How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Thursday, 29 September 2011
Bastola ya Rage angeonekana nayo Lema…
KITENDO cha hivi karibuni cha mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage, cha kupanda jukwaani na bastola kiunoni, si cha uungwana hata kidogo na hakiwezi kupita bila kujadiliwa.
Jaribu kufikiri. Kitendo hiki cha kihuni kingetendwa na mwanachama au mbunge yeyote wa upinzani kama Godbless Lema, Zitto Kabwe, Halima Mdee (CHADEMA) au David Kafulila wa NCCR Mageuzi, polisi wangehaha vipi kumweka ndani? Majibu mnayo.
Nije kwenye hoja yangu. Kumiliki au kutomiliki bunduki kwa Mtanzania ni haki ya kila mmoja kulingana na masharti na vigezo vilivyowekwa ili kuwezesha mtu kumiliki silaha.
Kitendo cha Rage kupanda jukwaani na bastola kuomba kura kwa ajili ya chama chake kilikuwa na lengo ama kuwadharau au kutishia usalama wapiga kura. Bastola kwenye mkutano wa hadhara wenye ulinzi wa polisi ya nini? Jamani Igunga si Mogadishu.
Bahati mbaya Rage na wenzake wanaona fahari kuwa na silaha viunoni. Na hii imejionesha hata kwa wabunge wenzake, Aeshi Hilal (CCM) Sumbawanga na Ester Bulaya (CCM) Viti Maalumu ambao ama kwa ulimbukeni au kwa uzuzu wa kumiliki bastola, waliripotiwa kufyatuliwa risasi hewani usiku wa manane.
Ingawa kujilinda ni haki ya binadamu, bunduki zinapotumika kutishia amani zinapoteza maana ya kujilinda na kwenda kwenye kuhatarisha usalama.
Tanzania siyo Somalia ambapo usalama wa mtu uhakikiwa na mitutu iliyomzunguka. Kitendo cha Rage kugeuza bastola kuwa kivutio na kitu cha mzaha kinapaswa kuziamsha mamlaka na kumfutia leseni ya kumiliki silaha hiyo.
Maana kwa tabia aliyoonesha ni wazi kuwa hana sifa za kuruhusiwa kumiliki silaha.
Kwa wanaojua umuhimu wa bastola, imetengenezwa kwenye umbo dogo ili kuweza kufichwa kirahisi kiasi cha kutomstua adui au watu wengine mwenye kuwa nayo anapokuwa nao. Mkutano wa hadhara hauna tofauti na baa. Unapoingia na silaha bila kuwa na mamlaka kisheria ya kufanya hivyo, unatishia amani.
Hii ni hatari kwako na wale waliokuzunguka. Hili ni kosa linalotosha kumsababishia mwenye kumiliki silaha kunyang’anywa haki ya kuwa nayo ukiachia mbali kufunguliwa mashitaka mengine yaendanayo na kutumia vibaya silaha na kutishia amani.
Kimsingi, kumilki silaha si haki kwa maana ya ‘right’ bali ‘privilege’, yaani haki ambayo haiwezi kudaiwa mahakamani.
Sasa tujiulize. Rage alikuwa anawahofia maadui wapi iwapo watu aliolenga kuongea na kuwa nao walikuwa ni wapiga kura? Je, Rage aliamua kwa maksudi kupanda jukwaani na silaha ili kuwatisha wapiga kura? Hizi ndizo mbinu za CCM za ushindi?
Je, Rage alipopewa silaha hakufundishwa masharti ya kumiliki zana hii hatari? Je, kwa mazingira ya mkutano wa kisiasa, kweli kulikuwa na tishio au ulazima wa kuingia kwenye eneo la mkutano na kupanda jukwaani na silaha? Tunaipeleka wapi Tanzania?
Je, kitendo cha Rage hakiwezi kuiathiri CCM, kama itashinda uchaguzi, kwa kigezo kuwa wapiga kura walitishwa?
Uchaguzi hauwezi kuwa huru na haki wakati kuna watu tena wapiga kampeni wanaingia kwenye mikutano na kupanda majukwaani na silaha viunoni. Maana kiakili ni kwamba mkutano wa kampeni ni sehemu ya amani ambapo wanaoruhusiwa kubeba silaha kwenye eneo hilo ni polisi tu na si vinginevyo.
Kwanini Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, ameamuru uchunguzi badala ya kumweka ndani kwanza huyu mvunja sheria? Hili halihitaji tafsiri za wanasheria. Kuingia kwenye ‘public gathering’ na silaha ni kuvunja sheria. Ni kosa la jinai ambalo mwenye kulitenda hupaswa kukamatwa na polisi na kuchukua maelezo yake na kumfungulia mashitaka. Je, kwanini polisi hawakumkamata na kuchukua hatua zinazopaswa kuchukuliwa kisheria hadi bosi wao achukue hatua?
Je, polisi wa namna hii wasiojua hata wajibu wao au kama wanaujua na kuwagwaya mabosi wao wanaweza kuaminika kusimamia uchaguzi bila kuibeba CCM? Maana kwa kitendo cha kumfumbia macho Rage ni ushahidi tosha kwa polisi kuwa wanalalia upande wa CCM?
Kwa tabia waliyonesha polisi, imewaondolea heshima na imani kiasi cha kuonekana wahuni kama kina Rage na wenzao wanaodhani silaha ni mwanasesere kwa watu wazima wenye akili za kitoto kuchezea mbele ya kadamnasi kama ilivyotokea Igunga.
Binafsi nalaani kitendo hiki cha kihuni na kigaidi. Tanzania tunapaswa kujiepusha na siasa za kijinga za Somalia, Afghanistan, Pakistan na kwingineko kwenye vurugu kutokana na ujinga wa wachache kukabidhiwa silaha. Rage awe fundisho kwa wengine wenye agenda za siri za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kijambazi.
Ni hatari kwa kitendo cha kihuni kama hiki kutendwa na mtu anayeitwa mheshimiwa mbunge wakati hana wala hastahili. Utastahilije heshima wakati umeshindwa kujiheshimu?
Kuna haja ya kuibana wizara ya mambo ya ndani ili itoe maelezo yanayoingia akilini badala ya kuunda tume za ujanja na ukweli wakati kosa lililotendeka halihitaji tume bali kumweka ndani mhusika na kumfikisha mahakamani.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 28, 2011.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment