How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 2 September 2010

Mt. Mpayukaji atuma salamu kwa Rais Kikwete


Ndugu Rais,

Pole sana kwa shughuli nzito za kampeni na pia kwa kukumbwa na sahibu la kudondoka pale Jangwani Jumapili ya tarehe 21 ulipokuwa ukifungua rasmi kampeni zako za kutaka kurejea kwenye urais.

Ingawa wengi wanasema mengi, usijali. Hata Yesu alidondoka mara tatu wakati akitimiza kazi takatifu ya kuwaokoa wanadamu. Hivyo furahi na kushangilia kuwa nawe umeanguka kama Bwana Yesu ili kuwakomboa Watanzania kwenda kwenye maisha bora uliyowaahidi miaka mitano iliyopita.

Kwanza niseme kitu kimoja. Mie ni shabiki na kipenzi chako kufa. Hivyo, habari za msiba huu licha ya kunisononesha, zilinifanya nikaribie kupata kichaa. Na laiti kama kungelikuwa na mkono wa mtu, bila kujali makali ya sheria, ningemchinja huyu mtu na kunywa damu yake huku nikimalizia na kula nyama yake. Maana angekuwa amekufuru kumwangusha kipenzi cha watu na Mungu.

Bahati mbaya au nzuri siku ile ya tukio sikuwapo Jangwani kutokana na kuwa na majukumu mengine. Najisikia vibaya kwa wapiga picha kuficha tukio zima. Wapumbavu hawa. Mpaka leo sijajua ni kwa nini waliamua kufanya hujuma kwa uhuru wa kupokea na kutoa habari ambao ulikuwa ukijivunia kuutekeleza wakati ukianguka?

Wapuuzi hawa nao ni wabaya wako wanaotaka kukuonyesha kama Mungu-mtu ambaye hawezi kuanguka wala kuugua. Nashauri umuite waziri anayehusika na habari na kumpa karipio. Umwambie kuwa siku nyingine ukianguka waonyeshe tukio zima ili kuwapa wananchi haki yao ya kupokea habari. Pia hii itasaidia kuwaonyesha kuwa Rais wao ni binadamu anaugua au kufa na kadhalika.

Kuna kitu kimeniudhi sana. Kuna watu wanasema eti kuanguka kwako ni utabiri wa rafiki yako mpenzi, Shehe Yahya Hussein. Eti wanasema alipotabiri kuwa watakaokupinga watapukutika aliogopa kukwambia ukweli. Wanasema eti alisema kinyume kuogopa usimnyime ulaji. Sasa nakutaarifu. Kuanzia leo najipa jukumu moja. Nikiwasikia hawa nitawatia adabu bila kujali kuwa navunja sheria.

Kitu kingine kinachoniudhi ni baadhi ya watu kusema eti unaumwa na unaficha ukweli. Hivi nani mzima Tanzania? Na isitoshe, wanaotaka uwambie hali yako ya kiafya wao mbona hawajawahi kukwambia zao? Hata kama unaumwa tena sana, wao inawahusu nini? Hivi wewe ni rais wa kwanza kuumwa akiwa madarakani? Mbona yule jambazi wa DRC, Joseph Desire Mobutu, Yassir Arafat wa PLO, Oumaru Yar' Adua wa Nigeria na wengine waliumwa hata kufa na haikuwa nongwa?

Mie nashauri usiwasikilize wanaotaka uweke wazi hali yako ya kiafya. Maana hii ni mojawapo ya siri za usalama wa taifa na uwazi na ukweli kuwa afya yako ni siri yako, mkeo, daktari wako na watu wako wa karibu. Hao hao ni wanga wanaosema eti utaanguka tena. Kwani ukianguka wao inawahusu na wanapata nini?

Unajua ndugu rais, ukifanya kosa ukaweka mambo hadharani, ujue: watu watataka na afya ya mgombea mwenza wako naye afanye hivyo. Juzi nilisikia minong'ono ya kipuuzi kuwa naye si mzima. Nilitamani niwakate vichwa waliokuwa wakisema hivyo, ila kutokana na kutosikia vizuri walichokuwa wakisema kwa mafumbo, nawapa muda. Lazima nitakufa na mtu. Kwani kama afya yake si mulua wao inawahusu nini?

Una habari? Kipindi hiki cha kampeni huwa ni cha fitina na uzushi. Usishangae kusikia watu wakizusha mambo mengi hata kufikia kusema unaumwa umeme. Maana wanasema wazi kuwa hawaamini kuwa kufunga kwa siku moja kunaweza kukausha sukari yote mwilini. Na wanaosema hivyo wengine ni madaktari bingwa. Kuna haja ya kutafuta mbinu ya kuliua hili kabla mtama haujamwagwa kwenye kuku wengi.

Jamaa wanajua fitina. Wanauliza mantiki ya msafara wako kuhusisha ambulance kama kweli wewe ni mzima. Mie nimewajibu kuwa uwe mgonjwa mahtuti au vyovyote wao inawahusu nini iwapo kila mtu lazima alinde kitumbua chake?

Hukusikia walivyoanza kumzushia mpinzani wako Dk. Willibrod Slaa kuwa ana udini na ametumwa na kanisa la Kirumi la Vatikani wakati ni upuuzi mtupu? Hukusikia wapuuzi tena wenye madaraka wakisuka mipango michafu kummaliza ili waendelee kuiba na kula bila kunawa?

Kwa vile umeahidi kampeni safi na za kistaarabu, nashauri ifuatavyo:

Hakikisha unawapiga stopu wale wanaoleta kampeni za kipumbavu kama vile kuzushiana uraia kama ilivyotokea kwa kijana wako Hussein Bashe. Eti wanasema ni Msomali! Hivi kwa nchi yenye kukirimu wageni kila mazuri hata vyeo, kuna kosa kuwa msomali? Mbona wengine wana uraia wa Tanzania, India, Uingereza na Kanada bado wanapitishwa kugombea? Kwani Bashe ndiye msomali pekee huko Tabora? Mbona hata wengine walio juu wana majina kama rafiki yangu Mgosi nanihii? Bado hapa hujamuangalia yule mpiga debe bingwa wa kunyemelea vyama na ulaji kutoka kwa kina Mgosi aendaye kwa jina la Tambo.

Huu ni upuuzi na kuishiwa kisiasa kuanza kunyamazishana kwa kisingizio cha uraia. Hivi kweli kama Bashe hakuwa raia, alifikaje kwenye ngazi ya juu ya jumuia ya chama? Nakusihi uwakaripie hawa wapuuzi wanaozusha upuuzi.

Ingawa sitetei mamluki kutawala nchi yetu, kwangu nawaona hawana tofauti na walioghushi vyeti vya taaluma au mafisadi wakubwa wanaojulikana wanaoendelea kupeta. Ila wakae wakijua, kwa vile umeahidi kupambana na ufisadi, lazima utawakamata siku si nyingi. Mie nakuamini sana kuliko hawa wanaosema eti ulitoa ahadi hukuzitekeleza.

Hawa ni wapuuzi. Mbona umetekeleza ahadi zote!Uliahidi maisha bora kwa wote. Nani ana maisha mabaya Tanzania? Juzi ulinifurahisha ulipowatolea uvivu na kuwaambia kuwa wakiona wanasongamana barabarani wajue ni maisha bora. Maana kusingekuwa na maisha bora magari hata kama ni mikangafu, yasingeongezeka hadi kujaza barabara.

Hata kwenye majumba wanasongamana kutokana na kuzaana sana bila kufa kutokana na wewe kuboresha huduma za afya hadi ikabidi watu kulipia kumuona daktari kutokana na kuwa na fedha nyingi zisizo na kazi.

Kuna hili la uchakachuaji mafuta. Wajinga eti wanalalamika wakati hii teknolojia kama itaungwa mkono inaweza kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yayozalisha mafuta kwa wingi kwa kununua kidogo toka Uarabuni na kukirudufu. Na teknolojia hii ikiendelea, inaweza kusaidia hata kupata wapiga kura wa kutosha kutokana na watu kutopenda kujiandikisha kupiga kura.

Juzi nilisikia wabaya wako wakisema eti usipewe kura kwa vile hukutangaza mali zako na mkeo na watoto wako! Ebo! Hivi kwa vibaka na mibaka na majambazi waliozidi Tanzania wanataka ujitie kitanzi? Hawajui kuwa ukitangaza mali zako wezi watakuja kukuvamia hata kukukuua ili waibe mali zako! Mijitu mingine eti inasema WAMA ile NGO ya mkeo inaingiza mabilioni ya shilingi yasiyokaguliwa wala kulipiwa kodi. Well done. Kosa liko wapi? Sasa wapuuzi hawa wanataka utangaze hayo mabilioni wamkabe hata kumuua mkeo wakitaka kumuibia? Hivi hawa hawajui kuwa kura huleta kula? Hawajui kuwa mke wa kaisari ni kaisaria wa wanawake wote kiasi cha kuwatumia kupata mshiko sorry kuwatumikia kutafuta mshiko?

Duh kumbe ni barua!


Chanzo: Tanzania Daima Septemba 1,2010.

No comments: