How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 6 October 2012

Muungano hautavunjwa kwa shinikizo la Uamsho




AKIHOJIWA na Malcom Webb wa Al Jazeera, Mselem Ali Mselem aliyedaiwa kuwa kiongozi wa uamsho alipodaiwa atoe sababu ya kutaka Zanzibar iondoke kwenye muungano, alisema eti mila ya watu wa bara na visiwani ni tofauti. Jibu hili lilitoa picha ya ajabu sana.
Baada ya kumhoji Mselem, Webb alirusha picha ya watu wanaofanya vurugu huku polisi wakirusha risasi. Pia alionyesha kipande cha mtu anayewataka watu wadai nchi yao akisisitiza kuwa wangetaka kuwe na serikali ya Kiislamu.
Angalau hapa ndipo nilipoanza kupata picha halisi ya kile inachotaka kufanya Uamsho.
Ingawa kumekuwa na kelele nyingi kuhusiana na ama kurekebisha au kuvunja muungano, wanaopiga kelele hawana hoja ya msingi hasa kwa hili la pili la kuvunja Muungano.
Kwanini sisi tuvunje muungano wakati wenzetu wenye nguvu na wanaotufadhili kama Ulaya wakiungana? Kwanini kufikiria kuvunja muungano huku tukijaribu kuunganisha Afrika Mashariki ili kuwa na sauti kiuchumi hata kisiasa?
Kama ni kuvunja Muungano, ieleweke kuwa hautavunjika kwa shinikizo la upande mmoja au kundi moja kama wanavyojitahidi kufanya Uamsho na mabwana zao.
Muungano kama ndoa ya watu wawili, haiwezi kuvunjwa kwa shuruti ya mmoja wa wanandoa bila kwenda mahakamani ambako ni Watanzania wote wa bara na visiwani.
Pia wanaoshabikia kuvunja Muungano wamekuwa wakiona kama visiwani wanahujumiwa na hivyo wasingekuwa chini ya Muungano huenda wangekuwa mbali kimaendeleo. Huu ni upuuzi. Pale Comoro kuna nini zaidi ya vurugu ambazo mara nyingi uhitaji msaada wetu kuzituliza? Madagascar kuna nini zaidi ya vurugu mtindo mmoja? Hiki ndicho wanachotaka hawa wasiopenda muungano?
Hata hizo nchi za kiarabu ambazo wengi wa wasiopenda Muungano hupenda kupigia mfano zimeungana. Kwanini hawaongelei Muungano wa Falme za Kiarabu yaani (United Arab Emirates)? Je, wanamdanganya nani? Wanakwenda mbali kama Mselem wakisema eti wanataka Serikali ya Kiislamu? Mbona hizo nchi zote tulizotaja zikiwemo na za jirani hazima huo utawala wa Kiislamu?
Waulize Misri, Tunisia na hata Libya ambapo ukiondoa Libya vyama vya Kiislamu vilishinda lakini vikasita kutangaza serikali za Kiislamu.
Zanzibar, kwa ajenda ya Uamsho, ina Uislamu gani wa mno kuliko hao waliouanzisha na kuueneza huko? Au ni yale ya kuwa mwanagezi mara nyingi hujifanya mjuvi kuliko mwalimu wake? Nani anataka Serikali ya Kiislamu kwenye karne ya demokrasia?
Ingawa Serikali ya CCM imekuwa kimya na legelege kuwashughulikia Uamsho, kosa la kutaka kuvunja Muungano ni uhaini tosha kwa vile suala hili haliwezi kuamriwa kihuni na genge la watu wachache wanaotumia mbinu za porini kama Uamsho.
Inashangaza kwanini serikali inatumia nguvu kubwa tena ya ziada kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani hasa CHADEMA, lakini serikali hiyo hiyo inashindwa kuwashughulikia Uamsho?
Je, ina faida gani na vurugu hizi za kihuni? Je, kwanini serikali inawalea Uamsho? Je, ni kwa sababu Uamsho wanaongea lugha moja na CUF ambayo ni mshirika wa CCM kwa sasa?
Rejea matamshi mengi ya kutaka kuvunja Muungano ambayo yamekuwa yakitolewa na Mbunge Ismail Jussa (CUF) mara kwa mara bila hata kukaripiwa na chama chake wala washirika wake.
Ingawa ni rahisi kwa watu wachache wasaka ngawira kudai tuvunje Muungano, tukithubutu watakaolia kwanza ni wale wale wanaotushinikiza tuuvunje.
Ingawa hili hawajawahi kuliona, wajiulize ni kwanini nchi zenye ardhi na uchumi mkubwa kuliko Zanzibar kama Kenya na Uganda wanalia tuungane nao wakati hiki kipande kidogo cha nchi hakiwezi kufika mbali peke yake?
Mfano mdogo ni kwamba kama tutasema tuvunje muungano na kuwaamuru watu wa visiwani warejee kwao, hapatakalika wala kutosha ukiachia mbali ugumu wa maisha kama bara ingeanza kutoza ushuru bidhaa zinazokwenda Zanzibar kama nchi nyingine ya kigeni.
Ingawa kila Mtanzania ana haki ya kutoa mawazo yake, lazima kuwepo utaratibu unaokubalika kisheria badala ya ghasia na uhuni.
Kwa mfano, wenye kuja na hoja lazima wawe wamesajiliwa kisheria na kujulikana shughuli zao. Je, Uamsho wamekidhi kigezo hiki na wanamuwakilisha nani kisheria zaidi ya kuleta vurugu?
Ingawa CCM imekuwa ikijifanya kama haioni hatari ya harakati za wana Uamsho, kuna siku itajikuta njia panda isijue la kufanya na la kuacha.
Je, huu ni mtihani wa mwisho kwa CCM baada ya kukosa uongozi madhubuti wa kuweza kushughulikia masuala ya Muungano ukiachia na mambo mengine ya muhimu kwa taifa?
Kwa ufupi ni kwamba wanaotaka kuvunja Muungano wafuate taratibu za kisheria ambapo ni kwa pande mbili kukubaliana na kuamua kipi cha kugawana na kipi cha kubakisha. Kinachogomba ni kwamba uzoefu umeonyesha kuwa nje ya Muungano, Visiwani itakumbwa na vurugu kiasi cha kuilazimu Bara kuingilia tena hasa kijeshi kutokana na Visiwani kutokuwa na jeshi wala mamlaka kamili ya kuweza kujiendesha kama nchi.
Hili linakera na kuuma, lakini ndiyo ukweli. Pia kama la kuvunja Muungano lingefanikiwa basi CUF ingekuwa imepata ambacho imekuwa ikikitafuta. Rejea kwa CUF kuwa na nguvu upande mmoja wa Muungano na katibu wake mkuu kuwa kila kitu.
Nimalizie kwa kuwashauri wanaotaka kuvunja muungano wafahamu wanafanya uhaini ambao adhabu yake mara nyingi ni kubwa kama hawatataka kufuata taratibu za kisheria.
Je, ni kwanini serikali inaendelea kuulea huu uhalifu wakati mojawapo ya viapo vya Rais wa Jamhuri ya Muungano ni kulinda mipaka na nchi ya Jamhuri ya Muungano dhidi ya maadui wowote wawe wa nje au wa ndani? Wakati wa kuwashughulikia wanaotaka kuvunja Muungano kihuni ni sasa. Tusingoje uchaguzi wa mwaka 2015.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 6, 2012.

4 comments:

Anonymous said...

Zanzibar bila ya muungano inawezekana na ilikuwa hivo.

kabla ya nyerere kumtisha karume kenge. ukimwona kobe juu ya mwembe ujuwe kapandishwa. muungano hauna kheri yoyote kwa zanzibar.
mkoloni mtanganyoko

Anonymous said...

“Mimi sitafuni maneno kwamba ni muumini wa Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na mashirikiano kati yake na Tanganyika kupitia Muungano wa Mkataba. Namshangaa leo anakuja kiongozi wa Zanzibar anasema tuna bendera na muhuri na wimbo wa taifa, hayo yanatosha. Hivi huyu anajua anachokisema au anatumikia maslahi ya waliomtuma? Una bendera gani hii ambayo mwisho wake Chumbe? Mimi nataka niione bendera ya Dola ya Zanzibar inapepea Umoja wa Mataifa, New York pale. Nataka tuwe na Paspoti ya Zanzibar, nikisafiri nitoe Paspoti ya nchi yangu. Nataka tuwe na Ofisi za Kibalozi za Zanzibar katika nchi za nje.

Leo hata mamlaka ya kiuchumi hatuna. Tumeamua rasilimali yetu ya mafuta na gesi asilia yasiwe mambo ya Muungano, mpaka leo Tanganyika wamekwamisha, wanatuzuia tusinufaike na rasilimali zetu tukajenga uchumi wetu. Wanasema tuna viwango na mfumo mmoja wa kodi lakini bidhaa zikitoka Zanzibar wanazitoza ushuru tena. Lengo ni kuua uchumi wetu ili hatimaye tudhoofike na tusalimu amri kwao. Yaguju! Wasahau hilo. Leo hata katika mikutano ya kimataifa, viongozi wetu wa Zanzibar

Anonymous said...

“Mimi sitafuni maneno kwamba ni muumini wa Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na mashirikiano kati yake na Tanganyika kupitia Muungano wa Mkataba. Namshangaa leo anakuja kiongozi wa Zanzibar anasema tuna bendera na muhuri na wimbo wa taifa, hayo yanatosha. Hivi huyu anajua anachokisema au anatumikia maslahi ya waliomtuma? Una bendera gani hii ambayo mwisho wake Chumbe? Mimi nataka niione bendera ya Dola ya Zanzibar inapepea Umoja wa Mataifa, New York pale. Nataka tuwe na Paspoti ya Zanzibar, nikisafiri nitoe Paspoti ya nchi yangu. Nataka tuwe na Ofisi za Kibalozi za Zanzibar katika nchi za nje.

Leo hata mamlaka ya kiuchumi hatuna. Tumeamua rasilimali yetu ya mafuta na gesi asilia yasiwe mambo ya Muungano, mpaka leo Tanganyika wamekwamisha, wanatuzuia tusinufaike na rasilimali zetu tukajenga uchumi wetu. Wanasema tuna viwango na mfumo mmoja wa kodi lakini bidhaa zikitoka Zanzibar wanazitoza ushuru tena. Lengo ni kuua uchumi wetu ili hatimaye tudhoofike na tusalimu amri kwao. Yaguju! Wasahau hilo. Leo hata katika mikutano ya kimataifa, viongozi wetu wa Zanzibar

Cruztkgn said...

“Mimi sitafuni maneno kwamba ni muumini wa Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na mashirikiano kati yake na Tanganyika kupitia Muungano wa Mkataba. Namshangaa leo anakuja kiongozi wa Zanzibar anasema tuna bendera na muhuri na wimbo wa taifa, hayo yanatosha. Hivi huyu anajua anachokisema au anatumikia maslahi ya waliomtuma? Una bendera gani hii ambayo mwisho wake Chumbe? Mimi nataka niione bendera ya Dola ya Zanzibar inapepea Umoja wa Mataifa, New York pale. Nataka tuwe na Paspoti ya Zanzibar, nikisafiri nitoe Paspoti ya nchi yangu. Nataka tuwe na Ofisi za Kibalozi za Zanzibar katika nchi za nje. Leo hata mamlaka ya kiuchumi hatuna. Tumeamua rasilimali yetu ya mafuta na gesi asilia yasiwe mambo ya Muungano, mpaka leo Tanganyika wamekwamisha, wanatuzuia tusinufaike na rasilimali zetu tukajenga uchumi wetu. Wanasema tuna viwango na mfumo mmoja wa kodi lakini bidhaa zikitoka Zanzibar wanazitoza ushuru tena. Lengo ni kuua uchumi wetu ili hatimaye tudhoofike na tusalimu amri kwao. Yaguju! Wasahau hilo. Leo hata katika mikutano ya kimataifa, viongozi wetu wa Zanzibar