MWENZENU jana niliota ndoto ya maana sana. Niliota nikiwa mkuu wa kaya. Niliota mie na bi mkubwa tuko Ikulu tukitanua na kuhudumiwa kama wafalme. Pia niliota bi mkubwa ameanzisha NGO na kila wafanyabiashara na wenye fweza walikuwa wakiichangia kama hawana akili nzuri. Niliota bi mkubwa wangu amechana na kujitona midhahabu kama hana akili nzuri.
Yawezekana niliota ndoto hii kutokana na jana ya usiku wa ndoto yenyewe kusimamia kikao cha kijiwe kujadili uteuzi wa ulaji wa wakuu wa mikoa uliofanywa na mkuu. Tulikuwa tukijadili jina moja baada ya jingine kuanzia wale wanaolipwa fadhila za mazabemazabe ya Richmonduli, waliochuja na kupachikwa viraka, watoto wa wakubwa wa zamani, mashoga wa bi mkubwa, nyumba nonihino za zamani za jamaa, ndata na vinara wa mitandao. Hivyo basi yawezekana kichwa kilirudia ngoa yangu juu ya jinai hii ya kupeana ulaji.
Nakumbuka. Baada ya kutangazwa idadi ya wakubwa wa mikoa, Msomi Mkatatamaa alitoa sentensi moja ya Kiingereza: “The same mess and blunders.” Hakufafanua ingawa sisi wajuzi wa ung’eng’e tulijua alichomaanisha kuhusiana na mkuu. Hayo tuyaache.
Leo nataka nisimulie ndoto niliyoota nikiwa kwenye maulaji kama mkuu ingawa asubuhi yake nilijikuta peupe nikikimbizana na ngwala ngwala kama kawa kuelekea mission town downtown kusaka uchache wa kununulia kauzi na sembe. Katika ndoto ile niliota nikiwa mkuu kweli kweli tena baada ya kushinda uchaguzi kwa kishindo.
Niliota eti baada ya kumalizika uchaguzi na baadhi ya washirika zangu kubwagwa, niliamua kuwapa ukuu wa kijiwe kwa ngazi ya mikoa. Pia katika ndoto hii wapo niliowapa ulaji kutokana na kuuokoa utawala wangu wakati ulipotaka kuangushwa na tume ya Mwakiwembe ambaye naye nilimpa ulaji kama shukrani.
Nadhani wasomaji bado mnaikumbuka kamati ya kijiwe ya Mwakiwembe iliyochunguza upoteaji wa kashata na mkaa ambapo waziri mkubwa kijiwe bwana Ewassa alitimuliwa ili kunioka mimi. Basi mwenzenu ndoto ya ukuu ilichanganyikana na yale yaliyotokea wakati wa kamati ya Mwakiwembe wakati ule Microphone wa kijiwe akiwa Sam Sixx ambaye naye ilibidi nimpe ulaji ili atulize kiherehere chake cha kutaka ukuu wa kijiwe. Six asiwazuge, naye nimempa ulaji baada ya kukubaliana asijiunge na Chama Cha Jeuri (CCJ) ambacho hapa kijiweni ni kundi la wanakijiwe wakongwe.
Katika ndoto hii niliota nikitoa ukuu wa mkoa wa kijwe kwa sister Stella Artois Matomatoes kutokana na kushirikiana na Mwakiwembe kuficha siri za kijiwe ambazo zilimaanisha kuangusha utawala mzima wa kijiwe na kuzihamishia kwa Ewassa.
Katika ndoto hii pia nimemteua Mwanatunu Baki Shemahiza na Joe Flag ili kuhakikisha wanakuwa kwenye ulaji wasije wakamwaga siri zetu. Niliota eti katika kuteua niliwapendelea washirika zangu hasa Ndata. Mnahabari mimi ni ndata kitaaluma. Nimepiga kwata sana kule Munduli na kupewa cheo cha Luteni Kano?
Niliota eti kuwa washikaji kama Fatie Mawasa na wengine ambao siwataji niliwapa ulaji ili nikitembelea vijiwe vya huko basi wanilinde.
Kuna kitu kilinikera na kunifedhehesha katika ndoto yangu. Nilifedheheka nilipogundua kumbe nilifanya makosa kuwateua watoto wa marafiki zangu na kuonyesha mfano mbaya wa kurithishana ulaji. Niliposoma majina kama Rehemia Nchimvi dada yake Emmy Nchimvi, Leo Gamaa na wengine wenye majina na koo kubwa nilijiona kama jinga vile. Lakini ningefanyaje iwapo nilikuwa nimeishapitisha?
Na kweli. Walevi watakuja kunistukia na kuniadhiri. Ukiangalia majina kama Mape Ninaye, Hoseni Muinyi, Jan Makambale na vitegemezi vingine ambavyo tumevipa ulaji sirikalini na chamani, unaweza kukubaliana nami kuwa kujisuta kwangu kuwa mimi ni wa hovyo ni kweli.
Baada ya kukumbuka blunder hii nilijiona dikteta kama M7 wa UG na Mutalaka wa Dziko la Bwino ambao waliwapa ulaji wadogo zao, watoto wao hata wake zao. Hata hivyo hatutofautiani ikichukuliwa kuwa Bi Mkubwa naye ana ulaji wake wa Ki-NGOs unaotokana na nafasi yangu ya kuwa mwenyekiti wa kijiwe.
Mie katika ndoto yangu nilimpiku Mutalaka wa Dziko la Bwino. Kwani yeye alimteua mdogo wake Peter wakati mie niliteua makumi ya watu wangu wa sirini na hadharani. Pia Mtalaka hana kitegemezi chake kinachotesa kwenye Chama chake kama mimi nilivyo na kitegemezi kinachotesa kwenye kijiwe changu cha kahawa. Mutalaka ana PhD ya kusotea wakati mie ninayo ya kugawiwa. Yeye alisotea mie nikapata kiubwete. Upo hapo mwanawitu?
Pia katika ndoto hii niliota tukimuangukiwa Kanji al maarufu Rostitamu yule Mhindi wa kijweni ambaye alisababisha upotevu wa mapesa kibao ya kahawa kwenye mchoro wa HEPA kipindi tukielekea kwenye uchaguzi wa kijiwe. Maskini wanywa kahawa hawakujua kuwa ponjoro huyu alitumiwa nami kutekeleza mchezo mzima ili nisijulikane na kuumbuka!
Huwezi kuamini kuwa niliota kuwa Dungong Denjaman Makapu Tunituni alikwenda sehemu sehemu akachafua hewa! Niliota nikimzaba makofi Tunituni kama yule jamaa wa Chama Cha Mafisadi aliyefumaniwa kule Igunga akila urodi wa kada wa chama chake.
Hawa jamaa wana hatari. Yaani kada anakula uroda wa mke wa kada na bado wanaendelea kuwa makada badala ya kukandamizana na mapanga! Kama ni njaa na dharau na kujidhalilisha na kudhalilishana huku kumezidi.
Mie naapa haki ya nani, hata kama ni nabii Suleimani. Nikikuta unakula urodi wa nke wangu napiga mipanga bila kujali kuwa naweza kunyongwa. Heri kunyongwa kuliko kuwa shahidi wa bi mkubwa kuliwa urodi wangu. Lo! Acha niachie mambo ya urodi hapa nisijeleta balaa kwa wasomaji. Kama mmeudhika mezeeni pia someni nisemayo na siyo niandikayo.
Ngoja niendelee kuwasimulia ndoto yangu. Niliota, kumbe kumekucha!
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 21, 2011.
No comments:
Post a Comment