The Chant of Savant

Thursday 23 September 2010

Utabiri wa shehe Asohaya Hoseni

MFUNGO wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan umepita salama.

Baada ya dhiki kuzidi kuongezeka na uwezo wa wadanganyika kufikiri kupungua, kiasi cha kuibiwa na kudhalilishwa na kila tapeli na msanii, nimegundua kuwa utabiri, usanii na utapeli vinalipa kweli kweli.

Hivyo, baada ya kuona maeneo ya Magomeni Mikumi, Mikocheni, Mwenge na Jangwani matapeli kujizolea sifa na ndururu, nami nimeamua nitie guu.

Kwanza nieleweke. Sitabirii njaa wala kujikomba wala kutafuta sifa uchwara bali mapenzi ya kaya yangu ya Danganyika inayogeuka kaya Juha. Pia sina ushindani na matapeli maarufu mnaowajua kuanzia kina Ka-Tortoise, Gamanyua, Rwakatarehe, mpiga ramli Shehe Ubwabwa Yaya na wengine. Wao ni vihiyo mie ni bonge la msomi tena mwenye PhD ya kusotea na si kupewa kama kilaza fulani asiye na kumbukumbu kama alivyosema msomi mwenzagu daktari Silaha hivi karibuni.

Wala mie si kihiyo kama mgosi Machungi wa Makambale. Mie ni msomi kama Shivji na gwiji kama Mchonga. Upo hapo mshirika? Mie siogopi mtu wala kitu bali kumwaga ukweli ili kuwakomboa wadanganyika wapumbavu ambao kila kitu kimewekwa mbele yao lakini bado wanaamini watapelekwa Kanani wakati ni motoni kwa kwenda mbele.

Nikiwa ndiyo najinyoosha kwenye sita kwa sita yangu na bi mkubwa akiwa anakoroma pembeni mwangu baada ya … we koma! Hili tuliache nimepata accident ya ajali ya ulimi. Maana nilitaka kwenda nje ya mpaka kama jamaa yangu anapokuwa akiwaongopea wadanganyika wakati wa kutoa ahadi. Utamsikia akisema: tutafanya tutafanya hadi anadondoka.

Nawaza kufanya kazi ya utabiri wa kweli siyo ramli za shehe Ubwabwa mtoto wa yaya mlea majini wa mitaa ya Migomigo.

Natabiri tena kwa kujiamini kuwa vigogo vitang'oka. Anayebishia hili au kuwa na wasiwasi nalo a jiulize ni vigogo vingapi vimeishaanguka wakati vingine vikingoja kunyofolewa? Sasa nasema mapema. Vile vigogo vilivyoko hatarini kuusikia ulaji magazetini vije kwangu haraka niwakinge na anguko hilo vinginevyo wataanguka tu. Hawana haja ya kwenda Bagamoyo wala Sumbawanga. Waje Manzese kwa Mfuga Mbwa. Namba ya nyumba sitaji wataulizia hadi wanipate.

Na kuhusu yule mgombea ninayemshabikia, nitampa kinga ya kuadhirika yaani kumshauri ajipumzikie asijeanguka hata kufa kama alivyomtabiri yule mhuni wa migomigo.

Aking'ang'ania nitamtengenezea zindiko ambalo huwezi kulinusa kwa pua na atakayejaribu kumchezea litakalompata asinilaumu. Mie siyo kama wale watabiri uchwara wanaotumia viungo vya majini na mazeruzeru kuwaibia wateja wao wapumbavu kwa kuwapumbaza na sifa na ahadi za kipuuzi kama wanazotoa kwa wadanganyika.

Mie nasema facts na I am more educated than all those goons calling themselves astrologers or preachers and whatnot. Looh! Nshachanganya na umombo utadhani niko kwetu mombo! Hata hivyo msinishangae. Siku hizi napandisha mwenembago wa kiinglish kutokana na kuwa rafiki mkubwa wa malkia.

Natabiri kuwa wale wote walioibia nchi ama kwa kushiriki MAEPA au Marichmonduli watakumbwa na aibu na magonjwa ya ajabu ajabu kama kupayuka, kuanguka, kuchezeana na kudhulumiana hata kukata roho.

Rushwa kwenye uchaguzi itaongezeka kiasi cha wale waliopaswa kusimamia kuiangamiza kuishiriki vilivyo wao wake na watoto zao bila hata chembe ya aibu. Maskini watumiao matumbo kufikiri watahongwa na kuahidiwa pepo ilhali wanao dhahiri wanavyoelekezwa motoni.

Neema za muda kama kuongezeana mishiko na uhuru mfu hasa kwa ndugu zangu wamachinga kuvunja sheria ya mgambo wa Kandoro zitaongezeka na kupotea baada ya kutangazwa matokeo yatakayotawaliwa na wizi mkubwa wa kura. Wauza gongo nao wakae mkao wa kula. Polisi waliozoea kuwapiga mabao wataamrishwa kusitisha zoezi zima la kuibiana hadi uchafuzi upite. Vyangudoa waliokuwa wakisumbuliwa na ndata kuwakamata uzururaji na kujiuza wanaweza kujiuza kwa sana hadi mwishoni wa Oktoba ambapo nyota zinaonyesha mambo yao yatabadilika kutokana bahari kuwa na mawimbi makali kutokana papa kuwa na njaa sana baada ya kukaa muda bila kula.

Pepo za vuli zitavuma kutokea Bagamoyo, Chalinze, Kangangani hadi Monduli lakini hazitakuwa na madhara yoyote zaidi kujifia kitambo si kirefu. Ngurumo zikisikika sana toka Karatu ikiwa ni ishara ya neema kwa wakulima. Maana baada ya hapo itanyesha mvua itakayosafisha uchafu wote uliokusanywa na pepo za vuli ambazo mara nyingi ni ishara ya uchafu.

Natabiri vurugu zitakuwapo kutokana na wezi wa kura kupambana na watakaotaka kuwaibia kiasi cha baadhi ya watu kufikishwa the Hague baadaye. Jamaa yangu madevu Mureno Okampo yuko anachekelea. Kama jamaa watatiana ngeu na kutoana roho kama ninavyoona kwenye utabiri wangu. Maana atakuwa na watu wengine wa kujaza kwenye sero zake karibu kabisa na Chaz Teila yule wa Liberia.

Natabiri kuwa atakayeiba kura na kushinda akaapishwa atakufa kabla ya kumaliza kipindi chake cha wizi. Pia natabiri kuwa wizi kwenye ofisi na mashirika ya umma utaongezeka kutokana na kufidia rushwa itakayohongwa kwenye uchaguzi. Natabiri kuwa wengi watapewa kakumba ya mipete ya ajabu ajabu kama kinga wakati ni kifo.

Nashauri hawa wajinga wajinga wanaodanganywa na wajinga wajinga wenzao waje kwangu niwape kinga ya kweli ambayo inaitwa UUUK yaani uadilifu, umakini, ubukuzi na kuongea lugha ya wananchi na kufanana nao kimatendo siyo kilongolongo kama wale wenye njaa kaya.

Kusikika ngurumo na radi ni ishara ya mababu kuchukizwa na utawala huu. Nasema wazi kwa kutumia utaalamu wangu wakitabiri kuwa mababu wa Danganyika hawana raha wala ladhi na yanayoendelea kwenye nchi yao walioipigania na kuifia.

Kwanza nisisitize. Mie sijikombi kwa gendaeka yeyote hata awe na maulaji kiasi gani. Kwanza sina appointment na daktari yeyote India kuhitaji kujidhalilisha na kujikomba ili gendaeka wenye madaraka wanilipe fadhila kwa kunilipia nauli na kugharimia matibabu kama shehe Ubwabwa bin Njaa Yaya.

Angekuwa anajua kutengenezea watu kinga si angejikinga badala ya kuhangaika na kujivua nguo ili apate pesa ya kwendea Inida? Kusum bin kusuru audhubillahi mina-shaitwan rajiim shehe Yaya Ubwabwa.

Pia natabiri kuwa bi mkubwa wa Njaa Kaya atafikishwa kwa pilato muda si mrefu asipoacha kujipendekeza na kufuja mali za walevi kwa kutanua na kupiga ndogo ndogo kwa ajili ya bwanaake. Juzi nimemuona hata Riziki naye akimpigia kampeni dingi wake. Kumbe tuna ufalme bila kujua!

Loh! Kumbe kumekucha!
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 22, 2010.

No comments: