The Chant of Savant

Thursday 8 September 2011

Ningekuwa Jakaya ningebuni dhana ya kuvaa gamba

Tukiacha unafiki sanaa na kujidanganya, hakuna gamba nene na zito kama Jakaya Kikwete miongoni mwa magamba yaliyopo nchini na kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mujibu wa List of Shame ya Dk. Wilibrod Slaa ya Mwembe Yanga ya Septemba 15, 2007. Hasa tukiangalia chanzo kilichoibua magamba ambayo kwa sasa CCM kimeshupalia, tunagundua kuwa hakuna gamba isipokuwa Kikwete. Hebu tukumbushe kwa kujierekeza kwenye mkutano wa hadhara kule Mwembe Yanga Dar es salaam wa Septemba 15, 2007 ambapo msemaji mkuu ni Dk Wilibrod Slaa katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Bila woga, Dk. Slaa anawataja mafisadi wanaolisumbua taifa letu. Katika orodha hiyo kuna Jakaya Kikwete kama kiongozi na mnufaika mkubwa wa ufisadi huu hasa ule ujambazi wa EPA.

Baada ya CHADEMA kufyatua kombara hili, wengi wa waliotuhumiwa mafisadi walitishia kwenda mahakamani kujisafisha ingawa baadaye waligwaya. Katika kundi la waliofurukuta kutishia kwenda mahakamani Kikwete hakuwemo. Yeye, kwa sababu azijuazo na kwa makusudi mazima, alichagua kukaa kimya! Wanasheria hapa wanasema circumstantial evidence applies though silence is not necessarily to plead guilty.

Je ni kwanini Kikwete alichagua njia ya kukanganya na ya hatari ya kujikanyaga na kukaa kimya kama hakushiriki? Je kweli hakushiriki ufisadi wa EPA ambao unamshusisha hata mtangulizi wake yaani Benjamin Mkapa? Je hakunufaika na ufisadi huu? Je Kikwete atajificha nyuma ya ukimya hadi lini na kwanini kama hakushiriki wizi wa EPA? Je hii ni mbinu salama huko tuendako ambako kiongozi wa zamani anaweza kufikishwa mahakamani kama ilivyotekea Malawi na Zambia?

Iwe ni kwa woga, kujikomba au unafiki wa kawaida, wengi wamekuwa wamkimshauri rais Kikwete kuwatimua mafisadi ilhali wakijua hawezi kufanya hivyo kutokana na sababu nyingi tu. Kimsingi, tunapaswa kumwambia Kikwete, tena bila kuzungusha wala kumung’unya maneno, kuwa naye ajitimue. Je kwa siasa uchwara kama alivyosema Rostam Aziz mnufaika mkuu wa ufisadi, Kikwete atajitimua au umma umtimue? Kwani yu gamba tena nene. Kwa lugha rais ni kwamba Kikwete ni gamba-kikwazo. Najua hawezi kujivua gamba mwenyewe hadi pale yaliyotokea Libya, Misri na Tunisia yamfike mlangoni mwake. Je itawezekana wakati watanzania nao ni magamba kwa namna yake? Japo inataka ujasiri wa mwendawazimu, potelea mbali, acha niwe wa kwanza kumvisha kengele paka kwa kumtaka ajivue mwenyewe kabla ya kuwavua wengine magamba.

Je inaingia akilini kumwambia gamba awavua magamba wenzake wakati lao ni moja nyuma ya pazia? Je anao ubavu wa kuwavua wenzake magamba akabaki salama? Je akiwavua wenzake magamba yeye atabaki salama hasa ikizingatiwa kuwa wanajua mambo yake mengi ambayo asingependa mtu yeyote ayajue hasa wananchi anaowaaminisha kuwa anafaa wakati hafai? Tuache utani. Hivi tunategemea CCM imvue mtu gamba wakati chama chote ni magamba matupu hamna mtu mle bali agamba?

Leo tunalalamika ulanguzi wa mafuta na umeme wakati nyuma ya pazia tunaowalalamikia ndiyo hao hao wanufaika.

Leo tunapiga kelele kumtaka Kikwete awashughulikie mafisadi kama wale wa EPA wakati ameingia madarakani kwa pesa hiyo hiyo ya EPA iliyowezeshwa na wawezeshaji wake! Ni ajabu na aibu. Wanaodhani ninamzushia wajiulize swali jepesi la kwanini Kikwete tangu shutuma za kuingia madarakani kwa pesa ya EPA ziibuke hajawahi kujitetea wala kuzijadili kama ni za uongo? Je ukimya hautoshi kutupa ukweli? Hivi mnadhani Kikwete ni mtoto mdogo kiasi cha kuzushiwa akubali jambo ambalo hakutenda? Can he allow himself to go down in flames? Tabia ya binadamu inajulikana awe mweusi au mweupe mtawala au mtawaliwa. Mtu yeyote akizushiwa jambo hawezi kunyamaza yaishe. Ukiona kanyamaza jua kuna ukweli kwa kiasi kikubwa kuliko uongo. Je ukimya wake unamaanisha nini zaidi ya kuthibitisha madai na shtuma? Je watanzania watakomaa lini na kuuangalia ukweli kama ulivyo hata kama unauma?

Ukiachia mbali kushiriki ufisadi wa EPA, Kikwete anakuwa gamba zito kutokana na matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma hasa kupenda ziara na kuwaachia wateule wake wajifanyie watakavyo. Rejea kujaza mawaziri mizigo wengi kwenye baraza lake la mawaziri. Hivi mawaziri kama Hussein Mwinyi, William Ngeleja, Ezekiel Maige, Vuai Shamsi Nahodha, Hawa Ghasia, Celina Kombani, Sofia Simba, Jummanne Maghembe, Shukuru Kawambwa na manaibu wao wanapaswa kuwa ofisini wakati wamevurunda kupita kiasi?

Pamoja na kustumiwa kuwa yu dhaifu na serikali yake ni legelege, Kikwete ameendelea kulegea zaidi kiasi cha kukatisha tamaa kwa watanzania. Uchumi unazidi kuporomoka huku ufisadi ukiongezeka kama ilivyofichuliwa hivi karibuni bungeni ambapo mamia ya wanyama yametoroshwa huku serikali ikiangalia na kujikanyaga. Leo tunaongelea mamia ya wanyama waliotoroshwa siku moja. Je wameishatoroshwa wangapi na kwa muda gani bila kujulikana? Je ni madini kiasi gani yameishatoroshwa kwenye mchezo huu?

Kikwete ameshutumiwa kuwa mbabaishaji. Ajabu ameendelea kuwa mbabaishaji zaidi. Angalia alivyojikanyaga hivi karibuni kuhusiana na watuhumiwa wa magamba kukataa kata kata kujiondoa kwenye nyadhifa zao. Hata mmoja aliyejitoa bado anaendelea kutesa huku akishirikishwa kwenye kampeni za mrithi wake kule Igunga! Huku ni kujipiga mtama na kuthibitisha madai kuwa siasa za sasa ni uchwara. Rostam aziz kadai na hakuna aliyempinga wala kumkaripia! Hii maana yake ni kwamba anachosema rostam ni kweli.

Hata hivyo tunaweza kumpongeza Jakaya kwa kuruhusu joka kuu yaani CCM ifie mikononi mwake. Kama ataendelea na kasi hii ya kukiua chama ipo haja ya kumsamehe makosa yake baada ya wapinzani kuchukua nchi na kuilekeza inakopaswa kuelekea.

Hakika ningekuwa Kikwete ningebuni na kutangaza sera ya kuvaa magamba zaidi badala ya usanii wa kujivua magamba.

Chanzo: Tanzania Daima Septemba 7, 2011.

No comments: