwa ni jambo jema. Ila wao ni watu wazima watajua where to vote kwani 'watamix with theirs'