Thursday, 28 October 2010

Chonde chonde CCM, damu mliyomwaga inatoshaCHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kupitia mgombea wake wa urais na wapambe zake, waliposema kuna njama za Watanzania kumwaga damu, wengi hawakuwabana wawataje wahusika.

Wao (CCM) walilenga kuuchafua upinzani kutokana na sera kuu ya CCM kwenye kampeni zinazomalizika kwa kuchafuana. Bahati nzuri ni kwamba Mungu huwa hamfichi mnafiki. Kwa yaliyoripotiwa hivi karibuni kutendwa na mashabiki wa CCM, Mungu amewafichua. Watawambia nini watanzania waliowahadaa kwa kuwasingizia wenzao?

Kwa wanaojua mizengwe ya CCM, walijua walichokuwa wakimaanisha wakubwa hawa wa CCM. Walimaanisha tofauti na walivyosema kama kawaida yao. Rejea madai mengi dhidi ya kuondoa kero mbali na kutoa ahadi nyingi ambazo ziligeuka kuwa usanii. Walitumia mbinu ambayo wazungu huita pre-emptive method wasijue yatawarudi!

Hii imekuwa sawa na walivyowahadaa watanzania kuwa watapambana na mafisadi wakaishia kuwapamba, kuleta maendeleo wakaishia kuleta maanguko na ufisadi. Rejea hatua ya wazi ya Kikwete kusimama bila aibu kuwapigia kampeni watuhumiwa wakuu wa ufisadi wa mabilioni yaliyowaacha Watanzania maskini. Hapa hujaongelea matumizi mabaya ya fedha na raslimali za umma.

Sasa hayawi hayawi huwa! CCM imekamatwa red handed ikitekeleza kile vigogo wake walichojifanya kulaani! Kumbe danganya toto!

Mara kadhaa Kikwete amenukuliwa akisema: “Sisi ni CCM. Sisi ni chama kisichohubiri umwagaji damu. Sisi ni chama cha amani. Umwagaji damu hauna maslahi yoyote na wala tija kwa yoyote isipokuwa kwa wanasiasa wanaotaka kutumia maiti za watu kama ngazi ya kuingilia Ikulu.”

Je, kweli CCM ni chama cha amani au vurugu? Inakuwaje kama ni chama cha amani kisilaani vitisho vilivyotolewa hivi karibuni na mnadhimu mkuu wa jeshi ukiachia mbali mganga na mtabiri wake, Yahya Hussein? Inakuwaje kisizuie vikundi vyake vya kigaidi vya Green Guard kuwakata watu wasio na hatia mapanga? Amani gani ndani ya migawanyiko, vurugu, rushwa, ukosefu wa haki, ufisadi na mitandao?

Baada ya kugundua uzushi wa CCM mpinzani wao mkuu kwenye mbio hizi CHADEMA walikaririwa wakisema: “Mimi sitaki kwenda Ikulu kwa kumwaga damu ya Mtanzania yeyote. Sijatamka hata siku moja kumwaga damu. Nataka uchaguzi wa amani na utulivu. Katika mikutano yangu zaidi ya 400 niliyofanya sasa, nimehimiza watu wangu kuzingatia amani…Nyie mkipigwa shavu hili geuza jingine, msiwe chanzo cha vurugu,” alikaririwa mgombea wa CHADEMA wa uraia Dk. Willibrod Slaa akisema.

Hata hivyo kuna maswali muhimu ya kujiuliza juu ya nani yuko tayari kumwaga damu. Nani anamiliki vyombo vya dola vinavyoweza kusababisha umwagaji damu zaidi ya serikali?

Maana tuliona kenya. Watu wengi waliouawa wanasemekana waliuawa na Jeshi la Polisi kutokana na amri za wakubwa wao. Hata yale mauaji yalilitia doa jina la Tanzania ya Zanzibar, walioua ni polisi na si wanasiasa wa upinzani.

Pia ikizingatiwa kuwa taarifa zote za usalama zimo mikononi mwa serikali, inashangaza kuona serikali haiwashughulikii hawa wabaya wa taifa. Lakini nani atawashughulikia iwapo wanatekeleza amri za wenye serikali yenyewe?

Yaliyojitokeza kwenye Jimbo la Musoma na Maswa hivi karibuni ni ushahidi kuwa watuhumiwa waliokuwa wakitajwa na CCM kumbe ni CCM wenyewe. Rejea watu kadhaa wa wakazi wa Kigera Musoma kukatwa katwa mapanga na wafuasi wa CCM maarufu kama Green Guards.

Waliokumbwa na mkasa huu walitajwa kama Suleman Mwita ambaye alidai kuwa viongozi wa CCM tawini Kigera walisimamia unyama huu. Ajabu CHADEMA wanaodaiwa kumwaga damu ndiyo wamethibitisha kuwa waokozi. Maana Mwita alikaririwa akisema: “Wakati nikiokolewa na wananchi kidogo likatokea gari la mgombea wa CHADEMA, Vincent Nyerere, ambalo lilinichukua na kunipeleka polisi kupata fomu namba tatu ya polisi kisha kunipeleka hospitalini.”

Mwingine aliyeathirika na vurugu hizi ni mtoto Rahab Malima (15) ambaye kosa lake ni kuzaliwa na mama Tatu William aliyeruhusu bendera ya CHADEMA kupepea nyumbani kwake. Kosa la kupeperusha bendera ya CHADEMA limesababisha Rahab kukatwa vidole vya mkono wa kulia!

Mbali na watajwa hapo juu, wengine waliojeruhiwa ni Kapuru Charles (44) na Mapambano Malima (30) wote wakazi wa Kigera. Bahati nzuri CCM haikukanusha habari husika ukiachia mbali na nyingine kama hii iliyoripoti wana CCM kufanya mashambulizi ya umwagaji damu kule Busanda mnamo mwenzi wa tisa.

Kwanini wahusika hawakamatwi? Hili ni swali litakalokuwa likiwahangaisha wengi. Jibu wanalo Charles Kayele, Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Musoma na mgombea ubungu wa CHADEMA, Vincent Nyerere waliokaririwa wakisema kuwa vyombo vya dola vimekuwa vikifumbia macho malalamiko dhidi ya CCM.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Musoma Haula Kachwamba, alipotakiwa kuelezea malalamiko dhidi ya chama chake alisema hana, kwa vile suala hili lilikuwa la polisi!

Hapo juu ni tukio moja kwenye eneo moja. Yapo mengi mengine kama haya. Nani mara hii kasahau unyama uliofanyika jimboni Busanda au Hai bila kusahau vurugu na vitimbwi huko Arusha?

Inabidi umma uibane CCM iache kumwaga damu. Damu haina uchache wala wingi zaidi ya kuwa damu. Tone moja la damu ya Mtanzania ni sawa na damu ya Watanzania wote.

CCM imeisharidhia umwagaji wa damu za vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi hadi kufikia kuteua mgombea anayehusishwa na jinai hii. Hii inatosha. Inatosha. Hakuna haja ya kuvuka mpaka na kuendeleza mauaji kama ilivyotokea kwenye visa vya hapo juu.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 27, 2010.

1 comment:

Anonymous said...

Hii atiko nzuri sana imefanyiwa utafiti vya kutosha-- CCM imeachwa uchi. Good piece mr Mhango.