Friday, 22 October 2010

Msiwaone wameacha kuvaa suti mkadhani ni wenzenu

SIKU hizi mzee mzima nimegeuka researcher au mtafiti kwa lugha isiyo ya kisomi. Natafiti kila kitu. Ila kwa kipindi hiki cha uongo na ujambazi mbuzi, nimejikita kwenye kampeni na kampani za uchafuzi wa uchaguzi. Katika utafiti wangu nimegundua mambo kadhaa ambayo walevi wanapaswa kujua na kuchukua tahadhali kabla ya kubamizwa mkenge.

Mosi, walevi wa masuti, dhahabu, na viwalo vya bei mbaya ukiachia mbali kujiona wao ni bora kuliko wengine, siku hizi wamevikimbia hadi vinalalamika makabatini. Nani avae suti? Wale walevi wa uheshimiwa siku hizi hawautaki. Ukimwita mtu mheshimiwa anakukata jicho kali.

Anafanya hivyo kutokana na kutaka kumharibia kitumbua hasa kipindi hiki cha kusia uongo ili kuutafuta uongozi.

Hamuwaoni wakijidhalilisha kwa kutoa shikamoo, kupiga magoti hata wengine kukaa chini ili waonekane ni wenzenu wakati ni watesi wenu?

Vitu vilivyoshindikana kukwepwa ni mabodigadi, ulinzi wa majini, ndege na mishangingi waitumiayo kwenda uswekeni kuwaongopea, kuwakoga na kuwatapeli walevi. Hamkumuona msanii mmoja msaidizi akitoa ubani kwenye msiba wa mlalahoi kule kwa waja leo waondoka kesho? Hizo ndizo kampani za kampeni. Kila mnafiki na mfisidi na hasidi atajifanya rafiki ilhali akiomba umpe kura yako kesho akukomeshe kwa kukuuza wewe na uzao wako.

Msiamini uzao wa nyoka hata wakijigeuza miwa. Nyoka ni nyoka hata ajitoe magamba hageuki samaki. Msifanye kosa kudhani chui akivaa ngozi ya kondoo hugeuka kondoo. Kwanini sasa na si siku zote kama kweli hawa ni wenzenu? Nani anahitaji usuhuba wa kinafiki na kiwizi? Hili pamoja na mengine ni swali kuu la kujiuliza kabla ya kuamua nani wa kumpa na nani wa kumnyima.

Msiwaone wamekimbia suti mkadhani ni wenzenu kwa vile wanavaa mavazi casual kama yenu. Mioyoni wanawaona nyinyi mabwege hakuna mfano. Baada ya kupata wanachotafuta, neno ndugu wanalotumia sasa litakufa na kuja mheshimiwa tena mbaguzi ambaye hatawa kumbatia wala kuwasalimia kama sasa ambao wengine wanafikia eti kukaa kwenye mavumbi wakati wao ni wa peponi huku wengine wakiwapigia magoti msijue chambo!

Ni samaki gani anakamatwa kwa kuonyesha ndoana tupu zaidi ya kuwekewa nyama? Je ni aibu kiasi gani mja kutenzwa kama hayawani?

Wakishapata kula hata hamtawaona tena huko madongo poromoka na mkiwafuata huko mjini mtaitiwa polisi na kukamatwa kwa kosa la kuwaghasi wakubwa na waheshimiwa hata kama wezi wa miwa.

Hamjamuona jamaa yangu mpenda suti na viatu vya bei mbaya anavyovaa malapa huku mama akivaa shanga na kukwepa midhahabu. Yote juu ya nini? Walevi waingie mkenge wadhani ni wenzao wakati siyo. Walevi stukeni hao ni wezi wanaotaka kuiba maisha yenu kwa miaka mitano ijayo.

Nichagueni mimi baba Kidume muone nitakavyoipaisha nchi kama dege la Ewassa kwenda Kanani kweli si hii ya Njaa Kaya na kundi lake la wezi.

Jamaa zangu wauza unga na gongo kwa sasa wana likizo hadi mwezi Novemba. Leo haya sitayaongelea kwa undani. Ila kabla ya kwenda kwenye mada, acha nitabiri kuwa mwakani kutakuwa na serikali ya umoja wa kitaifa kama kura zitaibiwa. Yale aliyoshangaa Tunituni kule visiwani yako mlangoni kutokana na hali niliyoiona kwenye maenga yangu ya kitabiri.

Kuna jambo lenye kusikitisha lililonichekesha na kuniacha hoi.

Nani angeamini kuwa kwenye karne hii ya sayansi na teknolojia kungekuwa na mtu au watu wangedhani pikipiki za miguu mitatu Bajaj zingekuwa kichocheo cha 'maendeleo'?

Kinachogomba si watu kutumia bajaj bali ile hali ya ahadi ya kuleta maendeleo kwa bajaj kutolewa na wale wanaoshindana na waarabu kununua mashangingi!

Katika utafiti wangu nimegundua kuwa lisirikali la kaya yetu lina zaidi ya mashangingi 6,000. Hapa hujaongeza yale ambayo wezi wakubwa wameishauziana kwa bei mchekea. Huwezi kuamini mkuu wake eti anaahidi vibajaj 400 kwa ajili ya kubebea wajawazito!

Swali ni kwanini wazaa chema wabebwe kwenye bajaj wakati wezi na mafisi na mafisadi wakizawadiwa mashangingi kwa ushangingi wao kwa uchumi wetu? Kwanini bajaj iwapo watoto wa wezi wakubwa wananunua mihekalu ya mabilioni ukiachia mbali hongo za hapa na pale kwenye kampani za uchafuzi?

Ni uchuro kiasi gani kuona mahawala wa watu fulani wakipewa vyeo simply because wamevua nonihino zao? Kwani uongo? Kwani haya hayafanyiki tena mbele ya hadhira na nyuma ya pazia?

Inashangaza ukiachia mbali kuchefua. Kwanini vinchi vidogo viwe na ambulance sisi tuwe na bajaj pamoja na utitiri wote wa madini? Kwanini tuendelee kurudishwa nyuma kwa kudanganywa tunasonga mbele. Zamani tulikuwa na ambulance za land rover. Leo tunaambiwa tutapewa bajaj tunakubali na bado tunajiona tuna akili kweli! Tutukanwe matusi gani tusituke jamani?

Mie napendekeza tuwape bajaj watawala wetu badala ya mashangingi ili waonje utamu wake kama wanaona bajaj ni dili.

Hakuna kitu kilinishangaza ukiachia mbali kunichefua na kunichukiza kama upuuzi niliousoma kwenye magazeti fulani uchwara, moja la kimombo na jingine la msimu. Vyandudoa wa maadili wanaojiita waandishi wa habari ingawa ni wahandisi wa uongo wa habari, walikuwa wakisifia kila upuuzi wa Njaa Kaya.

Nasikia wameahidiwa ukuu wa wilaya hata ubalozi! Kama ni kweli tumekwisha. Hawa wanaoongoza matumbo yao hata kwa kujivua nguo wataongoza nini yarabi?

Ajabu bado hawa hawa wanawadanganya walevi kuwa wanaweza kuondosha maovu wakati waovu ni wao! Hivi unapogawa vyeo vya umma wa walevi kwa wahalifu kama hawa kwa sababu eti walikupigia debe, kuna uovu kuliko huu? Je huku si kutumiana? Ajabu jitu linapewa sifa za uongo nalo linaamini eti limesifiwa. Huu ni ukahaba wa kimaadili hata ungepewa jina la mikakati.

Inashangaza kuona baadhi ya ofisi za umma na kiama kujaa wahalifu! Wengi tunawajua hawana hata elimu ya kutosha ukiachia mbali kughushi vyeti. Ila kwa vile kayani kwetu kughushi si kosa tena sawa na kuibia mabenki, huenda watapewa hivyo vyeo vya aibu.

Anayetoa na kupokea cheo wote ni vyangudoa. Ni vyangudoa sawa na wale watabiri na wahubiri wa uongo.

Yule kidosho mali kweli. Acha nimfukuzie nipige kampeni ya kupata …..

Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 20,2010.

No comments: