Wednesday, 29 September 2010

Kikwete, Lowassa ni mchapakazi?!!!!!!!Akiwa mkoani Arusha wilayani Monduli alikokwenda kufanya kampeni, rais anayemaliza muda wake Jakaya Kikwete alitonesha tena vidonda vya watanzania hasa wapinga ufisadi.

Alikaririwa akimmwagia sifa mgombea wa CCM mbunge aliyemaliza muda wake na waziri mkuu aliyetimuliwa (siyo kustaafu kama anavyopambwa), Edward Lowassa.

Kikwete sijui kuwa kusahau, makusudi au dharau alikaririwa akisema: “Lowassa ni mchapakazi hodari, hana mfano wake. Wananchi tusahau yaliyopita tugange ya sasa na yajayo, namuombea kura.”

Huku ni kufuja maneno. Wamezoea kufuja pesa ya umma hadi wanafuja maneno ya kutushawishi tufuje haki na akili zetu! Ni dharau na kuishiwa kiasi gani?

Ni ajabu na aibu. Kwani vyombo vya habari na watanzania kwa ujumla hawakulaani kauli hii ya kuwadhalilisha na kuwangopea. Kikwete alipaswa abanwe aombe umma msamaha kwa kutonesha vidonda vyake. Kwanini tusahau yaliyopita wakati tunaendelea kuuguza vidonda vyake? Huwezi kuganga yajayo bila kurejea yaliyopita. Kufanya hivi licha ya kuwa upogo ni kushindwa wazi. Maana kesho hutengenezwa na jana.

Tuache utani na usanii. Je kweli Lowassa ni mchapakazi kama alivyosema Kikwete au ni upotoshaji na jitihada za wazi kumsafisha na hatimaye kumrejesha rafiki na mshirika wake huyu ambaye rekodi zake ziko wazi kuwa si mchapakazi bali mtu aliyeliingiza taifa kwenye hasara na mateso makubwa kutokana na kuwa kizani kwa mwaka mzima ukiachia mbali ubinafsi na tamaa? Je huu ndiyo uchapakazi usio na kifani wa Lowassa?

Rekodi gani za Lowassa zinaweza kumvutia mpiga kura yeyote mwenye akili? Madai kuwa amejilimbikizia mali lukuki zisizo na maelezo na zitokanazo na ufisadi kama alivyowahi kudai baba wa taifa marehemu mwalimu Julius Nyerere? Ajabu, kwa kufuru na upotoshaji wa namna hii, utamsikia Kikwete akimsimanga Nyerere kuwa anamuenzi!

Inashangaza rais kutoa maneno kama haya hasa wakati huu anapokabiliwa na kibarua kigumu kurejea madarakani bila kufanya lolote la maana ukiachia mbali shutuma nyingi za ufisadi zilizomkabili rais binafsi na serikali yake!

Je bado watanzania kweli wanamhitaji Lowassa ambaye alilazimika kuachia ngazi baada ya kubainika alikuwa nyuma ya kashfa iliyotugharimu mabilioni ya Richmond? Je hii si dharau kwa bunge lililomtimua na wananchi kwa ujumla? Je mtu huyu analo jipya la kuwafanyia wananchi kiasi cha kuwaaminisha wamchague tena aendelee kuwakingia kifua marafiki zake?

Leo kasema Lowassa ni mchapakazi. Jana alisema waziri wake wa fedha wa zamani mwenye kesi ya matumizi mabaya ya madaraka Basil Mramba ni mtu makini! Mtu gani makini anaweza kushitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka na ofisi? Je Kikwete hajui kiswahili hivi au anatuchezea shere? Usishangae kesho kusikia Kikwete kaenda Shinyanga wilayani Bariadi na kusema mgombea wake wa jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, aliyeripotiwa na mashirika ya kijasusi ya Uingereza kuficha kiasi cha zaidi ya shilingi 1,000,000,000 nchini humo ni mchapakazi. Kazi ya kuhujumu na kufilisi umma!

Kesho kutwa utamsikia akiwa Igunga kumpigia kampeni Rostam Aziz akimnadi kama mtu mwaminifu na mfanyabiashara wa kupigiwa mfano!

Je huu si mshikamano wa kifisadi, uongo na matusi ya nguoni kwa waathirika yaani watanzania?

Ni Kikwete huyu huyu ambaye serikali yake imekuwa ikiuibia umma kwa kumtambua na kumlipa marupurupu ya ustaafu Lowassa wakati alitimuliwa na Bunge baada ya kamati teule ya Bunge kumkuta na kashfa ya ufisadi ulioteketeza mabilioni fedha ya umma.

Tuutazame ukweli bila makengeza. Je ni kweli kuwa Lowassa ni mchapakazi na waziri mkuu mstaafu au rafiki wa rais aliyenusurika kufikishwa mahakamani kutokana na kukingiwa kifua na rafiki yake?

Kwa kumtangaza Lowassa kama mchapakazi asiye na mfano, Kikwete, kwanza analidhalilisha bunge lililomkuta na hatia ukiachia mbali kuwakatisha tamaa wachapakazi wa kweli.

Ukiangalia alivyosimama bega kwa bega na Mramba, utagundua kuwa hata kesi inayomkabili ni changa la macho. Maana kama Kikwete kweli angekuwa na nia ya kumshughulikia vilivyo na si vunga, angejitahidi angalau kuepuka kuwapigia kampeni watu kama hawa ambao mbele ya watanzania ni machukizo na alama ya mshikamano wa kinafiki na wa kifisadi.

Sifa za Kikwete kwa swahiba yake Lowassa zimethibitisha tambo za Lowassa kuwa urafiki wao na Kikwete si wa barabarani na hivyo hauwezi kuvunjwa na vyombo vya habari. Je hii kwa mpiga kura mwenye uchungu na nchi yake inaashiria nini zaidi ya kuwa taarifa kamili kuwa wawili hawa na wenzao wanaotuhumiwa kushiriki uhujumu wa taifa maslahi yao na urafiki wao ni zaidi ya maslahi ya taifa? Je huu si ushahidi wa mazingira kuwa kashfa iliyomuondoa Lowassa ilikuwa na kila baraka za Kikwete na kutimka kwake kulimnusuru Kikwete na serikali yake kiasi cha kuwa tayari kwa lolote ilmradi mtu wake asiguswe?

Je huku si kutumia sheria na madaraka kibaguzi na kwa upendeleo? Rais anayejali urafiki, udugu, unyumba, kujuana, ushirika, mitandao na mengine kama haya hatufai. Rais wa Tanzania anapaswa kuwa ofisini kwa ajili ya watanzania na si marafiki au jamaa zake. Anayebishia hili aangalie mke na mtoto wa Kikwete wanavyokata mbuga kumpigia kampeni wakifuja mali na fedha ya umma. Je tunataka Kikwete atukwaze na kutuangusha mara ngapi jamani?

Ingawa watanzania hasa vyombo vya habari havikulaani upotoshaji na mshikamano huu wa kifisadi, nichukue fursa hii kama mtu binafsi kulaani jinai hii. Nitafurahi kama nitasikia watu wengine wakijitokeza kulaani upotoshaji huu. Nitafurahi zaidi wapiga kura kama watatumia upotoshaji huu kama sababu mojawapo, kati ya nyingi, kuinyima kura CCM.

Na niseme wazi. Kama Kikwete na CCM wataendelea na mshikamano na upotoshaji huu hawataachwa kuendelea kuitwa Chama Cha Mafisadi na majina mengi yasiyopendeza.

Ni vizuri wakumbuke. Tanzania si mali ya CCM, Lowassa, Kikwete wala mitandao ya kifisadi bali ya watanzania. Kuna siku umma utaamka na wanaotukoga watakosa pa kujificha. Nani alijua kuwa majambazi kama Mobutu Seseseko (Zaire), Jean Bedel Bokassa (CAR), Ferdinand Marcos (Ufilipino), Fulgencio Batista y Zaldívar (Cuba) na wengine wengi wangelidondoshwa tena kwa aibu na people's power?

Dalili za kuoza kwa mfumo wowote wa maisha ni pale watu fulani wanapojiona watukufu kuliko wengine kiasi cha kukufuru na kutetea uoza watakavyo kana kwamba hakuna kesho. Swali linabaki pale pale. Je kweli Lowassa ni mchapakazi au?

Chanzo: Dira ya Mtanzania Septemba 27, 2010.

3 comments:

Mbele said...

Makala yako hii ni nzuri sana. Laiti watu wangekuwa na moyo huu wa kutafakari mambo na kutafuta ukweli. Shukrani.

NN Mhango said...

Ndugu yangu Mbele haujakosea. Hata hivyo tusiache kufikiri na kuandika hata kwa niaba ya wananchi. Kuna siku msumari utaingia kama ilivyotokea Kenya ambapo imla wa nchi ile Daniel arap Moi na waramba viatu wake waliwahi kusema, kama CCM,kuwa KANU itatawala milele na wakaanguka ndani ya kipindi hicho hicho.
Hakuna dhambi isiyosameheka watatenda watanzania kama kumrejesha Kikwete na mafisadi wake.Mafisadi wameshikamana. Na thinkers tusikamane kuwafichua na kuwaumbua.

Malkiory Matiya said...

Nchi yetu imegeuzwa kuwa kampuni ya mafisadi pamoja na viongozi wa CCM pamoja na familia zao.

Ona mtoto wa Kikwete, mmoja wa watoto wa Makamba ambaye ni mbunge mtarajiwa anafanya kazi Ikulu na mwingine ni kigogo wa Voda baba bado yupo kwenye siasa. Naye binti wa Pinda ambaye ni mfanyakazi wa idara kuu ya utumishi kama siyo kupigwa chini alishakaribia kabisa kuukwaa ubunge.

Jamani hawa viongozi hawaoni hata aibu kutaka kuitawala nchi yetu wao pamoja na familia zao! Hapa ni suala la common sense tu.