The Chant of Savant

Sunday 2 April 2017

BASATA na Polisi acheni kujikomba

            Baada ya rais John Pombe Magufuli kutengua marufuku ya wimbo wa Wapo waEmanuel Elibariki aka Ney wa Mitego na kukamatwa kwake, tokana na katazo la Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na kukamatwa na jeshi la Polisi, tunaweza kusema kuwa sasa wanaojikomba na kujifanya wanajua hisia za rais wamekwama. Yaani mnakamata mtu bila kumpa onyo au haki ya kujitetea bado mnaona mnatenda haki kweli?
             Kwanza, ni aibu kwa taasisi zinazoendeshwa kwa fedha za umma kama Basata na Polisi kujikomba. Huu ni ushahidi kuwa taasisi hizi ima hazijui kazi zake zaidi ya kujigeuza vikaragosi vya kueneza woga na ujinga nchini au zinafanya kazi kwa woga usio na msingi ukiachia mbali kutaka kuwafurahisha wakubwa hata kama ni kwa kuwaumiza watu wasio na hatia.
            Pili, wapo waliopongeza hatua ya rais na kulaani hatua za Basata na Polisi. Kimsingi, hapa hakuna cha kupongeza hasa ikizingatiwa kuwa rais ndiye aliyeachia mambo haya kiasi cha kuyajengea mazingira hadi kujenga dhana nyingine kuwa nchi yetu inaendeshwa kwa woga na kupinda sheria hasa wanapoguswa wasiopaswa kuguswa au watu walio karibu na rais au hata kumgusa rais mwenyewe tokana  na mambo wanayotenda dhahiri.
            Tatu, sioni sababu ya kumpongeza rais kwa alichofanya hasa ikizingatiwa kuwa amejitahidi kukwepa aibu kwake na serikali yake ukiachia mbali kushtakiwa. Kama atajifunza tokana na kadhia hii litakuwa jambo la maana kwake na kwa taifa kwa ujumla. Haipendezi rais kuwa anaingilia kila jambo.  Kwanini rais hakuwaamuru Basata na jeshi la polisi au waziri anayehusika kutenguamarufuku ya wimbo wa Mitego na kushikiliwa kwake kinyume cha sheria? Sitaki rais wetu ageuzwe rahisi na wale wanasukumwa na woga na kujikomba kiasi cha kushindwa kusimamia sheria na haki. Nadhani baada ya rais kutengua uwaziri wa Nape Nnauye baada ya kuunda tume ya kuchunguza kashfa ya kuvamiwa kwa vituo vya Clouds, wanywanywa na woga walidhani hii ndiyo sera yake, kulindana, kutishana na kuumizana bila sababu.
            Nne, hata hivyo rais alitumia busura kuepuka serikali yake kuadhiriwa mahakamani. Hivyo, basi tokana na alichofanya rais,  Mitego ashitaki serikali kutaka afidiwe kwa mateso na athari alizozipata yeye binafsi na kazi yake ili liwe somo kwa wote wanaotumia madaraka vibaya kwa sababu za kulindana na masuala binafsi.
            Baada ya kusema haya, acha nimshauri rais Magufuli kuwa na subira linapotokea jambo japo si yote yanayotaka subira. Mfano, anapogundua kuna madudu yanayosababisha hasara kwa taifa, lazima achukue hatua za tahadhali mapema. Inapokuja kwenye masuala kama ukosoaji, rais anapaswa kuacha vyombo husika vitimize wajibu wake au kuingilia kwa kuwatumia wasaidizi wake badala ya kujiingiza kwenye mambo yasiyo ya hadhi yake kama kwenye kadhia hii ya Mitego ambaye bila shaka sasa anachekelea kuwa rais amemsaidia kuwa maarufu na kuonekana shujaa bila ulazima kama rais angekuwa anaacha walio chini yake waache kufanya kazi na maamuzi kwa woga.
            Sita, tunashauri wakuu wa vyombo husika waliotoa amri hizi za kijinga watajwe hadharani na kuwajibishwa mara moja ili liwe somo kwa wengine wenye kuendeshwa na woga na kujikomba kufanya maamuzi yao.
            Saba, kwa kuamuru wimbo wa Mitego uendelee kuchezwa, ni dalili kuwa sasa rais anaanza kuona madhara ya Bashite kwa utawala wake. Haiwezekani mtu mmoja tena asiyependa kujitetea wala kutoa ufafanuzi kuhusiana na tuhuma dhidi yake aliweke taifa rehani. Bashite ni nani katika Tanzania? Kwanini watendaji wetu wanakuwa wepesi kuwaadhibu watu wema wakati wakiwakingia kifua waovu? Hili halikubaliki tanzania. Kama ambavyo rais amekuwa akionya watanzania kuepuka kujenga mazingira yanayovunja amani nchini kwa kutolea mfano wa kilichotokea Rwanda mwaka 1994, vivyo hivyo, naye aepuke kupalilia hayo mazingira kwa kuwatendea watanzania kibaguzi na kiupendeleo kama ilivyo kwenye sakati la Bashite.
            Nane, uzoefu unaonyesha kuwa rais Magufuli hana mtu wa kudumu. Rejea alivyombadilisha Katibu Mkuu kiongozi, Ombeni Sefue hata baada ya kuwa amemhakikishia kuendelea kuchapa kazi lakini akamuondoa. Hata Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam ambaye yuko katikati ya kadhia hii anapaswa kuchukua tahadhali kuwa hakuna aliyeshindana na umma akaushinda. Angekuwa mkomavu kisiasa, angeachia ngazi kwa hiari yake ili lau umma umsamehe kama kweli alighushi hivyo vyeti na kuvamia Clouds.
            Tumalizie kwa kuwapongeza wote waliosimama kidete na kulaani ujinga uliokuwa umetendeka ambao ulionyesha wazi kuminywa kwa haki za kikatiba za watanzania za kutoa mawazo bila pingamizi wala kutishwa ilmradi wasivunje sheria. Hongera Ney wa Mitego kwa kutengua kitendawili cha Bashite ambacho kilianza kuwa donda ndugu na jipu kubwa tu lenye kumngoja rais alitumbue mara moja. Turudie, tanzania ni zaidi ya rais, Bashite na yeyote yule anayedhani ana haki ya kuwa juu ya wengine. Ni nchi ya kidemokrasia inayopaswa kuongozwa na sheria, kanuni na katiba chini ya matakwa na shuruti zote za utawala bora na wa sheria.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

5 comments:

Anonymous said...

Salaam Mwalimu Mhango,
Kuna baadhi ya viongozi katika bara letu la Afrika wanachoigania wao mara nyingi ni kubaki madarakani kwa njia yoyote ile katika nchi ambazo kuna mfumo wa demokrasia ambao haukujengewa kufuata katiba,kanuni na sheria ili kufikia utawala bora.Kwa maana kwamba wanatawala katika mfumo wa demokrasia ya rangi ya mdomo(lips stick) au "window show". Na kwa mfumo wa demokrasia ya lips stick au window show marais hawa daima hawaoni tabu kuipindisha katiba,kuvunja kanunu na sheria na kukosekana kupatikana mfumo wa demokrasia ya kweli na mwisho wa siku utawakuta marais hao baada ya kuwa wamekuja madarakani kwa kupitia masanduku ya kura ambayo wanayo yachakachua daima hatimae wanakuwa sio marais ambao waliochaguliwa na watu wao na wanageuka na kuwa na sifa zote za udikiteta,akina Museveni,Mugabe,Yahya Jammeh na Campore ni mfano hai.Na kwa madikiteta hawa ili wabaki madarakani wanatumia mbini zote chafu za kuwatia hofu,uwoga na "utakiona cha mtema makuni" au "kilichomtoa Kanga manyoya" pale tu panapokuwa na sauti za haki za upinzani dhidi yao. Na ili wafanikiwe kubaki madarakani huwa wanajenga tabaka la waramba vitu vyao,tabaka la "ndio Bwana"na kuvitumia vyombo vya usalama wa dola kuhakikisha kwamba wanabaki madarakani kwa muda mrefu iwezekanavyo,na kwa viongozi hawa wanakuwa hawajali kwamba wananchi wao waliwapenda,waliwachukia au waliwabeza muda wa kudumu kuna baadhi yao huwa wanadai kwamba muda wa kudumu wanaendeleza nchi zao kimaendeleo hakuna sababu yoyote ya wananchi kutaka viongozi hao waondoke madarakani muda wao ukifika kwa kupitia njia ya sanduku la kura.

Kuna baadhi ya viongozi wa kiafrika wao wanakuja madarakani wakiwa wanajua kwamba mwisho wa siku muda wao utakwisha na kuondoka madarakani.Viongozi hawa mara nyingi wanakuja na utamaduni wa kupigania umashuhuri rahisi(cheap populaty)kwa kutaka kupendwa na wananchi wao na wakati huo huo wakiwa wanafanya madudu yote ya kuididimiza nchi,ufisadi,kujilimbikizia mali wao na familia zao na jeshi la waramba viatu vyao bila kujali kwamba nchi itadidimia kwa kiwango gani.Katika nchi yetu baada ya kuondoka kwa Mwalimu Nyerere madarakani amekuja Mwinyi na "cheap popuraty"ya mzee wa rukhsa na udini hatimae akawa ni rais anaependwa na wananchi na waumini wa dini ya kiisilamu na kwa wananchi ambao mwamko wao wa kisiasa ni mdogo waliangalia masilahi yao binafsi na kufumbia macho madudu yote ya Mwinyi ya kuingamiza nchi,baada ya Mwinyi kuondoka madarakani amekuja Mkapa mzee wa ubinafisaji wa kile sekta ya serikali kwa kutafuta "cheap populaty"kwa wafanya biashara wakubwa na mabepari wa nchi za nje na wananchi wakafumbia macho madudu yake yote ya kuingamiza nchi,akaja Kikwete aliepigania cheap popularity ya kwamba anetataka kujitajirisha kwa haraka mno na ajitajirishe tu kwa njia zozote zile ambazo anazozijua na kuzielewa na matokeo yake ukafumuka mfumuko wa ajabu wa ufisadi ambao haujawi kutokea katika nchi yetu,ukiongezea yeye mwenyewe kuyatumia madraka yake vibaya kwa masilahi yake binafsi,familia yake na utitiri wa kundi la waramba viatu vyake.Na wananchi kufumbia macho madudu yake yote ya kuididimiza nchi.Amekuja Magufuli na cheap popularity ya kwamba ni rais wa wanyonge na baada ya kukubalika na wananchi kwa muda mfupi wa mwaka mmoja tangu aingie madarakani kwamba anastahiki sifa hiyo ya rais wa wanyonge,amekuwa ni rais wa kuingilia kila dogo na kubwa ambalo alistahiki yeye kuliingilia au hata kuliongelea na hatimae viongozi wa serikali yake na taasisi zote za kiserikali kuwa ni kivuli chake au kuwa kama ni wanasesere wake.Na hatimae kuumba tabaka la viongozi ambao waliojawa woga na hofu ya utekelezaji wa majukumu yao katika madaraka yao na tunaona wengi wa viongozi hao WAKIJIKOMBA,KUJIPENDEKEZA NA KUWA "NDIO BWANA ili wabaki katika vyeo vyao kwani wanajua wazi tu kwamba wakimchezea simba sharubu yatawatokea nyenye kuwatokea matokeo yake wanafanya kazi kwa matamanio ya kupendwa na rais wao na wala si kutekeleza wajibu wao kama inavyostahiki.

Inaendelea...............

Anonymous said...

Mwalimu Mhango,umeyafikisha kama kawaida yako mahadharisho,makemeo,busara na hekima kwa rais wet ni juu yake kuyafanyia kazi.Kwa hiyo wache nami nimalizie kwa kusema kwamba kwa utaratibu huu au utamaduni huu wa kutafuta "cheap populaty"kwa wananchi kwa viongozi wa aina hii na katika nchi kama ya kwetu ambapo wananchi hawana haki ya kumuuliza rais wao(accoutability),wananchi ambao hawana katiba yao ya nguvu,na serikali ambayo upindisha katiba,kutofuatwa kanuni na sheria kama ipaswavyo,tutawapata tu viongozi ambao kwa kulinda masilahi yao ya kubaki katika madaraka yao kuendelea kujikomba nakujipendekeza kwa rais huyu na hatimae kutofuata sheria,kanuni za utawala bora.Naam tunajua rais wetu ni mchapa kazi na ana nia njema na nchi yetu na wananchi lakini nia njema peke yeke haitoshi,na afanye kazi yake kutokana na ilani yake ya chama chake kwa kuwatekelezea wananchi na nchi kile kilichopo katika ilani hiyo bila ya kutafuta "cheap popularity"ya kutaka kusifiwa kwamba ni rais wa wanyonge na kusababisha madudu na mazonge ambayo hayahitajiki.Kama alivyosema Mwalimu Nyerere kwamba Ikuli ni mahala patakatifu na urais nao una heshima yake na hadhi yake na sio tu kujiingiza katika kila dogo au kubwa ambayo viongozi wako wa chini wanaweza kuyatekeleza bila ya woga au hofu au kukuridhisha wewe.Hii itatusababishia kuwa na viongozi ambao ni wanafiki,waoga na wasiojiamini.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon.
Nashukuru kwa mchango na dhana nzima ya ubinafsi wa shilingi mbili au cheap popularity ukiachia mbali ile ya lipstick na window dressing. Ninachokubaliana nawe ni kamba hata umpake lipstick kiasi gani nguruwe anabaki kuwa nguruwe. Nadhani Magufuli ameishiwa mapema hata kabla ya miaka miwili. Na hakuna kitu kitakachomuumbua na kumuumiza kama kung'ang'ania mtuhumiwa wa uhalifu wa kughushi vyeti kama Makonda. Kuna siku mtakuja kusema kuwa nilisema. Mfano, kwa sasa hata mapambano dhidi ya mihadarati yametoweka na nafasi yake imechukuliwa na kumlinda Makonda kiasi cha kujenga shaka ya ajabu. Angekuwa mkewe ungesema lau anamlinda mkewe. Kadhalilka angekuwa mwanae lau ungesema damu ni nzito kuliko maji. Ni aibu kiasi cha kuzua hisia nyingi za ajabu kuhusiana na wawili hawa.

Anonymous said...

Mwalimu Muhango,tumeyaona madhara ya "cheap popuraty juzi bungeni wakati wabunge wetu wawakilishi wa wananchi wakimpigia makofi na hata kumsimamia kisimamo cha heshima"standing of ovation" kwa Kikwete Bungeni!!Ni jambo la kushangaza,aibu,fedhea na la kukatisha tamaa kisiasa kwa nchi yetu na wanasiasa wetu.Je ni kweli kwamba wabunge hawa-sina uhakika kama wabunge wa upinzani walishiriki kwa hili-waliompigia makofi na kumshangilia Kikwete ni wasahalivu kiasi hiki au vipofu kwa kiasi kikubwa kwa madudu yote ambayp Kikwete aliyoyafanya dhidi ya nchi na wananchi wake?Je wabunge hawa wamekubali kuramba na kula matapishi yao wakati walipokuwa wakimkosoa Kikwete alipokuwa madarakani?Ikiwa wabunge wetu ndio wanasiasa wetu na wasomi wetu ndani ya nchi iweje wafikie kutokua wamekomaa kisiasa na kisomi?Nakumbuka vyema Mwalimu Mhango kwamba katika miaka kumi ya utawala wa Kikwete umekuwa mwenye kupayuka kwa nguvu zako zote dhidi ya utawala wa wake lakini leo hii kikwete amegeuka na kuwa ni "super star"wa kisiasa kwa sababu ya kujijengea "cheap popuraty"?Hii inaonyesha wazi kwamba wabunge hawa kwa kumshangilia kikwete na kumsimamia kisimamo cha hashima"standing of ovation" ni kuspoti madudu yote na ufisadi wote wa kikwete.Ikiwa wabunge wetu huo ndio upeo wao wa kisiasa na upeo wao wa kufikiri hivi nchi yetu itaendeshwa kwa siasa za ubinafsi,uroho,ushabiki na unazi?Je tunatoa picha gani kwa dunia iwapo taifa letu linaongozwa na wanasiasa wa aina hii?Siasa za ubinafsi,uroho,ushabiki na unazi hautotupeleka wal kutikisha popote pale.Na kwa wabunge hawa kwa kumpa sapoti yao yote Kikwete hawaoni kwamba ni kumsaliti kiongozi wao wa chama chao kiongozi ambae kwa muda mfupi sana ameleta maendeleo ya nchi na wananchi maendeleo ambayo hayajawahi kufanywa na viongozi wote wakiopita baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka madrakani?Mwalimu Mhango maswali ni mengi tu kuliko majibu nimalizie tu kwa kusema SHAME,SHAME,SHAME ON YOU FOR ALL THOSE MPS WHO SUPPORTED CORRUPT KIKWETE.Kuhusu Magufuli na Bashite ni mwiba wa mchongoma katika unyayo wa rais wetu kiasi ambacho mpaka wengine wamefikia dhana mbaya dhidi ya wawili hawa iwapo sio mkewe au mwanawe au mtoto wa member wa familia yake iweje amkingie kifua kiasi hiki kuna nini hapa katika mahusiano ya wawili hawa mpaka Magufuli achafue moja wa ukurasa wake wa kisiasa?Na tuuachie wakati utujibie swali hili la utata.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ndugu Anon.,
Kwanza nakubaliana nawe kuwa waliomshangilia Kikwete ima ni wasahaulifu, wanafiki au wapuuzi wa kawaida hasa ikizingatiwa kuwa kilichowasukuma kufanya hivyo siyo vichwa vyao bali matumbo yao. Hivyo, huna haja ya kushangaa hasa ikizingatiwa kuwa kichwa kinapoacha kufanya kazi na kuacha kazi hiyo kwa tumbo lolote lawezekana. Hizo ndizo siasa za CCM na Tanzania. Mfano mdogo ni kwanini watanzania wamemuachia Magufuli madaraka a kufanya atakavyo hata kwenye mambo wasiyoyaunga mkono kama kashfa ya Bashite? Huu ni ushahidi kuwa wenzetu walisukumwa na njaa na si heshima wala nini ukiachia mbali ngoa dhidi ya Magufuli kwa kutibua ulaji wao kuanzia chamani hadi serikalini. Laiti Magufuli asingejitwisha zigo la mavi la Bashite, angeng'aa kama nyota.