Tuesday, 17 May 2016

Kijiwe: Walioficha njuluku ughaibuni wanyongwe


        Japo si kawaida yake kuanzisha mada, leo Mchunguliaji kaamua kuvunja mwiko. Ameinigia akiwa amenunua gazeti lake mwenyewe. Kila mmoja anashangaa kunani leo. Baada ya kuamkua, anabwaga gazeti mezani na kusema, “Wazee mnaona tunavyoliwa twajiona kama mataahira?”
            “Mnaliwa wewe na nani, vipi na nani anayewala na anawala vipi na kwanini awafanyie hivyo usawa huu?” Mbwamwitu anauliza kama kawa kwa utani wake.
            Mchunguliaji anaonekana yuko serious. Anajibu, “Tunaliwa sisi sote wadanganyika na wale tuliowaamini ofisi zetu.” Anamgeukia Mbwamwitu na kuendelea, “Kwanza soma gazeti kaka usidhani natania au nataka kutukana.”
            Kabla ya kuendelea Mgosi Machungi aliyekuwa ameishaanza kufura anakula mic, “Sasa timekueewa. Sema tinaibiwa siyo kuiwa. Maana kuiwa tusi tena kubwa tu. Hakuna anayemla mwenzie hapa bai kuibiana. Kama ni kuiwa basi sisi ndiyo tinapaswa kuwaa hao wanaotiibia.”
            Msomi Mkatatamaa anaona kuwa hali yaweza kuwa tete. Anaamua kutia guu, “Kimsingi, mnachogombea ni kitu kidogo. Kuibiwa na kuliwa vyaweza kuwa sawa. Kwani anayekuibia anakula jasho lako. Hivyo, anakula wewe japo si kwa maana mnayodhamiria wengine hapa. Basi kuepuka utata tuseme wanaotuua au kutuibia.”
            Kapende anakula mic, “Nakubaliana nawe Msomi. Nadhani hapa si kupoteza muda kwenye lugha au maneno ya kutumia. Tunapaswa kujadili ujambazi huu ambao nami nshausoma na kuudhiwa nao kiasi cha kutamani kula nyama ya gendaeka na kushushia na damu yake.”
            “Kwa nanna hii wanioliwa ni wale waniotuibia yakhe. Basi tuseme wanioliwa siyo sisi tunioibiwa bali hawa waniotuibia wakaficha ughaibuni wakaishia kuliwa na mabenki ya ughaibuni tokana na kujua ujuha wao. Huoni yanivyoanza kuwachoma?”
            Mbwamwitu anauliza, “Eti yanawachoma!  Hii kali kumbe wanachomwa japo wakiwa hapa wanajifanya wajanja siyo wakati wachomwa siyo?”
            Mipawa amchomekea Mbwamwitu, “Heri wachomwe hapa hapa duniani. Je wanasababisha vifo vya wachovu wangapi? Hawa nao  ni majipu wazi kwa Dokta Kanywaji Kutumbua. Tunangoja kusikia tamko lake juu yao.”
            Da Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kutia guu, “Siamini kama huko wanachomwa. Heri tuwachome moto wenyewe badala ya kuhangaika na vibaka waliotengenezwa na hawa majambazi wakubwa. Tena ukiona orodha yao huwezi hata kuamini. Ama kweli alijisemea babu yao mzee Ruxa kuwa kaya hii ni kichwa alichokigeuza cha mwendawazimu walevi kujifunzia kunyoa!”
 “Sijui naye amekwapua na kuficha kiasi gani kwenye usawa huu ambapo kila mkubwa  na mchukuaji anajitahidi kuhomola na kuficha ughaibuni. Maana wachukuaji wengi hapa kayani ni magabacholi tena tangu enzi za mzee Mchonga. Sijui hapa kama Riz na dingi wake watapona.” Anachomekea Mijjinga.
            Mgosi anamgeukia Kanji na kusema, “Naona wengi waioficha njuuku ughaibuni ni magabachoi. Hebu tiezee tieewe. Kanji umeficha kiasi gani na wapi? Maana naona magabachoi wanatia foa kwei kwei kwenye uhujumu uchumi na ujambazi huu. Hapa azima tinyonge kenge na ngedere hawa wasio na haya waa huuma kwa umma wa wachovu.”
            Kanji ambaye hakuwa akitegemea swali hili anaonyesha kustuka. Anaamua kujitetea, “Kwani ni hindi pekee naficha jukuku ghaibuni? Mbona iko hata Swahili tena yenye weo kubakuba  na zungu mingi dugu yangu? Veve onea mimi bure. Iko sikini kama veve dugu yangu. Hapana jua kuwa hindi tajir hapa kunywa gahawa hapa dugu yangu? Hindi tajiri hapana panga jumbani ya Swahili kama mimi. Yeye iko panga jumba ya sajili bana.”
            “Yakhe Kanji hapa wallahi wankata! Yashangaza sana kuona  kuona baadhi ya walotuhumiwa na kuthibitika wameficha njuluku ghaibu bado wako mjengoni tena wakipewa nyadhifa za juu tu kana kwamba ni watu. Wakamatwe na kunyongwa mbwa hawa ili liwe somo kwa majambazi wengine kama wao,” anajibu Mpemba huku akisogeza karibu kikombe chake.
            Msomi aliyekuwa akidurusu gazeti vizuri anaamua kurejea, “Nadhani tungemuuliza mzee Mpayukaji tuliyemtuma Panama atupe majina zaidi ili kijiwe kikae na kuyapitia na ushahidi wake halafu tuanze kumbana mbavu Dk Kanywaji awachukulie hatua husika hawa majambazi wa wazi. Bila kuwakamata na ikiwezekana–kama umma wa waathirika utataka wanyongwe–atapoteza imani ya umma bila sababu. Hapa lazima aende mbele. Apitie na kurekebisha mikataba ya uwekezaji ambayo kimsingi ndicho chanzo kizuri cha fedha hii inayofichwa ughaibuni. Pia azidi kukaza Kamba kwenye ukusanyaji kodi na kupiga marufuku misamaha ya kodi wakati akitafuta namna ya kuongea na mamlaka husika ughaibuni kurejesha njuluku yetu.”
            Anakohoa na kuendelea, “Sina shaka hata kabla ya kusikiliza taarifa za Dokta Mpayukaji, hawa walioruhusu jinai hii kwa kushindwa kumilki madaraka yao nao watakuwa na njuluku ughaibuni. Ushahidi wa kimazingira unasema hivyo. Kwani walifanya hivyo kama biashara iliyowaingizia kipato kwa kuuibia na kuuhujumu umma. Hapa lazima hata wale wezi wa Kiwila, UDA na madudu mengine wachunguzwe kwa jicho kali na umakini.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la gabacholi Josefuali Manjii! Acha tulitoe mkuku ili tumtoe na kumfanyia kitu mbaya. Bahati yake dereva wake aliamua kututimlia vumbi vinginevyo sasa angekuwa anauguza maumivu baada ya kumuangukia kipopo kama siyo kumfanyia kitu mbaya.
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: