Friday, 8 October 2010

Je haya si matumizi mabaya ya madaraka?


Hakuna kitu kibaya kinachoweza kukubalika hata kama umma utalazimishwa 'kukikubali'.

Hakuna siri kuwa wadhifa wa mkuu wa wilaya nchini unaanza kuwa kama kichaka cha wachovu, waramba viatu, washirika na maswahiba wa rais. Uteuzi wa mkuu mpya wa wilaya ya Masasi, Nape Nnauye, hauwezi kupita bila kuhojiwa.

Wengi hasa waandishi wa habari na wachumia tumbo wengine wa kisiasa sasa wako kwenye heka heka za kuupotosha umma ili wateuliwe wakuu wa wilaya na rais kama kulipa fadhila kwa usaliti wao. Na zingatia hili. Baada ya uchaguzi mtashangaa sana kuona hata wahuni wakiteuliwa kuwa wakuu wa wilaya.

Mtaona marafiki., mashoga wa mkewe, marafiki wa wanae na wapambe wa rais wakiteuliwa kwenye wadhifa huu. Mtaona watu wa hovyo wasiofaa hata kuwa mabalozi wa nyumba kumi wakiteuliwa kuwa wakuu wa wilaya. Ila ikumbukwe. Pamoja na rais kulipa fadhila, ajue hawa wateule wake wanalipwa kwa pesa yetu na si pesa yake binafsi. Pia watu hawa wanaotokana na kujikomba na si uchapakazi, wanazidi kutukwamisha kimaendeleo. Maana hata wakivurunda hakuna wa kuwagusa ikizingatiwa kuwa aliyewateua ni mungu mtu kikatiba. Hamjaona mkewe, mwanawe na wapambe zake wanavyofuja pesa yetu kumpigia kampeni?

Mchezo huu wa hatari ulianza pale rais Jakaya Kikwete alipomlipa fadhila mpiga debe wake mwandishi wa habari Salva Rweyemamu aliyemteua kuwa mkurugenzi wa tume ya mawasiliano ikulu.

Hata wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa mchezo huu ulikuwapo japo si sana kama sasa. Angalia baadhi ya waajiriwa wa Ikulu. Utakuwa wengine wana udugu na mke wa Mkapa. Huu ni ufisadi hata kama unatendwa na wakubwa.

Na hii si siri. Kuna mwandishi mmoja tena tapeli ambaye hata sijui kama aliusomea huo uandishi wa habari ambaye alikuwa mhariri wa gazeti moja dogo la kila wiki lenye makao yake maeneo ya Kariakoo. Huyu anatangaza wazi wazi kuwa lazima ateuliwe kuwa mkuu wa wilaya. Sababu? Anaendelea kazi ya kuwachafua wapinzani wa Kikwete kwa kuzua mambo akifanya kibarua hiki kichafu ili ateuliwe kuwa mkuu wa wilaya. Uzuri ni kwamba anajulikana alivyoghushi vyeti. Ila kwa vile watuhumiwa wa kughushi vyeti vya kitaaluma wenye uswahiba na Kikwete hawaguswi, huenda mpumbavu huyu akapewa ukuu wa wilaya.

Na hii ndiyo sababu ya kuwasikia wapiga debe wachovu waliorundikana ofisi ndogo makao makuu CCM Lumumba wakihanikiza kupigia debe CCM hata kwa hoja chafu na zilizokufa.

Hivyo msishangae kuona wengi wa waliokataliwa kwenye kura za mchujo wa kugombea ubunge kupitia CCM wakiteuliwa kuwa wakuu wa wilaya. Rejea tamko la Kikwete kuwaasa wavumilie watatafutiwa nafasi.

Inashangaza mkuu wa wilaya anapokuwa kada wa chama kinyume na katiba ambayo inataka mtumishi wa umma asiwe na upande. Hata awe mteule wa rais, anapaswa kuzingatia hili. Ndiyo maana mahakimu, majaji, polisi na watumishi wengine wa umma wanapaswa kuwa neutral.

Wakuu wengi wa wilaya hata mikoa wamekuwa wakilaumiwa kwa kukibeba chama chao hata kufikia kutisha na kunyanyasa wananchi ili kufanikisha malengo yao. Hebu ninukuu kauli ya hivi karibuni na msajili wa vyama vya siasa John Tendwa aliyoitoa hivi karibuni jijini Arusha.

Alikaririwa akisema: “Nilisema Mbeya na sasa narudia Arusha, wakuu wa mikoa na wilaya, waache tabia ya kuzunguka vijijini na kuwatisha wananchi kuwa wakiwachagua wagombea wa vyama vya upinzani hawatapata maendeleo na kuwataka wakichague CCM, hilo halikubaliki.”

inashangaza miaka zaidi ya 50 ya uhuru bado kuna watu wanawatisha wenzao bila hata serikali kuchukua hatua. Nani atachukua hatua iwapo hawa wakoloni walioteuliwa na rais ndiyo serikali yenyewe?

Huu ni ushahidi tosha kuwa wahusika licha ya kufanya uhuni ni makada wa chama. Wanafanya kazi za chama. Lakini wanalipwa na serikali toka kodi za wananchi wote wakiwamo wanachama na wasio na wa vyama vya upinzani.

Na anayewateua makada wake kufanya kazi za chama chini ya ajira ya serikali anavunja katiba hata katiba yenyewe kama ni ya kizamani na chama kimoja. Pia huyu anapingana na kanuni za utawala bora. Yeye, wateule wake na chama chake wanaliibia taifa. Hawafai kuwa madarakani hawa. Kwani hawajiamini wala kuwa na sifa ya kuongoza ndiyo maana wanateuana kwa kujuana na si sifa za uchapakazi.

Tulimsikia rais Kikwete akiwapa moyo waliong'olewa kwenye kura za mchujo kuwa atawatafutia ajira. Je kwa kuanza kuteua watu wakati wa kampeni ni motisha kwa wale waliokuwa ima wakitaka kuhama chama au kutoshilikiana nacho kupiga kampeni wafanye hivyo kwa imani kuwa watapewa ulaji wa dezo wilayani?

Kweli hapa ndipo naona mantiki ya katiba mpya ya nchi jirani ya Kenya kuondoa vyeo vya mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa. Maana vinatumiwa na watawala wabovu kuwapa ulaji na kuwajaza serikalini marafiki zao ambao pia ni wabovu. Huu ni wizi na ufujaji wa mali na fedha za umma. Hivi tukiondoa vyeo hivi tutaokoa mabilioni mangapi ambayo yatatuwezesha hata kutoa elimu bure kama wanavyosema CHADEMA?

Tuhitimishe kwa kumtaka Kikwete kuacha kutuhujumu kwa kuwafurahisha na kuwaneemesha ima wanachama wake au marafiki zake.

Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 5, 2010.

No comments: