Wednesday, 30 November 2011

Mwenye Richmond kafunuliwaBAADA ya kuomboleza kifo cha rafiki, kipenzi na ndugu yangu Ya Mlamali bin Mohammad bin Abdussalaamu bin Humahidi bin Abu Minyaaaar bin Humahid bin Nairal al Fusso Kashafi, sasa umefika wakati wa kusoma hitma yake.

Hivyo wiki hii wanywa kahawa watakunywa kahawa na kula kashata bure ili kumkumbuka mwenzetu.

Hata hivyo katika kumkumbuka ndugu yetu huyu, nitatumia fursa hii kujirekebisha na kurekebisha baadhi ya mambo kuhusiana na ninavyotawala kijiwe. Hivyo, huu utakuwa ni wakati mkubwa wa kutafakari mustakabali wa kijiwe.

Katika kufanya tafakuri jadidi nitafanya baadhi mambo ambayo nataka kila mwanakijiwe ajue.

Mosi, nitakomesha kuendesha kijiwe kama mali ya familia au shamba la bibi. Mke wangu na kitegemezi changu na walamba viatu wote kijiweni nimeishawaambia kuwa nitawavua magamba.

Mie sitaogopa kama wale wanyama wenye magamba wanaoogopa kuvuana magamba. Niseme wazi. Hata gamba liwe nene kiasi gani nitalivua bila woga wala kuzungusha.

Hakuna cha gamba kugomea kiunoni wala urafiki wa chumbani wala barabarani kama wale. Maana nimejifunza kuwa kutawala kwa kutumia ukoo, kujuana, udini, uanachama na kulipana fadhila hauna tija na kama tija ipo si nyingine bali mauti tena ya aibu kama yaliyomkuta rafiki yangu Kashafi ya kuuawa kama kibaka mwizi wa kuku wakati alikuwa mtu mkubwa tu.

Nimeamua vitegemezi vyangu vijitafutie kama nilivyojitafutia badala ya kuniganda mgongoni kama kupe. Mbona vitegemezi vya mzee Mchonga vimejitafutia na vinaheshimika? Hakuna haja ya ukupe bila sababu tena kwa mgongo wa wanywa kahawa.

Hata bi mkubwa nimempa wazi kuwa ukupe mwisho. Niko tayari hata kumtaliki kama hatataka kubadilika na kuachana na ukupe. Mbona bi mkubwa Mary Mchonga anaishi tena kwa heshima? Kwani yeye ni nani aishi kama kupe wakati kupe mwenyewe anategemea damu ya ng’ombe. Bila ng’ombe kupe hana damu. Ng’ombe akiamua kukanyaga na kumsagasaga kupe hana wa kumzuia.

Kitu kingine ambacho nataka kieleweki ni kwamba nitawapuuzia waramba viatu wangu ambao wengi ni vibaka tu wanaonitumia. Maana likibumburuka na siku yangu ikitimia hawatabeba msalaba wangu nami zaidi ya kunigeuka kama akina Jibirili walivyomgeuka Kashafi na sasa kuula wakati wao hao hao ndiyo waliokuwa wakimtukuza na kumwambia uongo asijue walikuwa wakimchuuza.

Hapa kina Ewassa wangu na Endelea Chenga nasema mlie na mliwe tu. Lazima niwavua magamba bila kuoneana aibu. Nitatumia staili ya kumuua nyani bila kuwaangalia usoni ili nisiwasamehe. Nasema muelewe. Mie si mwoga wala msanii. Nitafanya kweli potelea mbali liwalo na liwe-lazima magamba yavuliwe hata kama ni kwa kuchana ngozi ya mtu.

Na katika hili sitaitisha vikao vya woga na upotezaji pesa za umma wa wanywa kahawa. Nitaamka kama chizi nakwenda kijiweni na kutangaza kuwa fulani na fulani na fulani na fulani nimewatimua uanachama wa kijiwe. Finish. Nisikie mtu akifanya fyoko atajua kama kahawa ni mma au maji.

Kitu kingine ambacho nimejifunza toka kwa Kashafi ni kuishi kwa kujilisha pepo na kupuuzia ukweli nisijue hautanipuuzia wala kunisamehe. Avumaye baharini papa nimegundua.

Nikiendelea kujilisha pepo wakati wanywa kahawa wakizidi kuishi kwa upepo kama magurudumu ya gari na baiskeli wataninyotoa roho siku moja tena kama kibaka. Aku! Singoji yanikute kama Kashafi mie.

Kitu kingine ninachoapa kuachana nacho ni usanii na ubabe. Hauna tija zaidi ya kuwafundisha wanywa kahawa ubabe halafu wanigeuzie kibao kama alivyofanyiwa Kashafi.

Kitu kingine ambacho nimejifunza toka kwa Kashafi na ninakitafakari kwenye hitma yake ni ukweli kuwa kila chenye mwanzo shurti kiwe na mwisho. Isitoshe, nimegundua kuwa unaweza kuwafanya watawaliwa mafala nao wakazuga kwa kujifanya mafala kumbe wanapanga kukunyotoa roho tena kinoma kama walivyomfanyia swahiba na ndugu yangu Kashafi.

Singoji yanifike. Heri nionekane mwoga nipone kuliko kujifanya jabali na mbabe nikaishia kunyotolewa roho nikimwaga michozi kama kichanga kama alivyofanya Kashafi.

Juzi nilimsikia mwanae akiongea habari za ki-al-Qaida akisema eti alijeruhiwa na makafiri na si wapendwa wake wa Libya! Kweli za mwizi zikifika-utasikia kila kitu.

Anadhani Walibya ni mafala wa zama zile za dingi wake. Too late dear, those guys are going to send you to the gallows just soon son. Zamu yenu ya kutesa kwishnei bwana mdogo Sefu al Islaaaam.

Kitu kingine nilichojifunza ni kwamba ngurumbili hawatabiriki wala kuaminika. Ni makosa kuwatabiri na kuwaamini kiasi cha kuwafanyia utakavyo ukidhani ni wanyama kumbe wanadeku kila kitu na kukuchora na kukusanifu hasa siku wakikupata.

Kuwa muwazi na mdemokrasia Kung’atuka kama mzee Mchonga ili nising’ang’anie na kuishia kunyotolewa roho kama kibaka.

Tumalizie na kutoa somo kuwa katika hitma hii tumejifunza kuwa kumbe Richmonduli wapo wawili.

Mzee mzima hatimaye amefichuliwa kuwa ndiye kila kitu na kama ni kuvuana magamba basi avuliwe yeye kwanza.

Maana ushahidi wote umemwingiza na kumbana vilivyo. Kwa vile jamaa ni bingwa wa sanaa na wadanganyika ni wapenzi wa sanaa huenda atanusurika. Ila hali ilivyo, enough is enough.

Haiingii akilini kama watanusurika badala ya kukashafiwa tena kwa aibu zaidi ya Kashafi.

Acha niishie nijiandae kwenda Tahrir Square kudai Njaa Kaya na Ewassa na hata Makidamakida wao wawajibishwe kwa kutiwa kitanzini na kuzomewa kuliko hata Kashafi.

Nasikia ving’ora vyake. Acha nianze kuzomea. Hilo, hilo, gamba kuuu, kubwa.

Chanzo:Tanzania Daima Nov. 30, 2011.

No comments: