The Chant of Savant

Friday 4 November 2011

Mpayukaji kwenda kuchunguza afya India

BAADA ya kuona wazito wote wanaougua wanapelekwa India, Mpayukaji naye ingawa ni mzito wa wanywa kahawa, ameamuru achangiwe madafu kiasi fulani aende kuchunguza afya yake. Sababu nyingine iliyomsukuma Mpayukaji kwenda India ni ile ya maadui zake kwenye kijiwe hasa wale wanaotaka afe wachukue ukuu kudhamiria kumnyotoa roho ima kwa sumu, nondo, kabari au mshale.

Habari za kiintelijensia ambazo Mpayukaji anazo ni kwamba pale kijiweni kuna wabaya wake wanaoongozwa na Mbwamwitu almaarufu akishirikiana na mwenzake.

Shushu wake mkuu mzee Machungi wa Mgosi ametoka Tanga hivi karibuni kutafuta zindiko la uchawi. Kwa vile wabaya wake wanataka kumlisha sumu na juzi amejisikia kuwashwa washwa na ukurutu sehemu za nonihino, ameamua kwenda zake India naye aonje huu ubora unaowapeleka wagogo na vigogo kwenda kutibiwa kule.

Sababu ya tatu ni kwamba kwa vile Mpayukaji anapanga kugombea ukuu wa Kaya, anaenda kule kuona hizo hospitali za kihindi zinazomaliza njuluku za Wadanganyika zimejengwa kwa ubora gani ili akiukwaa azijenge hapa na kuokoa pesa ya walala kizani wa Bongolalaland.

Sababu nyingine inayomfanya Mpayukaji kwenda huko Ugabacholini ni kwenda kuangalia miradi inayoweza kuwa imefichwa kule na wezi wenye maulaji wanaoweza ima kwenda kwenye mahospitali yao au kusuka dili ya kuingiza midawa ya hovyo kama ambayo mamlaka ya midawa inavyolalamikia kutamalaki kwa midawa fweki ambayo mingi inatoka kule na kule kwa Wala kila kitu wa kwa mzee Mao Zedongo.

Kwenda kwa Mpayukaji Ugabacholini ni suto kwa watawala wasiojali masilahi ya kaya zao wakiishia kuzurura na kuficha mifweza nje kama kashafi aliyenyotolewa roho kama kibaka hivi karibuni. Nami nina mpango wa kuwahamasisha walevi na wanywa kahawa tuwanyotoe roho wezi wetu saizi ya Kashafi.

Hata hivyo, mpango wangu wa kwenda kujichunguza afya yangi imayokabiliwa na kuwashwawashwa na ukurutu Ugabacholini haukupita kirahisi. Wanywa kahawa walichachamaa wakidai nakwenda kule kula maraha badala ya kutibiwa kwenye hospitali za hapa.

Mwenzao naumwa kweli. Wao, umaskini wao, walidhani nakwenda kujichana mikuku kule. Kuku gani wawe Ugabacholini iwapo magabacholi wenyewe wanakimbilia Bongolaland wanapokuja mikono mitupu na kuondoka mabilionea kama Chavda? Kule kuna kuku au dhiki tupu na viwanja vya jinai ya kutengeneza ufisadi. Hayo tuyaache kwa leo.

Wapo walioona kama nazusha masahibu ya kutaka kunyotolewa roho ili nipate ujiko na ulinzi wa chee. Waliuliza ni kwanini sikulipoti kwa mandata hasa mkubwa wao yaani PIG. Msisme natukana. Kwa wasiojua kirefu cha PIG ni Police Inspector General na si nguruwe kwa kimombo. Nami niliwajibu kuwa Daktari mwenzangu Mwakiwembe aliporipoti kwa PIG nini kimefanyika zaidi ya kuonekana mzushi hadi yalipomkuta? Nani anajali?

Hata kutoa maelezo hawataki zaidi ya kuahidi kufanya hivyo na kuja na misifa badala ya maelezo. Mwenzenu anaumia nyie mnaleta mashauzi ya kike? Kumbafuni nyote mnaochezea uhai wa wenzenu mkijifanya kuwajali wanapokufa kwa kuwaita mashujaa ambao mapengo yao hayawezi kuzibika wakati mmewazika nyinyi na uovu wenu. Kwani haya hayafanyiki?

Msidhani masihara.

Mwenzenu nawindwa kuuawa ili watu wapate ukuu. Kuna watu wamekwenda hadi urusini na kununua sumu aina polonium ambayo inaua kwa haraka na mateso usiambiwe. Yote haya yanafanyika na hakuna anayejali! Hawa usalama wa Kaya kazi yao nini au kutisha tisha watu na kuchakachua kura za kula? Senzi sana Usalama wa Kaya hamna hata maana. Nyie ni nepi za mafisadi na wauaji mtake mistake. Kumbafuni sana.

Watu wamegeuka wanyama. Yaani pamoja na aibu na mateso yaliyompata Gadhaffu sorry Kashafi bado watu wanatamani madaraka hata kwa kutoa roho za wenzao! Inatisha sana wajameni. Kwa mfano mie na Kijiwe changu tuna nini hadi watu kutaka kuninyotoa roho? Au ni huu ujiko wa shilingi mbili wangu na bi mkubwa kujidai na madaraka ya kijiwe utadhani hayatatutoka siku ikifika?

Nasisitiza. Mie siyo kama Kashafi au M7 na Kaga…malizia. Watu kwa umaskini wa matumbo na vichwa bwana. Kuna nini kwenye kijiwe changu cha ombaomba kila uchao? Kahawa na kashata vya dezo? Mungu naomba uniepushe na makafiri hawa wapenda madaraka hata kama hawana uwezo wa kuyatumia vizuri kama Kashafi. Mtakuja kufanyiwa nchezo mbaya kama Kashafi.

Turejee kwenye mipango ya kutaka kwenda Ugabacholini. Kwanza nikishafika kule, nitahakikisha narejea na siri inayowapeleka kila mtu kule. Je, yawezekana Ugabacholini kunatumika kama kisingizio cha kutoendeleza huduma bora hapa kayani? Kweli yawezekana. Tangu uchumi wa kaya ulipowekwa mikononi mwa kunguru unategemea nini? Mambo yanazidi kuongezeka. Baada ya kuweka uchumi wa kaya na kuridhika na ten percent sasa tunaweka hata afya zetu mikononi mwa magabacholi yarabi. Hili halitakuwa chini ya utawala wangu kama nitafanikiwa kuchaguliwa kuwa mkuu wa kaya piga ua.

Huwa siachi kujiuliza. Kama Kashafi aliweza kutoa elimu bure, wake bure, umeme na makando kando mengine na bado akanyotolewa roho na kufanyiwa vitendo vibaya, ikifika hapa itakuwaje? Hivi hawa wanaofanya madudu wana akili kweli au ni mataahira wasio na hata kumbukumbu? Mwenzenu Kashafi kanyolewa kwanini msitie maji badala ya kuendelea kukenua na kujipa matumaini kama paka kukalia mkia akadhani kakalia bonge la kochi.

Shauri yenu. Mwenzenu naelekea Ugabacholini hivi karibuni ili kufichua siri zenu na kuja hapa na kuwaumbua. Maana sielewi kwanini hata mwenye ugonjwa wa ukurutu anaenda kutibiwa India? Kaeni chonjo Mpayukaji aja.

Acha niwahi eapoti kununua tiketi kwa ajili ya safari yangu ya Ugabacholini.

Chanzo: Tanzania Daima Novemba 2, 2011.

1 comment:

Yasinta Ngonyani said...

Nakutakia safari njema na pia mafanikio mema kwa kila jambo.