Friday, 27 May 2016

Mlevi kusafirisha bangi na mirungi kwa ndege


            Zamani nikisikia ule mpasho wa viumbe wazito ni kama ulikuwa unapiga chenga. Nilidhani ni mipasho ya akina mama nisijue kuwa baadaye mpasho huu utakuwa na mantiki kwa kaya yetu. Mwanzoni nilidhani viumbe wazito ni majini au mashangingi nisijue siyo. Juzi kwa– mara ya kwanza na kwa macho yangu tena bila kulewa wala kuvuta–niliwaona viumbe wazito pale uwanja wa Ndege wa Mzee Mchonga walipoumbuliwa na rais Dokta Joni Kanywaji Mkufuli.
            Ama kweli duniani kuna viumbe wachokozi wanaopaswa kuchokonolewa kujua wanajiamini nini. Tabia mojawapo ya viumbe wazito ni kutobadilika. Wamezoea kufanya mambo ya hovyo na hovyo hovyo na kwao ndivyo ilivyo hata kama mambo yenyewe wanafanya ndivyo sivyo. Wamezoea kiasi cha kuwa vigumu kubadilika bila kutumbuliwa. Pamoja na ujanja na kiburi changu, sikuamini kuwa kuna watu na akili zao wangefikiria–achilia mbali kutenda–kumdanganya dokta Kanywaji. Mnamdanganya dokta Kanywaji tena mbele ya kamera bila hata chembe ya aibu! Yaani mnamwambia kuwa mimashini ya kufichulia mabomu inafanya kazi wakati ilijifia miaka kumi iliyopita! Hakuna kilichoniacha hoi kama ukweli kufichuka baada ya kimbembe pale Dokta Kanywaji alipotaka mashine ziwashe na zikawashwa na kuonyesha zisivyofanya kazi. Kana kwamba haitoshi, alipouliza ziliharibika lini alipata majibu matatu ambayo ni majipu si majibu kitu. Kwani muongo wa kwanza alimwambia kuwa mashine zilikuwa zimeharibika zaidi ya mwaka mmoja. Muongo wa pili alimwambia kuwa ilikuwa imeharibika kama miezi minne iliyopita huku muongo wa mwisho akimwambia kuwa ilikuwa na wiki moja tu tangu iharibike. Hadi dokta Kanywaji anaondoka hakujua mashine zilikuwa zimeharibika lini na kwanini zaidi ya kuharibiwa au tuseme kuhujumiwa.
            Hawa wanaizaya wana bahati. Sijui kwanini hajawatumbua pale pale kavu kavu kama alivyowafanyia akina Kimlango! Wana bahati ya mtende. Ingekuwa zama zangu ningeita ndata na kuhakikisha wanafungwa pingu na kwenda kunonihino kwenye debe. Mijitu mizima inaongopa tena bila hata ya kupepesa macho! Baya zaidi inamudanganya mkuu wa kaya kana kwamba ni kidhabi yule yule viliyezoea akipita pale kwenda kuzurura na kuwapungia mikono akikenua huku kaya ikiliwa!
             Kwanza, nilinusa harufu ya ukabila pale. Karibu majina yote ya akina Rweyungayunga na Rweshomashoma. Kwanini majina ya wanene wa vitengo ile yawa ya akina nshomile tu kama hakuna namna? Japo mzee Mchonga alijenga kaya isiyo na ukabila–kama ufisadi,na uhalifu mwingine kayani vinavyoongezeka–ukabila nao unaonekana kurejea kwa mlango wa nyuma. Hili nalo ni jipu na nadhani ndiyo chanzo kizuri cha watumishi hewa, utegaji, uzembe na ushenzi mwingine vilivyokuwa vimetamalaki kwenye asasi za umma. Kuna haja ya Dokta Kanywaji kuanza kufuatilia ukabila kwenye asasi za umma.
            Kwa vile nimegundua kuwa uwanja ule ni mtupu, basi nitaanza dili la kusambaza mihadarati na hata nyara za taifa kabla hawajastuka na kuchukua hatua.Nitakuwa nachukua mirungi yangu toka pale Meru kwa akina Mvaithe na kupitisha Sirari; baada ya kutoka pale Ulenchoka na kujaza mifuko ya Bange then nadandia pipa Musoma na kupitia uwanja wa ndege wa Mchonga bila kukaguliwa. Maana niliona mwenyewe mimashine ilivyohujumiwa kama alijisahau mmoja wa waliomdanganya Dokta Kanywaji alivyosema.
            Ili kutengeneza njuluku haraka, lazima nitakuwa nakwenda zangu Maswa na Serengeti kuwinda chui, tembo, faru na kila kinachopita mbele yangu na kusafirisha kuja kuuza Masaki kwa wachina na kutengeneza mshiko kama sina akili. Sina haja ya kujiingiza kwenye biashara uchwara ya kuficha sukari wala mafuta ya kula au bidhaa.
            Pia nitafanya utafiti kujua kama uwanja wa ndege wa KIA una upenyo wa kusafirisha wanyama na bange nje.  Kama uliweza kusafirisha wanyama hai kama twiga tembo na madude mengine makubwa utashindwa kago yangu siyo? Sijui wale waliosafirisha wanyama wetu umangani nao wameishia wapi maana sisikii wakitumbuliwa? Kama magabacholi wanapitisha tanzanite kila uchao, kwanini nami nisipitishe madude yangu au wataniminyia kwa vile mimi si gabacholi?
            Kwa sababu kaya iko uchi tena ni shamba la bibi na kichwa cha mwendawazimu, lazima nichange njuluku haraka haraka na kuwa mmojawapo wa mabilionea vijana toka kaya hii. Hapa bila shaka wahariri wa jarida la mabilionea la Forbes wanisake kama sukari usawa huu. Pia nitachunguza kama waziri wa usafirishaji anautwanga mma kama kitwanga ili niunde kampuni ya Lingumi kuweka vifaa vya kukagulia mizigo viwanja vya ndege ima nilete vibovu au niwaache Solemba kwa kujenge mijumba ya bei mbaya na kununua ndinga za bei mbaya huku nikizungushia mabausa kibao kuonyesha ufalme wangu.
            Kitu kingine, nafanya utafiti kujua kama Dokta Kanywaji ana kitegemezi chake ambacho naweza kukitumia kupata tenda.
            Kwa vile nataka nitegeneze njuluku kiasi cha kulala maskini na kuamka bilionea, leo sitachonga sana. Nawahi kwenda zangu Kenya kuchukua mirungi na Musoma kuchukua bangi tayari kuanza kufanya majaribio ya utafiti wangu kabla hawajastuka. Hivyo, walevi jiandaeni kupigwa ofa za ulabu za kufa mtu. Niombeeni dua nifanikishe kuvusha madudu yangu ili tusherehekee na kuselebuka kwa njuluku zitokanazo na kaya ya walevi.
Chanzo: Tanzania Daima. 

No comments: