The Chant of Savant

Tuesday 6 September 2011

Barua kwa Edward Lowassa




Mpendwa waziri mkuu aliyeachia madaraka kutokana na kujiingiza kwenye kashfa ya Richmond, Edward Ngoyai Lowassa (MB).

Salamu sana na habari za siku nyingi? Leo naomba nichukue fursa hii adimu na muhimu kuwasiliana nawe kwa njia hii ya waraka wa wazi. Najua una mambo mengi ya kufanya na kufikiri hasa ikizingatiwa unakabiliwa na shinikizo la kujivua gamba.

Naandika waraka huu kutokana na kuadimika kwako kwenye vyombo vya habari siku hizi. Mbona umekuwa kimya sana? Je unatafakari jinsi ya kujibu mapigo au kujivua gamba kama yule "mwarabu" wa waziri mkuu aliyetajwa na Bangusilo Ibrahim Msabaha? Je ule mpango ulioripotiwa mwezi jana kuwa unapaswa kujivua gamba kama Rostam Aziz na kama hutafanya hivyo mwenyewe utavuliwa gamba unauchukuliaje? Je unadhani ni danganya toto au watafanya kweli?

Mpendwa,lazima nikiri na kusema ukweli. Hakuna siku nilihuzunika kiasi cha kumwaga chozi kama alivyofanya mkeo kama siku ili niposhuhudia kwenye runinga ukitoa hotuba yako ya mwisho ukiwa waziri mkuu. Namkumbuka, mama Regina, kama alivyoitwa wakati ule. Sikujua kumbe umama unakwenda na cheo! Utasikia mama nonihino. Kila aendeko heshima na makandokando. Wengine wamefikia kuenziwa sawa na waume zao. Ila madaraka yakitimka nao hutokomea. Cheo cha mumewe kikishatimka na umama unapotea na kuja ugumba wa madaraka!

Hata hizi NGO za uongo na ukweli za kuchumia utajiri wa haraka huchangiwa baba akiwa madarakani. Akishakitoa NGO inadoda kama vile haijawahi kuwepo. Nikikumbuka Equal Opportunity and Trust for First Lady (EOTFL) ilivyododa sasa naamini kweli cheo ni dhamana. Nikimbuka mbwebwe za jamaa aliyetangulia akitisha vyombo vya habari na alivyonywea sasa, naamini kweli avumaye baharini papa. Bahati mbaya, wengi wa namna hii hili huwa hawalijui hadi linapowakuta! Hayo tuyaache ndiyo wizi wa kisasa na kisiasa.

Mpendwa,hata kama miaka imeyoyoma, picha hii mbaya sana huwa inanijia mara kwa mara kiasi cha kuninyima raha. Najua wewe huwa hutishiki kirahisi ingawa ukibanwa sana hufanya maamuzi ya kustukiza na yenye kustua. Je una mpango wa kutustua kwa kujivua gamba kwenye dakika za majeruhi kama alivyofanya Rostam? Je una mpango wa kuachia ngazi kwa kustukiza kama ulivyofanya wakati wa kuutema uwaziri mkuu au unangoja uvuliwe gamba kwa aibu na fedheha? Mie, hata kama si mshauri wako wa karibu wala mwandishi wa habari wa kukusifia na kukusafisha, nashauri ujivue badala ya kungoja kuvuliwa. Je kati ya hayo niliyoshauri hapo juu una mpango gani ndugu yangu?

Mpendwa,baada ya kuona umekaa kimya sana, nilijawa na wasi wasi kiasi cha kuanza kuwaza: kama utavuliwa ulaji wako ndani ya chama, kweli utakuwa na nguvu tena hata za kuweza kugombea urais kama wengi wanavyosema? Huoni, kama utavuliwa gamba kwa nguvu, utatimiza unabii wa Nape aliyesema kuwa lazima mvuliwe magamba wewe na Andrew Chenge na mkitoe? Maana, Nape alisema kuwa samaki huwa na nguvu akiwa majini, ila ukishamtoa majini si chochote si lolote. Kwanini hukumjibu hata kwa vijembe? Hayo tuyaache.

Mpendwa, nakumbuka ulipoulizwa kipindi fulani ueleze mipango yako kuhusiana na kujivua gamba kwa mwenzio ulisema kuwa muda ukifika utaweka mambo hadharani. Je utatimiza ahadi yako hii lini wakati muda unazidi kuyoyoma?

Mpendwa,uliwahi kung’aka kwa vyombo vya habari kuwa wewe ni rafiki mkubwa wa rais Jakaya Kikwete na urafiki wenu hakuanzia barabarani na wala hautavunjwa na vyombo vya habari. Je kwa sasa una msimamo gani kuhusu hili hasa ikizingatiwa kuwa urafiki wenu haukulenga kwa wewe kuwa gamba? Je unadhani rais ataendelea kujichafua kwa kulinda urafiki wako au msimamo wa chama na maadili badala ya madili?

Mpendwa, juzi juzi nilisoma sehemu fulani mtetezi wako akisema eti wewe ni mchapa kazi wa kupigiwa mfano. Ajabu jamaa huyu mbumbumbu asiyejua anachosema wala kuandika alisahau kuwa watu wanajua kati ya pumba na mbegu linapokuja suala la uchapa kazi! Bahati mbaya watu wengi wanakuelezea kama mchapa kazi wa kupigiwa mfano bila kutoa mifano ya kazi zako nzuri zaidi ya zile unazoshutumiwa kuzifanya! Je jamaa alimaanisha kazi zako kama vile Richmond na kutafuta mvua kule Thailand?

Mheshimiwa, naomba unisamehe kwa muda wako nitakotumia kuwasiliana nawe. Leo ni maswali mengi kutokana na kutokuwa na nafasi ya kuja Monduli kukuhoji. Nakumbuka juzi juzi uliwaonya wakubwa wa chama chako na serikali kwa kusema eti wana ugonjwa wa kuogopa kufanya maamuzi magumu hata kama watalaumiwa. Je wewe una mpango wa kufanya uamuzi gani mugumu kati ya kujivua gamba na kutimka au kuvuliwa na kutimliwa? Je unangoja nini wakati muda unazidi kuyoyoma?

Sambamba na kuonya juu ya ugonjwa wa kuogopa kufanya maamuzi magumu, nakumbuka: ulimshauri waziri mkuu, Mizengo Pinda, kupunguza wizara yake kutokana na kuwa kubwa kupita kiasi ingawa hukuona wala kufanya hivyo wakati ikiwa chini yako. Je umeishamkumbusha tena kufanya hivyo kutokana na ukweli kuwa tangu utoe ushauri huo, tuseme; ulipuuziwa au kuwekwa chini ya busati? Je ni kwanini hukuliona hili ulipokuwa incharge wa wizara hiyo?

Ingawa hili si jipya kwako nami, unajibuje tuhuma kuwa ulijilimbikizia mimali lukuki iliyopatikana kinyume cha sheria? Maana ni miaka mingi tangu tuhuma hizi zitolewa bila kujibiwa. Naomba nawe ufanye maamuzi magumu lau ujibu tusikie upande wako. Na je unajiteteaje kuhusiana na tuhuma kuwa ulililingiza taifa kwenye kiza na hasara ya mabilioni kutokana na kupigia debe kampuni feki la Richmond? Naomba nitumie ushauri wako uliowapa wenzako kuwa wasiogope kufanya maamuzi magumu hata kama watalaumiwa. Je wewe una mpango gani wa kujibu tuhuma ili usionekane mnafiki wa kuona ya wenzio wakati yako huyaoni? Hilo la kujivua gamba tuliache.

Je una mpango gani wa kutoa maelezo au tuseme utetezi kuwa watoto wako waliajiriwa na Benki kuu kutokana na ushawishi na nafasi yako serikalini? Je una habari kuwa ni makosa kutumia cheo chako kuwanufaisha ndugu au wanao? Je huu nao ni sehemu ya uchapakazi wako?

Samahani katika waraka huu nitakuwa nakwenda mbele na nyuma. Hivyo naomba unisamehe na kunivumilia kwa hili. Maana mambo ya kujadili ni mengi na ya muda mrefu.

Naomba nimalizie waraka huu kwa kuomba lau nami unijibu hata kwa mafumbo kama utaweza. Pia naamini kuwa kwa muda uliobakia kufikia kusuka au kunyoa, usipotumika vizuri, kuna hatari ya wewe kugeuka historia mud si mrefu. Mungu apishe mbali na kila la heri ingawa maji yameishafika shingoni na mbuzi hawezi kuimbia kisu.

Chanzo: Dira Agosti 2011.

No comments: