The Chant of Savant

Thursday 8 September 2011

Tangu leo sitacheka tena

Baada ya kugundua walevi wamenuna kwa matatizo huku wezi wachache wakichekacheka, nimeamua kununa kuwaunga mkono. Kwa sasa wanamtamani rais Nunanuna na mbabe baada ya Chekacheka kuwaingiza mkenge. Pia ukichekacheka hovyo kama mwenye kiharusi, unatoa nafasi kwa mafisadi na majambazi kukuzoea kiasi cha kukutumia. Kuchekacheka kunafanya watu wengi wakudharau na kukuona kama mtu ambaye si makini wala serious. Hivyo, nimeamua kuchukia kinyume cha kucheka. Nafanya hivyo kama sifa mojawapo ya kuweza kupewa kura na walevi ambao uchaguzi ujao watafanya kinyume.

Nani amesahau kuwa muhula ule walevi waliangalia vicheko, ahadi za uongo na bashasha wasijue hata shetani ni bingwa wa kucheka? Kwa vile walevi wameishachoka urembo na mashauzi, imebidi nianze kununa ili nionekane, kwanza sicheki hovyo na pili nina sura mbaya kama yule rais mbabe bingwa wa mipasho na ubishi wanayemtamani.

Kuna msemo kuwa what matters is not how big your house is but how big your heart is. Nami nasema. No matter how big your smile is but how big your wrinkles are. My heart rich in angers not in dribs and drabs but full of the same. Hivyo, walevi wajiandae kuwa na rais anayenuna hata kwenye harusi na siyo yule waliyezoea anayecheka hata kwenye msiba. Tunahitaji mabadiliko. Mpayukaji I am for changes big changes so to speak. Kupitia kununa, niko tayari kuondoa kiza na kuleta mwanga. Sasa wapiga kura watachagua vicheko kwenye kiza au kununa kwenye mwanga. Mie nitawanunia mafisadi na kuwakamata hata kama baadhi yao watakuwa mke au watoto wangu na washirika zangu.

Kupitia kununanuna wauzaji wa wese waliojigeuza walanguzi hawatawanyonya wala kuwachezea watu wangu kwa kuwalangua wese. Nitakachofanya kwa wale watakaojifanya wana magamba manene ni kunyongelea mbali kabla ya kuruhusu vurugu za wese kuinyonga serikali yangu. Hakuna kitu kinanifanya ninune hadi kupata saratani ya akili kama kuona watu wangu wakilanguliwa wese wakati kwenye nchi za jirani bei ni za chini.

Kwa vile nitakuwa nanuna nuna hovyo, nchi nyingi hazitapenda kunipa mialiko. Hivyo sitasafiri wala kutalii hovyo na kupoteza pesa nyingi za walevi. Kwa vile nitakuwa nimenuna kila saa, hata mshirika wangu wa bedroom hataandamana nami iwapo nitakuwa na ziara ya lazima ughaibuni.

Pia kwa kununanuna naamini hata mawaziri nitakaowateua kwenye serikali yangu hawatafanya madudu kwa kuogopa nisiwapasukie. Hivyo, mawaziri vilaza kama Bill Ngelanija, Milima ya Kigoma, Makorongo Muhanga, Safia Lion, Hawa wana Ghasia, Semakombania, Shukrani kawa Mbwa, Jfour Majembe, Emmy Nchimvi, Bill Luku-mvi, Meli Nyago, Vurumai Nahodhi, Hosseni Mwuinyi, Stevu Wa Hasira na wengine hawataweza kunigeuza zoba la kuibia walevi kama ilivyo sasa.

Hata magabacholi wanaojichekesha kutokana na kuitikia vicheko hawatanipata. Maana akijifanya anataka appointment ya kukutana nami namtolea mihasira yangu na kumsweka lupango bila kuuliza. Bila kufanya hivyo, huwezi kuendesha kaya. Mara hii mmesahau mzee Mchonga alivyokuwa akinuna? Juzi nilikuwa nikipitia hotuba zake baada ya kuutwika. Nilisikiliza hotuba moja kamambe alipokuwa akitoa sifa za rais mpya baada ya mzee Ruksa. Alisema wazi. Lazima rais ajaye awe anachukia rushwa na akisema nachukia rushwa, ukiangalia usoni mwake unaamini kabisa huyu anachukia rushwa. Alionya kuwa kusema nachukia rushwa au nitawapeleka Kanani si jambo la maana iwapo anayesema hivyo anachekacheka na kuonyesha wazi anavyowatapeli walevi.

Sasa mimi nasema. Nachukia rushwa na ufisadi. Si kuchukia tu. Ukinitajia ufisadi ua rushwa nanuna nusura ya kupasuka. Mie nisemapo nachukia rushwa, inabisi mnielewe. Nikigundua kuwa waziri wangu hata mtoto wangu au mke wangu amekula rushwa au kuwa fisadi, lazima nimnyonge. Heri kumpoteza mpenzi au mtoto wangu kuliko kujiingiza kwenye vitendo vichafu na kupoteza heshima yangu.

Isitoshe, nikishachaguliwa kuwa rais ambaye si rahisi kama ilivyo, nitahakikisha naandika katiba upya na kutamka wazi wazi kuwa atayekula rushwa au kufanya ufisadi anyongwe mara moja. Pia nitahakikisha katiba inatamka wazi kuwa kwa mtumishi wa umma kushikiwa kunatosha kumuondoa mtu kazini au ofisini ili sheria zichukue mkondo wake. Hivvo ningekuwa nimeishaapishwa, watuhumiwa wote wa rushwa, ufisadi uwe wa fedha au elimu wangekuwa lupango wakingojea kunyongwa kama siyo kupigwa risasi kwenye viwanja vya Jangwani ili wengine wajifunze na kupokea onyo toka kwa rais Nunanuna Mpayukaji PhD isiyo ya kupewa wala kughushi.

Pia nitakapokuwa nimewashawishi walevi kwa ndita zangu na kuchaguliwa kuwa rais, nitahakikisha bunge linaendeshwa na spika mwenye elimu na hadhi na si vikaragosi vya mafisadi. Nitahakikisha bunge linakuwa na meno na hadhi badala ya kuwa rubber stamp ya kupitishia bejeti uchwara na madili ya mafisadi wakubwa wakubwa kama ilivyo katika baadhi ya nchi kwa sasa.

Juzi niliongelea majambazi manne yaani Ngelanija, Milima, Ruhani-njoo na Devil Jahiri. Kama ningekuwa rais tayari wangekuwa marehemu.ninaposema marehemu nieleweke, siyo kisiasa bali kibaolojia. Na nazidi kuwaahidi walevi kuwa mkombozi wenu niko mlangoni nachungulia ikulu kuja kuondosha uchafu na kuparejesha kuwa patakatifu pa patakatifu toka kwenye kuwa patakataka pa patakitu.

Wale wauza bwimbwi wakae mkao wa kuliwa. Mie sitashughulika na biashara hii haramu kwa kuwapiga baadhi ya watu vijembe. Nitanuna na kukamata wauzaji na kuonyesha hadharani ili nisipoteze muda wa majibizano ya kitoto. Sitataja majina ya wauza bwimbwi. Watajitaja wenyewe siku nikiwaonyesha kwa umma bila kujali nyadhifa zao au kama ni makafiri, mashehe, maaskofu au watakatifu. Mie nitasema kwa vitendo. Hivyo wauza bwimbwi kaa mkijua kuwa nikichaguliwa ndiyo mwisho wa biashara zenu.

Kwa kutumia kanuni ya kununa, nitahakikisha kila mwananchi anataja mali zake. Najua walevi wengi hasa wa uswekeni watataja chawa na mapanya kama mali zao. Poa kuliko wanaotaja au kuficha mahekalu ya wizi. Kwangu maskini anayekula jasho lake ni bora kuliko jambazi anayeishi kwa kunyonya wenzake kama kupe. Pia nalaani ule msemo wa kipumbavu kuwa mtaji wa maskini ni nguvu zake. Mtaji wa maskini ni raslimali za nchi yake. Kwanini mtaji wa maskini iwe nguvu yake ilhali mtaji wa wezi wenye madaraka ni jasho la maskini?

Hivi nikiwa rais mafisadi si watajinonihino kwenye nguo zao?

Naona Rahma ananibeep ili twende kujivinjari kwenye kiza.
Usimwambie mtu.

Chanzo: Tanzania Daima Septemba 7, 2011.

No comments: