How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 2 October 2010

Shehe Mpayukaji atoa kinga kwa mgombea

WIKI jana nilieleza utabiri wangu ambao si sawa na yule mpiga wa Migomigo aitwaye Shehe Ubwabwa Yaya. Mie ni mtabiri tena msomi aliyesoma somo la Nyotology, Ontology, Metaphysic na Astrology na kutoka na alama A.

Unaweza kuona jinsi ambavyo sitabirii njaa wala kutafuta kujikomba ili nipewe mabaki yatokanayo na pesa ya ufisadi.

Natoa kinga bure wala sihitaji kusafirishwa kwenda India. Hata nikiumwa nikahitaji kwenda kule nitakwenda kwa pesa yangu halali na si makombo ya mafisadi. Nitatoa kinga kwa mgombea anayeuzika na asiye shirika na mafisadi.

Hili halihitaji ruksa ya mtu wala taasisi. I mean it. This is not a calumny or con aiming at anybody. Sorry. Siku hizi nina ka-ugonjwa kama ka waheshimiwa wasio heshima kitu ambao hawamalizi sentensi bila kumwanga ung'enge uchwara ili waonekane wasomi ingawa wengi wao ni vilaza walioghushi vyeti. Hayo tuyaache. Nani atawagusa iwapo mwenzao mwenye madaraka ameamua kuwakingia kifua ili watumiane?

Hamkumsikia juzi akimuombolezea na kumwagia sifa Ewassa kwa kusema eti ni mchapakazi duniani hakuna! Wakubwa kwa kupenda kusifiana. Anyway, leo humu si mwake. Kuna siku nitawatokea kinoma ili wajue njemba nipo na bado nawapumulia kisogoni.

Kwanza nitawatajia nyota za wagombea wanaotisha kwenye kijiwe chetu, yaani Njaa Kali na Willie.

Nyota ya wa kwanza yaani Njaa Kali ni aina ya Al-dhi’b wal shaari yaani mbwa mwitu wa shari na jini wake ni infritah ambaye ni mbaya kuliko shaytan mwenyewe. Huyu jini akikupenda utapendwa. Akichukia utachukiwa hadi ujichukie.

Anapokuwa amechukia mwenye kuwa naye huanguka hovyo hovyo na kutamka maneno bila kuyamalizia. Ni jini mbaya sana ambaye anaweza kusababisha mtu kupenda ngono hata starehe. Nyota ya mama yake ni mkia yaani Al dhayl yaani asiye na faida sawa na mkia kama wenye nyota hii.

Kwa wale waliosoma khutba al Dhayl Lisan al-mizan wajikumbushe maneno: Ruwat duafa aw tukullima fihim, lam yudhkaru fi kutub al-duafa wa-al-mutakallam fihim, wanaweza kujua nimaanishacho hapa ingawa kinyume. Msiende ndani hivyo. Huko ni kwa magwiji kwenye kunga. Hivyo chukulia hiyo kama rejea tu. Kumradhi kwa kuwakoga kwa usomi wangu wa fani ya utabiri.

Jini huyu hupenda kuwafanya wenye kuwa naye kuwa na uwezo mdogo wa kufikiri ukiachia mbali kuwanyima aibu. Huwafanya wachekecheke hovyo hata mahali pasipostahili kiasi cha kuonekana kama watu wa mzaha mzaha ambao ni rahisi kutumiwa na watu wengine kufikia malengo yao. Wenye jini huyu ni watu wa kuhurumiwa.

Kwani mara nyingi huwa hawajijui wala kujua wanachofanya zaidi ya kuwa watumwa hasa wa sifa za kipuuzi. Huwafanya wafanye vitu vya kipuuzi ambavyo huviona vya maana huku vya maana wakiviona vya kipuuzi.

Watu wenye jini huyu, kama ni wanaume, huwekwa mikononi na wanawake na kama ni wanawake huwa asharati hakuna mfano. Kwa wanaume huwa hawajiwezi kimapenzi yaani wako tayari hata kutembea kwa magoti ilmradi wapewe ngono hata kama ni kwa kuhatarisha usalama wao. Hawafai kuongoza hata kaya achia mbali taifa.

Wanapopata madaraka basi jua rushwa ya ngono itakuwa kubwa na kina mama hasa wenye uhusiano nao watapewa vyeo kama asante ya huduma yao.

Sasa nije kwa huyu wa pili. Huyo nyota yake ni ni Al Maisan wal Heri. Hii ni nyota nzuri sana kuwa nayo. Mtu mwenye nyota hii hupendwa na kuenziwa. Hata akifanya makosa kidogo husamehewa haraka kutokana na kuwa na vipaji vingi.

Mwenye nyota hii ni mpenzi wa watu ambaye mara nyingi yuko tayari hata kupoteza uhai wake kwa ajili yao. Si rahisi kutumiwa, kuhongwa, kudanganywa wala kugeuzwa juha iwe na wanaume au wanawake.

Jini la huyu wa pili ni Al-Nasr At-Ta'ir au tumbusi anayepaa. Huyu ni hodari wa kufanya mambo ya maana. Ni jabali hasa ambaye hata akisema kitu kinashawishi na kuaminika.

Hana mzaha katika shughuli zake. Si mkurupukaji wala mbabaishaji. Akisema kitu lazima akitolee ushahidi tena wenye kuingia akilini siyo bora ushahidi. Si rahisi kutumiwa na watu zaidi ya yeye kuwaongoza katika ufanisi. Huyu anaweza kuaminiwa hasa uongozi wa nchi hasa kama yetu iliyoko kwenye makucha ya mafisadi.

Kwa vile mpinzani wake ameaahidiwa ulinzi wa majini, japo nao ni upuuzi nami leo natangaza rasmi kuwa mgombea wangu daktari atapewa ulinzi wangu. Ulinzi wangu unajulikana na kuingia akilini. Ulinzi huu si mwingine bali kuwataka wananchi wampe kura kwa wingi awatumikie na kuwaondoa kwenye uchafu wa hawa wachovu mafisadi wasio na visheni wala utu. Mpeni kura WS mjionee mambo.

Mkimpenda mkamchagua na kumuunga mkono nani mwingine atamdhuru? Afya yake ni fit na hana ugogoro wala la kuficha. Hivyo ulinzi wangu ni kura ya ndiyo na si majini uchwara yatokanayo na njaa na kujipendekeza.

Ulinzi mwingine ni kumtangaza kila kosa hadi kila mpiga kura popote alipo amfahamu na kumkubali kuwa anaweza kutuvusha kama tutamwingiza madarakani na kumbana atimize ahadi zake anazotoa leo ili asiwe kama JK aliyeahidi pepo akaleta ghalika.

Maana wale wezi wamekuwa wakitumia ujinga na ukosefu wa habari kama jimbo lao ukiachia mbali kuwageuza wapiga kura maskini na wajinga shamba la bibi la mafisadi kujihomolea kama ambavyo wamekuwa wakifanya miaka nenda rudi.

Mwaka huu kiutaalam wa utabiri ni mwaka wa ngurumo ambazo zitasikika toka Danganyika karibu maeneo yote hadi mji wa The Hague. Hii maana yake ni kwamba wagombea wanaoshinda kwa kutegemea kuiba kura hawatafanikiwa mwaka huu kutokana na wapinzani wao kuwa makini na tayari kufa wakilinda kura zao.

Hali hii itasababisha malumbano hadi watu kunyea debe kama wataendelea na jinai hii. Kuondokana na hili ni kwa wahusika, hasa wale wezi wa kura, kuachana na jaribio hili. Maana wakati umebadilika. Kondoo wanaweza kuwatembezea kichapo hadi hata kuwaua fisi.

Na wakati wenye ndiyo huu ambapo hakitaeleweka hadi haki itendeke. Na wananchi wasiogope. Utabiri unaonyesha kuwa atakayethubutu kuiba kura atashindwa hata kufungwa. Natabiri kuwa mwaka huu Tanzania inaweza kufanya maajabu kwa kuwapiga teke wababaishaji na watesi wa taifa. Lolote lawezekana.

Wapiga kula msicheze chandimu wakati kuna chakudema. Nyinyi ni malaika na walinzi wa ukombozi. Hivyo. nitatoa ulinzi wa malaika si majini ya wale washenzi na washirikina wasiojiamini.

Natabiri kuwa kijiwe kitakomea hapa leo.

El Commandante Mwenyewe.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 29, 2010.

No comments: