HAKUNA ubishi kuwa uteuzi wa wakuu wa mikoa na upanuzi wa ukubwa wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete umewashangaza wengi. Na hii si mara ya kwanza kwa Kikwete kuonyesha anavyotenda tofauti na ahadi zake.
Kwa wanaokumbuka, Rais Kikwete wakati wa kampeni za kuwania urais mwaka 2005, aliahidi kuunda serikali ndogo ili kuokoa kodi za wananchi. Lakini punde tu baada ya kuingia madarakani, alijipiga mtama na kuunda serikali kubwa huku akiunda wizara zisizo na ulazima nyingi tu. Kikwete hakuishia hapo.
Alinogewa na mchezo huu uliompa sifa kwa baadhi ya watu bila kujali madhara kwenye uchumi wa nchi. Aliongeza idadi ya mikoa na wilaya bila kuja hata ahadi zake za awali. Hili la kutojali hali ya uchumi wa taifa na ulaghai yamekwisha kuzoeleka.
Katika uteuzi wake wa juzi, Kikwete kwa mara nyingine aliandamwa na jinamizi la kashfa ya Richmond iliyomng’oa rafiki yake, Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani aliyegeuka hasidi wake mkuu. Baada ya kuondoka Lowassa na baadhi ya mawaziri waliotuhumiwa kuwa nyuma ya kashfa kubwa, Kikwete ‘alisuka’ baraza la mawaziri upya. Katika kufanya hivyo, aliwalipa fadhila wakombozi wake wawili, yaani Spika wa zamani, Samuel Sitta na mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya kuchunguza Richmond, Dk. Harrison Mwakyembe.
Kikwete alisuka baraza la mawaziri upya baada ya kupoteza mawaziri wa zamani waliokuwa ima wamepoteza udhu au kuhusishwa na kashfa mbalimbali, wakiwamo Basil Mramba, Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi, Kingunge Ngombale - Mwiru, Juma Ngasongwa, Anthony Diallo, Joseph Mungai, Zakhia Meghji na Andrew Chenge.
Hawa wawili walipewa uwaziri kutokana na kutimiza majukumu mawili kwa Kikwete na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jukumu la kwanza ilikuwa ni kumtwisha Lowassa zigo lote la kashfa ya Richmond kiasi cha baadaye Dk. Mwakyembe kusikika akisema kuwa kama wasingeficha baadhi ya mambo serikali nzima ingeporomoka badala ya ‘bangusilo’ Lowassa.
Jukumu la pili ilikuwa ni kwa Sitta na Mwakyembe kuvuruga mipango ya kuanzishwa kwa Chama Cha Jamii. Ingawa hatuwezi kueleza kuwa walikubaliana, bila shaka mazingira yanaonyesha hivyo, hasa baada ya wale waliodhaniwa kuwa wapambanaji dhidi ya ufisadi ghafla kupewa vyeo na kuufyata. Hii ndiyo awamu ya kwanza ya Richmond kwenye uteuzi wa Kikwete.
Jukumu la tatu lililotokana na kuteuliwa Sitta na Mwakyembe ni kuanza kuonekana uhasama wa wazi baina ya kambi ya Kikwete na ya Lowassa. Wengine huita kambi hizi mitandao.
Awamu ya pili ya jinamizi la Richmond ilijitokeza hivi majuzi wakati wa uteuzi wa wakuu wapya wa mikoa, ambapo mjumbe machachari wa kamati ya Mwakyembe Injinia Stella Manyanya aliteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Ukiachia mbali uteuzi wa jinamizi la Richmond, kuna kile tunachoweza kuita ‘recycling’ na kurithishana ulaji. Hivi haishangazi kuona kuna Nchimbi waziri na Nchimbi mkuu wa mkoa? Hapa kuna nini kama si kujuana?
Katika ‘recycling’ tunamaanisha uteuzi wa watu walioshindwa kwenye ubunge kama vile Mwantumu Mahiza, Joel Bendera na Ludovick Mwananzila. Hili lilithibitika zaidi pale baadhi ya wakuu wa mikoa waliostaafu kusemekana eti watapangiwa kazi nyingine, ambao ni Bibi Amina Mrisho aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani; Dk. James Msekela aliyekuwa Dodoma; Abeid Mwinyimusa aliyekuwa Tabora na Daniel ole Njoolay aliyekuwa Rukwa. Kazi gani baada ya kustaafu kama si kulea kundi la political Jay-walkers (sina Kiswahili chake).
Ukiachia mbali ku-recycle, kuna kuzidi kuendeleza mfumo wa zamani wa kiujima wa kuteua wanajeshi kwenye ukuu wa mkoa na wilaya.
Hapa hatujaangalia wengine wanaotia kila aina ya shaka jinsi walivyofika hapo. Si ajabu siku moja tukaambiwa wengine walikuwa mashoga wa mke wa rais hata marafiki zake wa utotoni na mambo mengine kama hayo.
Kutokana na tabia hii ya ajabu ya rais, baadhi ya watu wamefikia mahali kutabiri kuwa hata mawaziri walioshindwa kwenye uchaguzi kama Lawrence Masha tusishangae wakapewa ubalozi hata ukuu wa mkoa.
Hapa hujaongelea wengine wasio na mbele wala nyuma kisiasa, watakaoteuliwa kuwa wakuu wa wilaya, kulipwa fadhila kutokana na kutoa baadhi ya huduma halali na haramu. Hayo tuyaache.
Leo tumeangalia jinsi jinamizi la Richmond linavyoandama uteuzi wa Kikwete. Akifanya uteuzi wa wakuu wa mikoa iliyobakia na wilaya, tutakuja na uchambuzi kuangalia msukumo wa kufanya vile hasa kujuana. Pamoja na yote, wengi wanajiuliza, Kikwete atajifunza lini na atakumbukwa kwa lipi la maana zaidi ya kuwa muhimili wa ufisadi na kila aina ya madudu?
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 21, 2011.
No comments:
Post a Comment