Wednesday, 23 November 2011

Hoja ya Kikwete kuhusu katiba ni dhaifu

Hivi karibuni rais Jakaya Kikwete alivunja kimya chake cha muda mrefu ingawa kufanya hivyo, hata hivyo hakukuwa na tija yoyote. Wengi walidhani penye kimya kingi kungekuwa na mshindo kiasi cha Kikwete kuja na angalau jambo moja jipya kuhusiana na hali inayolikabili taifa hasa kuzorota kwa uchimi na kuporomoka kwa sarafu yetu. Akiongea na wazee wa Dar es salaam kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba juu ya hali ya uchumi nchini na mchakato wa Katiba, Rais Kikwete alisema atatia saini sheria ya mchakato wa kuunda katiba mpya ambayo inatokana na muswada uliopitishwa na hivi karibuni baada ya kususiwa na wabunge wa upinzani. Hakutaka kugusia uchumi akijua fika atazidi kujipalia mkaa.

Kikwete alikaririwa akisema: “Siku zote katika mchakato wa Katiba, tume huundwa na Rais, sasa iweje sasa?... Rais amepungukiwa sifa kikatiba?” Haieleweki Kikwete alimaanisha nini aliposema siku zote tume huundwa na rais. Kwani lazima rais afanye kila kitu? Kama watawaliwa wanataka katiba mpya kwanini rais aingilie kati utadhani naye ni mtawaliwa. Inaonekana Kikwete bado anafanya mambo kwa kufuata mazoea na mawazo mgando ya kale; badala ya sheria na alama za nyakati. Kama Kikwete angekuwa mweledi wa sheria na mwenye kusoma alama za nyakati vilivyo, asingejidhalilisha kwa kujitetea na kuonekana kung’ang’ania kuwa lazima rais aunde “tume yake” ya kuandika katiba badala ya kuacha umma ufanye kazi hiyo ambayo ni yake kisheria. Inasikitisha; kwani Kikwete ameshindwa kujiuliza swali rahisi- kama awamu tatu zilizopita ambapo marais waliunda katiba- walifanya nini cha mno iwapo hatuna katiba inayoendana na maslahi ya watanzania- hadi kuhitaji katiba mpya. Laiti Kikwete angeelewa suala rahisi kuwa tumo kwenye mchakato wa kuandika katiba mpya inayoendana na mazingira ya sasa baada ya watangulizi wake kufanya mizengwe kwa kuunda tume ambazo hazikufanya lolote la maana zaidi ya kutafuna pesa ya umma na kupokea maelekezo toka kwa walioziunda ili kulinda maslahi yao ya wakati ule na baadaye. Rejea, kwa mfano, rais mstaafu Benjamin Mkapa kuvunja katiba na kuhujumu nchi lakini akaendelea kulindwa na katiba viraka tunayotaka kuipiga teke. Kama tume husika zilizoundwa na marais waliomtangulia Kikwete zingefanya la maana basi tungekuwa tunapoteza muda, pesa na nafasi kuandika katiba mpya.

Alichopaswa kuelewa Kikwete ni kwamba kutia katiba viraka na kuandika katiba upya ni vitu viwili tofauti. Awamu ya kwanza ilitia katiba viraka ili kuendana na mahitaji ya chama kimoja wakati ule baada ya kuunganisha vyama viwili kuwa kimoja. Awamu ya pili iliweka viraka mara tatu mojawapo ikiwa kuvunja na kuua Azimio la Arusha jambo ambalo limetuletea madhara makubwa kijamii kisiasa na kiuchumi. Maana huu wizi tunaoshuhudia ukihalalishwa, ulizaliwa wakati ule. Hata hawa mafisadi wanaotukoga kila uchao wakiiba kila mahali na kulindwa ni zao la viraka vya awamu ya pili. Hili si jambo la kujivunia kwa rais mwenye nia njema na taifa. Je Kikwete anajivunia hili kutokana naye kuwa mnufaika wa ‘mabadiliko” haya ya katiba yaliyowezesha ujambazi kama EPA kufanyika na wahusika kuendelea kuwa kwenye ofisi za umma?

Tukija kwenye awamu ya tatu, kadhalika hamna la maana lililofanyika baada ya serikali kuja na white paper. Serikali ilifanya hivyo kuogopa mawazo ya wananchi yaliyokinzana nayo.

Kwa wanaojua kanuni za uundaji na uandikwaji wa katiba mpya ni kwamba kinachounda katiba si bunge wala kamati teule ya rais bali mkutano wa katiba au constitutional convention ambao hujumuisha asasi mbali mbali na wadau mbali mbali nchi nzima. TumeonaAfrika Kusini na Kenya zilivyoandika katiba zao kutokana na kongamano la kikatiba la umma na si bunge wala tume ya kufinyangwa jikoni mwa rais. Rais anayeng’ang’ania kuandika katiba licha ya kuwa imla ni mwoga wa kushughulikiwa hapo baadaye. Kama kweli Kikwete ametimiza wajibu wake vilivyo anaogopa nini?

Kisheria, katiba ni mkataba kati ya watawaliwa na watawala na ni mali ya umma. Hata kama mamlaka ya rais ni kuunda tume ya katiba kama anavyotaka Kikwete lakini si kuingilia tume husika kama ambavyo imekuwa ikitendeka hapa nchini.

Hivi Kikwete na magwiji wa katiba na sheria kama Profesa Issa Shivji na Joseph Warioba tumsikilize nani? Je kati ya Kikwete na wananchi nani anapaswa kusikilizwa?

Mwaka 1991 na 1992, alisema iliundwa tume nyingine iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali ya kukusanya maoni ya Katiba ya kutoka mfumo wa chama kimoja kwenda vyama vingi. Ajabu maoni ya tume hayakutekelezwa yote au tume haikufanya kazi vilivyo. Maana tusingeendelea kuwa na katiba ya chama kimoja kwenye mfumo wa vyama vingi. Kikwete alikaririwa akisema “Tume hii ilipendekeza sheria 40 zifutwe, zilifutwa na nyingine zinaendelea kufutwa ikiwemo sheria ya kumweka mtu kizuizini,” Huu ni ushahidi wa usanii wa marais. Maana kama suala ilikuwa ni kufuta sheria 40 za kikandamizaji, basi zingefutwa pale pale siyo kwa mdomdo kama ilivyo sasa hata baada ya kupita miaka zaidi ya kumi. Huu ni ushahidi mwingine kuwa tume zinazoundwa na rais badala ya kongamano la katiba ni upotevu wa muda na fedha na usanii wa kawaida ingawa unafanywa na watu wenye madaraka makubwa.

Ingawa Kikwete ametumia muda mwingi kuwashambulia na kuwatisha CHADEMA, tunawashauri wasikubali kutishwa kwa maslahi ya kikundi kidogo cha watu. Kikwete amegeuka imla kwa kupora haki na stahiki ya wananchi na kujiamria la kufanya kuhusiana na mstakabali wao. Rais yupo na atapita lakini umma hautapita. Utakuwapo siku zote. Kikwete hana jipya kwani anatetea tabia ya kuweka katiba viraka ili kulinda maovu ya watawala. Hivyo, umma unapaswa kumpuuzia na kuhakikisha unapambana kupata katiba mpya itokanayo na umma na si rais na wakwasi wenzake wachache. CHADEMA na upinzani kwa ujumla hakikisha mnasimamia hili. Vinginevyo tutaendelea kuchezewa mahepe na CCM kama ambavyo imefanya kwa miaka zaidi ya 50.
Chanzo: Tanzania Daima Nov. 22, 2011.

1 comment:

Anonymous said...

Word!