Sunday, 3 October 2010

Tishio la jeshi linadhalilisha taifa na jeshi

Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo akitoa vitisho mbele ya waandishi wa habari
Tamko au tuseme kitisho kilichotolewa hivi karibuni na mnadhimu mkuu wa majeshi ya Tanzania Luteni Jenerali Adbulrahman Shimbo, licha ya kulidhalilisha taifa na jeshi ni ushahidi kuwa nchi yetu iko hatarini-haina jeshi bali waganga njaa wanaojikomba kwa Chama Cha Mapinduzi ili wafaidi makombo ya ufisadi.

Jeshi liache siasa kwa wanasiasa. Lifanye kazi ya ulinzi badala ile ya kufua nguo chafu za CCM. Ni aibu na hatari.
Inashangaza. Wananchi wamegwaya kiasi cha kushindwa hata kuandamana na kulaani uimla huu! Muhimu ni jeshi na CCM kutambua kuwa atakayemwaga damu ataishia kunyea debe kule The Hague kama Charles Taylor. Mambo yamebadilika siyo kama zamani ambapo jeshi lilijiona kuwa juu ya kila kitu na kufaidi bajeti kubwa za siri zilizoishia kufaidiwa na mafisadi wa kijeshi.

Hivyo wananchi wapuuzie vitisho vya jeshi na kusimama kidete kuhakikisha kura zao haziibiwi. Maana tishio la jeshi ni ushahidi wa kushindwa kwa Kikwete ambaye bila kubebwa na jeshi, tume ya uchaguzi, polisi na wezi wengine wa kura hawezi kushinda. Atashinda kwa lipi iwapo ameiuza nchi badala ya kuitawala?

Inashangaza jeshi kujichafua kwa kuridhia wizi wa kura na likawa tayari kuubariki, kuulinda na kuulazimisha kwenye mioyo ya watanzania. Hii ni kashfa sawa na EPA hata Richmond. Je kazi yake ni kuwatumikia wananchi na si wananchi kulitumikia jeshi. Licha ya kuwapo kwa utashi wetu, lipo kutulinda na mali zetu zikiwemo kura.

Je kwanini jeshi letu limefikia hapa? JWTZ yaani Jeshi la Wananchi wa Tanzania sasa ni jeshi la watawala uchwara na mafisadi.

Kwanini wanafanya hivyo? Je wamezuzuliwa na vyeo vya kukatiwa vya wakuu wa wilaya na mikoa?
Kwa njaa yake limejivua heshima ya kuwa jeshi la wananchi na kuwa Kamanyola lile jeshi habithi la Zaire lililowalinda wezi wakiongozwa na jambazi Mobutu Seseseko.

Limeikataa heshima iliyoyandisha majeshi ya Kenya, Malawi, Zambia na Benin yalipokubali mageuzi ya kweli ya kidemokrasia yachukue nafasi hata kukataa shinikizo la wachovu waliokuwa madarakani.

Letu limegeuka mbeleko ya kuubeba mzigo uitwao CCM uliojaa mafisadi. Hivi jeshi halina common sense kujua kuwa kuvunjika kwa amani hakusababishwi na wapinzani bali ukosefu wa haki?

Hebu malizia makala hii kwa kujikumbusha makufuru ya Shimbo mwanajeshi-mwanasiasa na kada wa CCM.

Alikaririwa akisema, tena baada ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari ili kuwatisha watanzania kama ifuatavyo: “Dalili zimeanza kuonekana za kutaka kuvunja sheria katika kampeni, kuchochea fujo na uvunjifu wa amani… dalili hizo sio nzuri. Pia kuna baadhi ya taasisi na mashirika yameanza kujiingiza kwenye kampeni kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu upigaji kura au kutoa matamko yanayolenga kushabikia vyama vya siasa na wagombea.”

Kumbe kuwapa wananchi elimu ya uraia ili wachague vizuri ni dalili ya kuvunjika amani! Je amani kwa Jeshi ni pale kundi la mafisadi wenye madaraka wanapokula bila kubughudhiwa huku nalo likiwalinda? Kwanini halijawahi kutishia mafisadi kuwa watavuruga na kuondoa amani? Je ni kwa vile wengi wa wakubwa zake ni mafisadi?

Hebu angalia upuuzi huu wa Shimbo: “Napenda kulisisitiza hili, vyombo vya ulinzi na usalama havifungamani na upande wowote katika siasa. Kuvihusisha huko ni kutuchokoza, msituchochee wala kutuchokoza tuko kwa ajili ya kuwalinda,”

JWTZ inafungamana CCM na ushahidi ni hiki kitisho cha hivi karibuni. JWTZ imejigeuza mbwa ajikombaye kwa anayemfuga kwa malipo ya makanyagio (ukuu wa wilaya na mikoa) na upuuzi mwingine. Hili haliwezi kuwa jeshi alilolisuka mwalimu Julius Nyerere baada ya lile la kikoloni la KAR kuasi usiku wa jumamosi kuamikia jumapili 18-19 Januari 1964.

Kwa ufupi ni kwamba jeshi letu limetudhalilisha na kujidhalilisha na linapaswa kusukwa upya. Jeshi gani linalobariki wizi wa kura ukiachia mbali kutojua chanzo cha kuvunjika amani. Lijiepusha kuwa kama jeshi la polisi lililoua wananchi kule Zanzibar mwaka 2001 ukiachia mbali kuwa kinara wa rushwa na ujambazi nchini.

Jeshi la Mafisadi wa CCM halipaswi kuitwa jeshi la wananchi wa Tanzania. Haya ni matusi ya nguoni. Jeshi liache kutuchokoza na kutoa visingizio vya kitoto.


NB: Wasomaji mnaweza pia kupitia kwenye taarifa ya Human Rights Watch juu ya uvunjaji wa amani na mauaji ya Zanzibar ya mwaka 2001 vilivyofanywa na jeshi la polisi. Soma kwenye comments utaiona kwenye maoni yaliyotolewa na ndugu MBELE.

10 comments:

Anonymous said...

Ni kweli jeshi letu limepoteza heshima na maana. Kikwete amegeuka mzigo kwa kila mtu na hafai hata jeshi liingelie kati. Hii ya The Hague ni jibu kwa ubabaishaji na vitisho vya jeshi.

Mbele said...

Nimechungulia kwenye taarifa magazeti, na kama kilichoandikwa ndicho kilichosemwa na Afande, sina matatizo na kauli zake.

Ila tu, napenda kukumbushia kwamba CCM ina historia ya kuhujumu amani, kama ilivyotokea Visiwani mwaka 2001. Taarifa ya Human Rights Watch inaonyesha kuwa CCM na polisi ndio chimbuko la matatizo yale.

Kwa hivi, jeshi lijitahidi kuichunga CCM, maana watu wanaogopa yaliyotokea kabla, kama vile kuibiwa kura. Hii hofu ya kuibiwa kura na CCM iko, na niliishuhudia nilipokuwa Tanzania kuanzia mwezi Juni hadi Agosti.

CCM itamke hadharani, na isisitize na kuthibitisha kabisa, kwamba haina mpango wa kuvuruga uchaguzi, wala kuiba kura. Hii ni muhimu katika suala la kuhakikisha kuwepo kwa amani.

Mimi kama raia ambaye si mwanachama wa chama chochote ninasikitishwa na hali iliyopo, ya watu kuogopa kuibiwa kura zao. Na kwenye hizi kampeni, naona jinsi wapinzani wanavyohangaikia suala hili, wakitafuta mbinu za kulinda kura.

Mazingira ya hofu namna hii ndio mazingira yanayokaribisha uvunjikaji wa amani. Hii hofu inatokana na yale yaliyotokea kabla.

Ningetegemea kuwa rais angeweka kipaumbele kwenye kuhakikisha kuwa kuna amani nchini, hata ikibidi kuwakemea CCM ambao kuna taarifa kuwa wamekuwa wakileta vurugu.
Sijamsikia amewakemea hao CCM. Amezama kwenye kampeni kama mgombea wa CCM, badala ya kukumbuka kuwa ana kofia ya urais ambayo inamlazimisha kuweka mbele maslahi ya nchi kwanza, si maslahi ya chama.

Mimi kama m-Tanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote naifikiria nchi yangu. Sina undugu na chama chochote, na hata vikisambaratika, nchi itabaki. Nchi ilikuwepo kabla ya vyama, kabla ya CCM, kabla ya TANU. Vyama vyote vikienda na maji, nchi itabaki. Namtegemea rais wa nchi akumbuke jambo hilo na kulizingatia.

Taarifa ya Human Rights Watch,ambayo inaonyesha jinsi kule Visiwani CCM ilivyofanya hujuma na uchokozi, na jinsi polisi ilivyofanya umachinga kwa CCM, ni hii hapa.

NN Mhango said...

Nakushukuru sana Bro. Mbele kwa mchango wako uliosogeza wazo langu mbele zaidi. Ingawa sikubaliani na yote uliyosema, kuna haja ya kukubaliana kuwa nchi haiwezi kuishi bila uongozi. Hivyo, ni kweli kuwa vyama vinaweza kupotelea mbali na taifa likabaki. Lazima liwe na mfumo ongozi uliojikita kwenye utashi na maendeleo ya watu na si kikundi cha wezi wachache kama ilivyo nchini kwetu. Kama wasomi na Thinkers, tunapaswa kulisimamia na kulisisitizia hili kwa nguvu zote. Kuna haja ya kuondokana na CCM na kuanza upya kuanzia alipotuacha Mwl. Julius Nyerere.
Na hatuwezi kuanza bila kuanza na kuifurusha CCM ili tujue mwelekeo wetu kama taifa na jamii ya watu wenye akili na utashi wa kuendelea kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Mbele said...

Hata mimi msimamo wangu ni huo huo ulioufafanua, kwamba tuwe na "mfumo wa uongozi uliojikita kwenye utashi na maendeleo ya watu na si kikundi cha wezi wachache..."

Hii ndio maana halisi ya demokrasia. Tatizo ninaloona ni kuwa wa-Tanzania, bila kutafakari historia yao na uhalisi wake, bila kutumia fikra huru, wameiga tu dhana ya chama au vyama.

Mfumo wa chama au vyama ulibuniwa Ulaya, na huenda unalingana na historia na uhalisi wa maisha yao, na kadhalika.

Watanzania hatukufanya tathmini, ya uhalisia wa kule tulikotoka, katika historia au utamaduni wetu, bali tuliiga dhana ya chama au vyama tangu wakati wa ukoloni, na leo tunashinikizwa kwamba lazima tuwe na vyama. Kinachoendelea leo ni ukoloni mambo leo, si matokeo ya fikra huru zetu wenyewe.

Tukirudi kwenye ile tafsiri ya demokrasia uliyotoa hapa juu, na ambayo tunakubaliana, utaona kuwa kitu kinachoitwa chama au vyama haiko pale.

Sasa hapo ndipo ninaposema kuwa wa_Tanzania tutafute mfumo unaoweza kutufanya tuwe na demokrasia au tujenge demokrasia.

Wahenga wetu walikuwa na mfumo wa demokrasia. Lakini hawakuwa na chama au vyama. Je, sisi wa-Tanzania hatuwezi tukawa na fikra huru, bila kuiga mambo ya Ulaya, tukatafuta njia ya kujenga demokrasia ambayo inaendana na uhalisi wa historia, jadi na mila zetu kama wa-Afrika?

Tumepoteza hata uhuru wa kuuliza suali hili na kulitafakari au kujaribu mfumo mwingine. Tukithubutu, waheshimiwa waliotutawala zamani watatuadhibu. Ndio maana nasema tunachoshabikia wa-Tanzania kinaonekana kama mfumo wa kujenga demokrasia nchini kwetu, kumbe ni ukoloni mambo leo.


Mfumo huu wa chama au vyama unatuletea migogoro ya wazi, kama tunavyoona. Mtafaruku unaonekana wazi katika jamii yetu. Ni ushahidi wa yale ninayosema, kwamba kuna haja ya sisi kuwa na fikra huru na kutafuta mfumo unaotufaa, na naamini utakuwa ni mfumo wa demokrasia bila chama au vyama. Ndio maana nasema kuwa vyama viende na maji, naona sawa tu.

Katika kuongelea demokrasia ya wahenga wetu, Mwalimu Nyerere alisema kuwa wazee walikuwa wanakaa chini ya mti na kujadiliana hadi wakubaliane. Ule ni mfumo walioutumia, na haukuwa wa kuigwa au kushinikizwa kama huu mfumo wa chama au vyama.

Haya ni baadhi ya masuali ambayo nimeyauliza kwa undani zaidi katika kitabu changu cha CHANGAMOTO.

NN Mhango said...

Hapa nimekupata Bro. Mbele. Huu umekuwa ugomvi wangu na mfumo wetu wa uombaomba ambapo rais mzima wa nchi anakwenda akijipiga kifua na majisifu kwenda kupiga magoti kwa rais mwenzie kuomba-umatonya.

Kimsingi fikra zako zinahitaji mfumo mpya wa kufikiri ambao hauko pengine bali kufumua na kufuma upya mfumo wetu wa elimu ambao ni muendelezo wa fikra tegemezi.

Sipendi vyama na sina chama zaidi ya kuamini katika freethinking. Tofauti yangu ni kwamba tunaweza kuanza kuzamisha chama nyemelezi kwa kuchagua vingine ili hapo baadaye utokee msuguano wa kuunda mseto kama tulivyoona Kenya. Matokeo ya msuguano huu ni kupatikana kwa katiba mpya itokanayo na wananchi. Kuuzika mfumo mfu wa sasa unaosimamiwa na kulindwa na wezi-nufaika si suala la kufumba na kufumbua. Tunaweza kuanza kutoa adabu kwa kuipiga teke CCM na kuwaambia wanaoingia kuwa huu ni mwanzo wa mambo.

Japo umependekeza mfumo-huru na asilia wa demokrasia ya kiafrika wa kukaa chini ya mti-bunge, je ni wasomi wangapi tulio nao wana mawazo kama haya au kuunga mkono wazo hili na kulifanyia kazi? Tuna madaktari na maprofesa wengi wasio na hadhi hata ya kugusa kiatu cha profesa wa kweli. Huwa nina mfano rahisi. Je marehemu Abeid Karume na Dokta Salmin Amour nani ni msomi hasa ukiangalia walichofanya kama viongozi wa Zanzibar?

Nakubaliana nawe. Leo utamkua profesa kama Ibrahim Lipumba akifungwa na chama kiasi cha kusimamisha ubongo wake na kuanza kukimbiza ruzuku huku akiendeshwa na Maalim Seif.

Wapo madaktari kama Lamwai Masumbuko. Warid Kaboro na wengine walioamua kujigeuza mbwa badala ya mbwamwitu wanaohenyeshwa na zuzu kama Yusuf Makamba, Kinana, Rostam Aziz, Edward Lowassa hata Jakaya Kikwete.

Nimejadili ugonjwa huu kwenye kitabu changu cha SAA YA UKOMBOZI na kuutolea mifano hai kwenye kitabu kingine ambacho kiko mbioni kutoka cha NYUMA YA PAZIA.
Nimefarijika na kunufaika na uoni wako usio upogo wala makengeza bali miali ya ukombozi na utambuzi vinavyolenga kuirejesha heshima ya taifa na jamii yetu.

emu-three said...

Mimi sijui kwanini, kwasababu polisi na jeshi ni serikali. Kazi yao ni kukaa pembeni ili kukipokea chama kitakachotawala...je linafanyika hilo?
'Kuna dalili' Je ni nani akemee kama hizo dalili zipo? Ni polisi, au ni nani? Je anayeongea hapo kapata kibali toka kwanani? Au yeye ana `amri hiyo' kusema pale kunapotokea fununu?
Labda tuelimishwe kidogo na wahusikia, isije tukalaumu bure!

Mbele said...

Ndugu Mhango, shukrani kwa changamoto hizo zote. Tuendelee kuyatafakari masuala haya ya Taifa letu na dunia kwa ujumla.

NN Mhango said...

Asante sana ndugu yangu Mbele kwa michango na changamoto zako ukiachia mbali kunitembelea. Jana nilikutembelea na kufurahia mandhari ya mji wetu wa Lushoto ukiachia mbali kukumbuka historia yake ya miaka 1950.
Kwa vile hujawahi kuishiwa kufikiri na kuandika, naamini moto utakuwa ule ule wa kuikomboa jamii yetu na kuonekana watu kati ya watu.
Kila la heri

Anonymous said...

Gen Shimbo kachemka kwelikweli.
Wanajeshi wote wa HadHi yake Duniani hukaa kimya kupanga mikakati ya kuchukua nchi kama jeshi pindi mambo yakienda kingelenyuma.
Sasa huyu Habithi wa kijeshi anashabikia chama,anakubali kukaa mkiani ukingoni mwa VENT ya CCM,anakubali kutumiwa kama ya ndani na wanasiasa wenye matumbo yasiyo shiba kaa magari yakusomba taka.CCM watamtumia kuwatia hofu wananchi kisha watamtosa kama chambio.
Kwa Mjeshi kujenga uaminifu wa dhati chini ya chama cha kisiasa ni sawa kabisa na kulala na changu doa kisha asubuhi yake kukurupuka kwamba na kupigia simu wazazi wako kwamba umechumbia na mipango ya koana iko mbioni. Wewe kama ni mjeshi Heshima na Uaminifu wako ni chini ya serikali. Kama huridhiki na serikali unachukua nchi kinguvu wewe mwenyewe.
Acha kijipendekeza kishamba Gen Shimbo.

MADELA WA MADILU

Anonymous said...

vlaganje denarja [url=http://www.vzajemniskladi.info]alta skladi[/url]