The Chant of Savant

Thursday 10 November 2011

Anayeivuruga CCM kati ya hawa ni nani?

HIVI karibuni gazeti hili liliripoti kisa cha wenyeviti wa mikoa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kugawanyika kuhusiana na dhana nzima iliyokwama ya kujivua gamba.

Dhana hii ambayo, kimsingi, ilianzishwa na rais Jakaya Kikwete ama kwa makusudi au bahati mbaya, inaanza kumvua nguo baada ya kuonyesha wazi asivyo na ubavu wa kuwavua gamba watuhumiwa wawili yaani Andrew Chenge, waziri na mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali na Mbunge wa Bariadi Mashariki na Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli.

Matamshi ya baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa CCM yanatia kinyaa ukiachia mbali kuacha swali kama kweli bado CCM ina sera na udhu hata mshikamano. Maana huwezi kuamini kuwa mwenyekiti wa mkoa angeamka na kusema hadharani kuwa waziri fulani afukuzwe uanachama eti kwa vile alimtukana rais.

Tusi lenyewe eti ni kulumbana na spika. Kwanini kwa mfano waziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki Samuel (EAC), Sitta atuhumiwe kumtukana rais badala ya spika aliyekuwa akijadili jinsi upatikanaji wake ulivyokuwa mizengwe mitupu?

Kwa mujibu wa gazeti hili la Novemba 2, mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja alitaka Sitta atimuliwe kwa vile kwa mujibu wa Mgeja, Sitta alimtukana Rais Kikwete na wajumbe wa CC, kupitia kipindi cha dakika 45, kinachorushwa na kituo kimoja cha TV, akilalamika kwamba waliweka kigezo cha jinsi kwa shinikizo la mafisadi kumuengua kwenye kinyang’anyiro cha uspika ambacho kilijenga mazingira kwa Mama Anna Makinda kupita kirahisi.

Je, si kweli kuwa kigezo hiki walikiweka wao bila kutoa sababu na maelezo ya kufanya hivyo zaidi ya kumzuia Sitta?

Je, kama Sitta ni muongo au alimtukana Kikwete, kwanini Kikwete hakumwajibisha. Hapa anayemtukana Kikwete ni Sitta au Mgeja anayezusha mambo na kutoa ushauri wa uongo na usio na maana? Je Mgeja katumwa na nani kama si mafisadi hao hao ambao wanajulikana walivyo na mitandao nchi nzima. Kwanini kwa mfano Mgeja aone kosa la “kumtukana” rais alilotengeneza kuwa kubwa kuliko anaowatetea ambao, kama ni kumtukana Kikwete wamemtukana matusi ya nguoni kwa kukataa kujivua gamba wakiendelea kushikilia msimamo kuwa hawakukutana na Kikwete barabarani?

Je, ni uongo kuwa Makinda hakuchaguliwa kwa mizengwe ili kumzuia Sitta? Mbona akina Mgeja na wenzake wanakuwa kama hawajui kusoma na kuandika ambapo katiba imeweka wazi kuwa ubaguzi hauruhusiwi nchini?

Nini maana ya binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja ambayo ni mojawapo ya ahadi za mwana-CCM. Au ni kwa vile CCM imeegemea wenye nazo kiasi cha kuabudia madili badala ya maadili.

Baada ya kumalizana Sitta ambaye ameishaanza kuwa majeruhi kutokana na kile kinachoeelezewa kuwa ni kula huku na kule, kina Mgeja waliamua kumgeukia Nape Nnauye kuwa anakivuruga chama.

Nape anakivuruga vipi chama? Anataka mafisadi wavuliwe magamba. Wapo wanaoona kama Nape anatimiza maagizo ya bosi wake yaani rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa CCM. Pia wapo wanaoona kama Kikwete anaogopa kuwakabili watuhumiwa wa ufisadi wanaopaswa kujivua gamba kwa kuogopa wasimvue kofia.

Hili limethibitishwa na maneno ya hivi karibuni ya mtuhumiwa mmojawapo wa ufisadi ambaye alisisitiza kuwa yeye na Kikwete hawakukutana barabarani.

Kwa wanaojua siasa za nchi hii zilivyo chafu walijua kuwa huu ujumbe ulilenga kuwafikia wananchi ili wakate tamaa huku ukimkumbusha Kikwete kuwa ajue rafiki yake anamjua kuliko tunavyomjua. Hivyo apunguze mwendo kwenye kasi yake mpya na ari mpya na nguvu mpya ya kumwagiza Nape awashambulie.

Kuhusiana na Nape ni bahati mbaya kuwa Kikwete hajawahi kukanusha madai kuwa anamtumia kuwashambulia marafiki zake ambao hana ubavu wa kuwaambia “uso kwa uso kuwa tokeni mmechafuka na kuchafua chama.” Wapo wanaoona kama Kikwete hana jinsi na anachofanya ni sawa kwa vile naye alitajwa kwenye orodha hiyo hiyo iliyowazaa hao magamba ya chama chake.

Je, kuna ukweli nyuma ya dhana hii kuwa Kikwete anawagwaya akina Lowassa na hivyo kumtumia Nape? Yote yawezekana. Jiulize Nape anapata wapi jeuri ya kuwakabilia hawa watuhumiwa wakati wengine wamenywea? Yuko wapi Wilson Mukama aliyeingia ofisini na viapo kuwa atakisafisha chama asijue kitamchafua na atanywea kama alivyofanya.

Swali kuu ni je nani wanakivuruga chama kati ya akina Mgeja, Nape, Sitta, Lowassa na Kikwete? Je, kwa wanachama wa CCM kujiweka rehani na kando wasiingilie kunusuru chama chao nao hawakivurugi? Maana inaonekana wanatumika kama kondoo kuswagwa wasipojua wala kutaka bali mswagaji.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 9, 2011.

No comments: