How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Monday, 11 October 2010
Miaka 11 bila Nyerere: Ni fitina, unafiki mtupu
KESHO ni Oktoba 14, siku ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa taifa, Julius Nyerere kilichotokea Uingereza mwaka 1999.
Mwaka huu ukiwa wa 11 tangu mwasisi huyo wa taifa la Tanzania afariki, pengo lake linaonekana kila siku na kila mahali. Chini ya uongozi wake (si utawala), nchi ilijijengea heshima kubwa ndani na nje hata kama ilikuwa maskini kwa kiasi fulani.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) alichoasisi mwaka 1977, kilikuwa mfano wa kuigwa. Kiliheshimika, kupendwa na kuaminika tofauti na sasa. CCM chini ya Mwalimu haikuwa inazomewa na hakukuwa na kashfa lukuki.
Hakikuwa na vinyamkera na changudoa wa kisiasa na kimaadili kwenye ofisi na safu yake ya uongozi. Nani angeweza kuingia kwenye ofisi zilizoongozwa na mtu mwenye udhu ili kutafuta kujaza tumbo lake?
Leo ni tofauti, watuhumiwa wa ujambazi, wauzaji dawa za kulevya, wezi wa pesa katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), wenye kashfa ya rushwa ya rada na mkataba wa kifisadi wa Richmond; wanapigiwa debe nao wawe viongozi.
Yako wapi maadili aliyosisitiza Mwalimu?
Waandishi wa habari sasa wamegeuka mbwa mwitu wakiandika kila aina ya uchafu na uongo ili wazawadiwe vyeo serikalini na kwenye chama. Uko wapi uadilifu wa kitaaluma?
CCM ya Nyerere ilifanya mengi, kubwa zaidi likiwa kutoa huduma za jamii bure na kujenga jamii ya watu walio sawa bila kujali rangi, kipato wala mtu atokako. Mbona leo pengo kati ya maskini na matajiri ni kubwa?
Viongozi waliolelewa chini ya misingi ya uadilifu ya Mwalimu, sasa wamekuwa fisi wanakula bila kunawa wala kusaza raslimali za nchi. Huko ndiko kumuenzi Baba wa Taifa?
Watu wenye fikra, visheni na utashi wanasema elimu na huduma za jamii zinaweza kutolewa bure kwa jamii, lakini viongozi waliopo wanathibitisha aliyosema Horace Kolimba, kwamba hawana dira. Wameng’ang’ana kuwa haiwezekani. Kwa nini hawafunguki akili?
Mwalimu angekuwepo angewaambia viongozi hawa kuwa elimu bure inawezekana. Angekemea ulafi huu wa raslimali; angekemea mafisadi, matajiri kutawala siasa na serikali kukumbatia matajiri.
Katika kipindi cha miaka mitano serikali imetengeneza mafisadi 11; wameshiuka chama na serikali; viongozi hawafurukuti kwa sababu baadhi ya mafisadi ni viongozi wa serikali.
Mafisadi hawa wanauza viwanja, wale wanatia saini mikataba na kupewa ahsante ya asilimia 10; wengine wanakula kupitia madini na baadhi wanakulipa kwa kampuni hewa. Viongozi wakubwa kwa wadogo wanakula nchi; aibu tupu.
Watanzania watamuenzi Mwalimu kwa aibu na unafiki? Watasoma risala za utii, watasema huku wamejishika vifua kwa hisia kali, watadai wao wanafuata nyayo za Mwalimu lakini kwa uongo mwingi.
Watu wenye akili wanacheka hususan wakiona mambo yanayofanyika sasa.
Wanasema huwezi kumuenzi shujaa kama huyu kwa mipango ya kuhujumu demokrasia, kutoa ahadi za uongo na kufanya usanii.
Huwezi kumuenzi Mwalimu kwa kutegemea ushirikina na ramli; kwa wizi wa mali ya umma au ufisadi; kwa kutumia vibaya na kufuja fedha za serikali.
Huwezi kumuenzi Mwalimu kwa kukwapua raslimali za taifa alizotunza kwa ajili ya vizazi vijavyo; kwa kutoa madaraka kwa kujuana (ndugunaizeisheni).
Wenye akili wanasema huwezi kumuenzi Mwalimu kwa kuendekeza unafiki na lugha tamu wakati matendo ni mabaya; kwa kuendekeza utawala uliogeuka ulaji na kulipana fadhila.
Huwezi kumuenzi mwalimu kwa uchafuzi wa maadili na mazingira kama vile watu wa Buhemba walioachiwa mashimo na wawekezaji baada ya kuchukua madini.
Viongozi hawawezi kusema wanamuezi Mwalimu kwa kuwafukuza wachimbaji wadogo na nafasi yao kuchukuliwa na makampuni ya kigeni.
Madhara yake ni wazi kabisa: Wachimbaji wa Mererani, North Mara, Buzwagi wamegeuka vibarua katika machimbo yao na nje ya migodi.
Watu waliosoma, kufanya kazi na kumpenda Mwalimu wanajisikia vipi wanapoona urithi aliouacha unachotwa na wachache?
Mwalimu alipokuwa anahoji watu wanaokimbilia ikulu, hakuwa anamaanisha wapinzani tu bali hata wanachama wa CCM, kwamba baadhi yao hawakuwa na sifa.
Mwalimu alisimamia mchakato wa kupata viongozi safi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 Miaka minne baadaye akaaga dunia.
Tangu hapo na mambo yalianza kuharibika. Viongozi wameweka kando miiko ya uongozi na misingi ya utawala bora. Sasa ni bora liende.
Chanzo: MwanaHALISI Oktoba 13,2010.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment