The Chant of Savant

Saturday 19 July 2014

Mlevi ampongeza Riziwani kuwapasha makanjanja

Bwana Riziwani,
Baada ya kutundika mibangi na gongo naomba nichukue fursa hii kukupongeza kwa kuwatolea uvivu makanjanja wanaokosoa utawala wa dingi wako. Well done and bravo plus kudos mtu wangu.
Nillikusikia ukisema, “Asilimia kubwa ya waandishi tuliokuwa nao ni makanjanja, ni ukweli kabisa wanapokaa kwenye meza zao wanaandika vitu tu, wanapokaa kwenye ofisi zao wanaandika vitu tu, yaani mtu anapikapika tu vitu.”  Usemayo ni kweli. Kwanini wasiwe makanjanja kama hawakusifu na mema yote ambayo serikali ya baba yako imefanya? Mfano, dingi aliwaahidi maisha bora kwa wote na kweli wote wana maisha bora. Rejea alivyogundua kuwa hili limefanikiwa kutokana na kuwapo mikangafu mingi barabarani kiasi cha kusababisha misongamano. Je huu si ushahidi kuwa maisha bora kwa wote yapo? Nani haoni misingomano ya mikangafu?
Nakubaliana nawe. Waandishi wengi ni makanjanja wanaopika mambo kama walivyofanya mwaka 2005 ambapo katika ulingo wa siasa tuliambiwa kuwa hata wababaishaji na mihimili ya ufisadi ni vipenzi vya watu na chaguo la Mungu lililoishia kuwa pigo la Mungu kwa watu kutokuwa makini.
Ridhiwani usemayo ni kweli. Waandishi hawajui kuwa siku hizi kuwa kanjanja siyo kutokuwa na elimu kama zamani bali kukosa shukrani ya kuisifu serikali ya mzee. Yaani watu wanashindwa hata kughushi wakati hata mawaziri wanaghushi na hakuna anayewashughulikia? Hakika huu ni ukanjanja wa kujitakia. Kwanini wasiimbe sifa kwa wenye mamlaka nao wakawapa ulaji kama wale nguli wa 2005 ambao baadhi yao tunawaona wakitanua kwenye ulaji kama malipo na fadhila ya uimbaji wao mahiri wa sifa za watukufu wenye ulaji? Baada ya kusoma karipio lako nilisikia watu wakihoji ukweli wake eti kwa vile halikuwa na takwimu zozote. Nani anataka takwimu usawa huu kuumiza kichwa wakati mtu anaweza kujisemea kwa kujiridhisha na akajihisi ametenda haki wakati siyo? Wapo makanjanja wanaohoji maana ya “asilimia kubwa” wakiuliza “asilimia kubwa” kulinganisha na ipi? Wapuuzie. Hawajui utukufu wako hawa.
Hivi hawa wanaoona kama umewakosea adabu waandishi wanaishi dunia gani? Kwanini hawaendi kuwauliza wenzao akina Salva Rweyemaamu na Prinsi Bageeenda magwiji walioamua kuchapa kazi kwa kuwaponda wale wote walioonekana kuwa tishio kwa mzee hadi wakakubuhu kuwa nguli? Huwezi kuwa nguli bila kusifia wenye madaraka vinginevyo umehongwa na wapingaji. Yoyote asiyeimba sifa za mzee jua ni kanjanja. Maana, kama wanaofanya hivyo wanapata ulaji kwenye ofisi za wilaya za chama hata kwenye ikulu, kwanini hawa, kama si makanjanja, wanajivunga kuchangamkia ulaji? Kipindi fulani niliwahi kuwasikia baadhi ya makanjanja wakiwatukana nguli kuwa ni nepi wanaoweza kufanya kazi yoyote au dirty laundry. Kwani dhambi kuwa nepi? Nani anaweza kuishi bila nepi hasa utotoni?
Juzi nilimsikia fyatu mmoja akihoji u usomi wako akisema eti hta hiyo  masters ya sheria anayodai kuwa nayo ameisomea baada ya baba yake kuukwaa urais. Eti wanasema unaweza kuwa ulighushi hasa ikizingatiwa kuwa hujawahi kuifanyia kazi. Wanakwenda mbali na kusema kuwa nawe ni kanjanja wa kisiasa aliyetumia jina la baba yake kupata ukubwa. Kwanini nao wasitumie majina ya baba yao waone kama yanalipa? Eti wanasema kuwa msomi aliyeiva hawezi kutegemea jina la baba yake zaidi ya taaluma yake. Hawa wamepitwa na wakati na ni wavivi wa kufikiri wasiojua kuwa mambo siku hizi yamebadilika hasa usawa huu wa madili na ulaji wa kifamilia na kichama.
Hivi namneno yako haya ambayo nayanukuu kweli ni ya kupingwa au kutiliwa shaka? Ulisema, “Mimi ningependa sana kuwasihi waandishi wetu hebu kidogo tuandike vitu vinavyofanana na hali halisi, hatusemi kuwa watu wanapofanya mabovu wanyamaziwe, hapana, wabovu waandikwe na mabovu yao, wanapofanya mazuri wasifiwe ili kuendelea kutiana moyo katika kulijenga taifa.”  Baada ya kulinukulia maneno haya kanjanja fulani lilisema eti waandishi wana jukukumu la kuusemea umma na si kufisia serikali ambayo ina waajiriwa kwa kazi hiyo.  Liliongeza kusema eti nyani haoni nonihino lake. Lilirudia swali lile lile likisema, “Mbona Ridhiwan ambaye tunaambiwa ni mwanasheria amekimbia taaluma yake na kujiingiza kwenye siasa kwa kupitia mgongo wa baba yake? Je yeye ni mbunge kanjanja? Ridhiwani asitegemee kusifia au kupendelewa. Chama chajiuza na kibaya chajitembeza.”
Jingine liliongeza, “ Inasikitisha sana kuona kuwa Ridhiwani haoni madudu ya serikali ya baba yake iliyoahidi watanzania maisha bora kwa wote yakaishia kuwa kitendawili huku wote wakigeuka marafiki na ukoo wake bila kusahau hata waramba viatu wake ambao mwanae anawaona ni waandishi mahiri kwa vile wanaweza kusifia kila analofanya baba yake hata kama ni la hovyo.”
Jingine lilisema, “ Hivi Ridhiwani anataka tumsifie baba yake kwa kusafiri sana au kutokaa ofisini ukiachia mbali matumizi mabaya ya fedha za umma, kufuga ufisadi, kufanya mambo kishikaji, kuruhusu familia yake watumie ofisi yake kujineemesha kama alivyoukwaa ubunge Ridhiwani, kulinda wauza unga, majangili, mafisadi, walioghushi na wahalifu wengine? No way. Ridhiwani aambiwe ukweli amechemsha na kama ni ukanjanja basi yeye nambari wani.”
Kwa vile mimi ni shabiki wako kufa, baada ya kuona upuuzi umezidi, niliamua kuwatia watu mikono kiasi cha kuokolewa na polisi. Vinginevyo kungekuwa na marehemu tokana na sakata hili la kukukosoa wakati hupaswi kukosolewa. Wao ni nani hadi wamkosoe mtoto wa mfalme ambaye pia ni mfalme mtoto?
Nimalizie kwa kuzidi kukupongeza kwa kuwatolea uvivu makanjanja wanaojifanya wafichuaji wa uchafu unaotendwa na wateule. Wateule huwa hawakosei na wakikosea lazima waandishi mahiri waseme hawajakosea. Badala yake wawasifu kwa kila wanachofanya.
CHANZO: Nipashe Julai 19, 2014.

5 comments:

Anonymous said...

Huyu mtoto ni Nani haswa katika watoto
Nashangaa sana kumpa kichwa na kigirii chake cha sheria tena kwa Kuwa alikuwa mtoto wa kigogo
Jeuri hii kanitoka wapi huyu mtoto ana nini haswa
Watanzania Acheni ushamba
Mbona watoto wa Nyerere Hawana ulimbukeni huu

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon una hoja. Kumbuka watoto wa Nyerere ni watoto wa Nyerere. Mara nyingi tabia za watoto huonyesha ubora au uhovyo wa malezi waliyopewa. Nyerere hakuwa kibaka wala tapeli hivyo na watoto wake wamefuata hili. Wa sasa si watoto wa rais bali rais watoto, Ndiyo ufisadi wenyewe wa kiakili na kimfumo. Tuombe Mungu atuondolee balaa hili.

Anonymous said...

Tena amekuwa msema ji sana tangu alipokuwa mbunge tena kwa kuiba kura
Nashangaa waandishi wa habari kumpa kichwa bwege hili licha ya kuwakandia waandishi wa habari
Anani huyu mtoto mdogo kisa kazeeka sura mpaka akili ja
Kalewa madaraka na mapunda aliyowebebesha sembe wako china
Naanatuma Watu kwenda china kuwajulia hali
Tu najuwa sana
Na ndo maana china bongo vyama Yao vina uhusiano
Wachina wanaoiba meno ya Tembo,thahabu.
CCM siiipendi hadi akhera

Anonymous said...

Tanzania hakuna Hamasa wa kuuwa Watu Kama hawa

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon hapo juu mmenena. Kweli madaraka hulevya tena hulevya sana. Tunangoja kumuona baada ya baba yake kufungasha virago ikulu. Nadhani huyu dogo anatumia udhaifu wa baba yake ambaye ashakum si matusi ukisema ni kichwa cha panzi.