How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Thursday, 15 September 2011
HIVI karibuni, Rais Jakaya Kikwete, alikiri waziwazi kuwa nchi inanuka rushwa. Alikaririwa akisema: “Sasa hivi kila kona rushwa, ukienda barabarani polisi wanaomba rushwa, watendaji wakuu wa serikali wanachukua rushwa na makandarasi nao wanatoa rushwa ili waweze kupata zabuni. Ni tatizo, lazima tuikemee, itatufikisha kubaya.”
Kukiri kwa Rais Kikwete kuwa nchi inanuka rushwa kila kona na idara, hakutoshi. Ni jambo la kufurahisha kuwa hatimaye rais amekubali kuwa serikali yake imejaa rushwa. Pia ni jambo la kuhuzunisha kuwa na rais mwenye tabia ya kulalamika bila kuchukua hatua. Kukiri na kulalamika haitoshi. Kinachotakiwa ni rais kuchukua hatua. Rais na wapambe wake ambao wamekuwa wakiwachukulia kama wachochezi hata maadui waliothubutu kusema hili. Sasa ni wazi kuwa maji yamefika shingoni.
Kama alivyokiri rais, ni kweli kwa sasa kila kona kuna rushwa. Ikulu kuna rushwa, bungeni kuna rushwa, mahakamani kuna rushwa hata makanisani.
Kwenye NGO kuna rushwa na hata Misikitini kuna rushwa. Kama rais analijua na kuliona hili, kwanini alalamike badala ya kuonyesha amefanya nini kupambana na uchafu huu anaokiri kuuona na kuujua? Je, kulalamika ni jibu au ulegelege ambao wapinzani wanausema kuwa serikali ya Kikwete inao?
Kwa ukumbusho tu, rais aliwahi kukiri mwenyewe kuwa ana orodha ya majambazi, wauza unga, wala rushwa na wahalifu wengine. Cha ajabu ni kwamba, pamoja na mamlaka aliyo nayo, rais hajawahi kuwashughulikia angalau hata mmoja. Sasa kama rais anakiri kuwa anawajua wahalifu tajwa na hawashughulikii, wananchi wasio na mamlaka wala vyombo vya dola wafanyeje? Je, hii haiwezi kuwa mwanzo na mzizi wa watu kujichukulia sheria mkononi huku wateule wake wakizivunja hata kudharau mahakama kama ilivyotokea kwa katibu wa ardhi, Patrick Rutabanzibwa?
Hebu tuangalie nukuu nyingine ya rais Kikwete, aliyekaririwa akisema: “Katika sekta ya ununuzi wa mali za umma ndiyo kabisa, wanaagiza mali za serikali kwa kuongeza gharama, kuweka cha juu, ili wakifanikiwa waweze kugawana huku wakifahamu kwamba fedha zinazotumika ni za serikali. Lazima watendaji kama hao waangaliwe kwa umakini sana kwa sababu wanaweza kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.”
Kumbe rais anajua hata sekta zinazokumbwa na mdudu rushwa kwa viwango vya kutisha lakini hachukui hatua! Swali linaloulizwa kila wakati ni kwanini rais hataki kuchukua hatua? Kwenye ngwe yake ya kwanza hakuchukua hatua. Hii ni ngwe ya lala salama. Je, rais atawashughulikia lini hawa wahalifu aliowageuza ‘souvenir?’
Mwandishi nguli, Mark Twain, alituachia wosia kuwa: “Ni heri kustahiki heshima ukaikosa kuliko kuwa nayo wakati hustahili.” Hatutaki rais wetu afikie huko. Maana kwa cheo chake na hadhi yake, si mtu wa kulalamika bali kutenda. Ingawa watu wakimkumbuka marehemu baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere, wanaonekana kufikiri kurudi nyuma, ukweli ni kwamba alituachia urithi usio kifani.
Nyerere hakuwa mtu wa kulalamika lalamika bali kutenda bila kujali kuna watakaomlaumu au kumpenda. Yeye aliangalia haki badala ya upuuzi mdogomdogo kama kujuana na kuogopana.
Rais anapolalamika, licha ya kujidhalilisha, anatoa mwanya kwa wahalifu kuendelea na ‘business as usual.’ Maana wanajua alivyo legelege na mwoga. Hatutaki kuamini kuwa rais wetu ameshafika huko hata kama anaelekea huko au alifika zamani kutokana na haya tunayoshuhudia. Je, hicho ndicho kile alichosema Edward Lowassa, kuogopa kufanya maamuzi magumu? Je, haya ndiyo maamuzi magumu wazee wa CCM walimtaka rais afanye ? Kwanini rais anakuwa mwepesi wa kufanya maamuzi magumu angamizi kama kuendelea kuvumilia ufisadi na uhalifu mwingine? Je, rais wetu anataka akumbukwe kwa hili baada ya kuwa ametoka madarakani? Je, kuna namna rais ananufaika na jinai hizi yarabi? Sitaki kuamini hivyo hata kama ni hivyo.
Rais wetu ana mapungufu. Ni binadamu anayepaswa kupewa msaada. Leo tunaongelea kukithiri kwa rushwa kila sehemu. Inashangaza hata naye anahusishwa, si mara moja wala mbili, tena bila kukanusha na akifanya hivyo anafanya mzaha kama tulivyosikia juzi juu ya hongo za suti. Kuwa mke wa Kaisari hupaswi kutuhumiwa. Kutuhumiwa tu kunatosha kujiwajibisha. Kutofanya hivyo ni kuonyesha ni kwa jinsi gani mtuhumiwa asivyo msafi. Je, hii ndiyo sababu ya rais kuendelea kukalia ushahidi aliosema alipewa na wahusika anawajua? Je, anaogopa na yake yasifichuke? Bila kuja na utetezi wa maana kuhusiana na kadhia hii, makaripio na matusi ya watetezi wake hayatafua dafu.
Katika sakata la kushutumiwa kuhongwa kwa mfano suti tano, ningekuwa rais, mtu wa kwanza kumfukuza kazi alikuwa mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, ambaye ametoa utetezi uchwara kwa mihemko badala ya kuingia kwenye madai na kuonyesha ukweli ni upi. Huwezi kumuita balozi mpuuzi bila kutaja upuuzi wake ni upi. Mbona mabalozi haohao wanapotoa misaada hamuwaiti wapuuzi? Dawa ya kuepukana na ‘upuuzi’ huu ni ‘ku-deliver’, badala ya kupuuzia kuwachukulia hatua mjaarabu wanaohujumu uchumi na taifa letu. Huwezi ukawa tegemezi, ukaotesha mapembe. Wanaokufadhili watayakata. Na isitoshe, uzoefu unaonyesha kuwa serikali ya sasa inapotuhumiwa, hurukia kuwaita wazushi, waongo na wapuuzi, wanaofanya hivyo.
Nani amesahau kuwa, Dk Willibrod Slaa, alivyoitwa mchochezi, mmbea, mpuuzi, mzushi na majina mengi mabaya kabla ya ukweli kuumka na kuwaacha watuhumiwa uchi wakivuana magamba? Kwa kuangalia historia hii, tukubali, tusikubali kwenye tuhuma lengwa kuna ukweli hata kama si mia kwa mia.
Nani mara hii kasahau ‘List of Shame’ ambayo imegeuka jinamizi kwa serikali na chama cha Kikwete huku naye akihusishwa? Haya ndiyo mambo ya kujadili kuangalia ni kwanini rais wetu anakuwa mtu wa kulalamika badala ya kuchukua hatua. Je, yeye ni salama? Je, nyumba yake na waliomzunguka nao ni salama? Tusimuogope wala kumdanganya kama watetezi na washauri wake. Wao wanatetea kitumbua, nasi tunatetea taifa.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 14, 2011.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment