Wednesday, 30 November 2011

Lowassa kajivua gamba, kamvika mwenye gamba

HAKUNA ubishi kuwa Rais Jakaya Kikwete alipokuja na dhana ya kujivua gamba, alilenga kutua mizigo ambayo imemwia mizito tangu alipoingia madarakani.
Kwa mawazo yake, alidhani mizigo hiyo ni swahiba wake, Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge. Lakini kwa kadiri Rais Kikwete alivyoutega mtego wake, umemnasa hata kabla wale aliowalenga hawajanaswa.

Wakati Kikwete akiandaa mtego alisahau kitu kimoja. Alisahau kuwa alioutega kwenye njia moja hiyo hiyo ambayo alitaka kupitia kurejea salama nyumbani.

Je, angeleaje nyumbani kupitia njia hiyo hiyo asiutegeu mtego au asinaswe nao? Sasa si siri.

Lowassa amemvisha gamba Rais Kikwete kiasi cha kushindwa kuelewa gamba ni nani na nani si gamba. Ingawa Lowassa amejitetea kuhusiana na Richmond, bado hawezi kukwepa kunaswa na mtego wa marehemu baba wa taifa.

Kwa wanaofuatilia hali ya mambo na jeuri ya akina Richmond hadi walipojibadili jina na kuitwa Dowans, wamepata siri ya jeuri yao. Kwa maneno ya Lowassa, hakuna shaka yoyote Richmond-Dowans ni Kikwete.

Hebu tunukuu baadhi ya maneno yake. “Mwenyekiti utakumbuka kwamba mimi nilishaamua kuvunja mkataba wa Richmond mapema, lakini baada ya kukupigia simu ukiwa katika safari nje ya nchi ulisema tusubiri, kwani ulikuwa umepata ushauri wa makatibu wakuu wa wizara, sasa leo hii ninahukumiwa nakuitwa fisadi kwanini?”

Je, Rais Kikwete aliingilia mchakato mzima bila faida binafsi? Je, anayevunja kanuni na kuvuruga utawala wa sheria anafaa kuendelea kuongoza nchi ambayo kimsingi anaikwamishwa kwa sababu zake binafsi?

Hapa hakuna shaka kuwa kitendo cha Rais Kikwete kumzuia Lowassa kuvunja mkataba kililenga kulinda masilahi fulani ya rais ambayo hata hivyo hayatajwi kwenye utetezi huu jadidi wa Lowassa.

Je, tujiulize swali moja, kwanini utetezi huu haukutolewa mapema? Jibu analitoa Lowassa kuonyesha kuwa la Rais Kikwete na Lowassa ni moja.

Anasema, “Nilijiuzulu kuwajibika kwa ajili ya kuilinda serikali yangu na kwa heshima ya chama changu, sasa kwanini leo nahukumiwa kwa jambo hili, tena natukanwa na wana CCM wenzangu na si wapinzani nchi nzima kwamba mimi eti fisadi?”

Kwa jinsi Lowassa alivyoyapanga maneno yake, kwanza anataka aonewe huruma kama mbuzi wa shughuli tuseme alitolewa kafara.

Pili, anataka kumkumbusha Kikwete kuwa asingejitoa kuubeba msalaba wake naye Rais Kikwete kwa pamoja wote wangekuwa msalabani.

Pia ni taarifa kwa Rais Kikwete wakati wake naye kubeba msalaba wa Lowassa ni huu. Na kweli, Lowassa amefanikiwa kuzima harakati na shinikizo la kuvuliwa nyadhifa zake na kuadhirika.

Laiti Rostam Aziz asingefanya papara, naye angegoma. Maana mgomo na ushawishi na siri vya Lowassa havikumwokoa peke yake bali hata mwenzake Chenge.

Kimsingi, hoja ya Lowassa ina mashiko kuwa magamba ndani ya CCM si mawili wala matatu bali wote. Hali inakuwa mbaya zaidi gamba kuu linapokuwa rais na mwenyekiti wa CCM ambaye kwa kiasi fulani anaweza kuonekana mnafiki kuanzisha harakati hii bila kujua kuwa naye ni sehemu ya gamba tena nene kuliko yote.

Kimsingi, Lowassa amefanikiwa kuvua gamba lake na kumvisha mwenye gamba. Tumesema. Lakini hatukusikilizwa.

Kitu kingine ambacho Lowassa amefanya ni kuthibitisha ukweli wa madai ya Dk. Willibrod Slaa, Katibu Mkuu wa CHADEMA aliyetoa orodha ya mafisadi kule Mwembe Yanga ikiongozwa na Rais Kikwete mwenyewe.

Rais Kikwete alijitahidi kutojibu tuhuma za Dk. Slaa akidhani zitajifia na kuwang’ang’ania wenzake, asijue ikifika siku ya kifo kila mtu atapambana kuokoa nafsi yake kama alivyofanya Lowassa.

Hivyo tuhitimishe kwa kusema kuwa mchawi aliyekuwa akitafutwa na CCM kumbe ni mwenyekiti wao! Je, Rais Kikwete ameelewa amedhalilika kiasi gani kwa kuwahadaa watu wake kuwa anaweza kupambana na ufisadi wakati yeye pia ni kati ya watuhumiwa wa ufisadi huo huo?

Tumalizie kwa maneno mengine ya Lowassa. Anasema, “Mwenyekiti nikukumbushe mwaka 1997 kule Zanzibar, kina mzee Daudi Mwakawago walikuja na mafaili yakiwa na tuhuma dhidi ya mtizamo hasi wa jamii dhidi yako, kwa hiyo wakati ule kama si busara za kina mzee Mkapa (Benjamin) leo usingekuwa hapo ulipo.”

Kauli hii ina ujumbe mahususi kuwa Rais Kikwete asijisahau. Pili, ni kumkumbusha kuwa, licha ya kuchafuka kiasi cha kutotamanika, bado ana rungu la urais ambalo anaweza kutumia kumwokoa Lowassa ili aweze kuendelea na mbio zake za kuusaka urais mwaka 2015.

Ukweli huu umo kwenye maneno haya ya Lowassa, “Mwenyekiti nikukumbushe jambo jingine, kule Zanzibar mwaka 1997 walipoleta tuhuma za mtizamo wa umma dhidi yako, ulisema kwamba kuwa rais ni mipango ya Mungu.”

Wengi wanangojea kuona kitu gani kingine atafanya Kikwete kuepuka aibu hii. Pia hapa ndipo siri ya kuenguliwa kwa spika wa zamani na Waziri wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta inapojulikana.

Maana, kimsingi, Bunge ilipaswa likae na kuangalia kashfa ya Richmond upya pamoja na ukweli kuwa rais na Lowassa (waziri) mkuu licha ya kulidanganya Bunge na taifa, walificha ukweli kwa faida zao binafsi.

Hakika, huu ni mtihani mwingine kwa Spika wa sasa Anne Makinda na tuhuma kuwa alipachikwa pale kufua nguo chafu za serikali. Ajabu ya maajabu, bado magamba haya yanawafuatafuata kina Sitta kutaka kuwaadhibu pale ambapo wanapaswa kuadhibiwa wao.

Je, wabunge wetu nao watakubali kugeuzwa nepi za vigogo Ikulu? Pia kuna haja ya kuangalia upya hata haya malipo ya Dowans bin Richmond. Maana kutokana na shutuma hizi mpya ni kwamba anayelipwa ni mwenzetu na watu wake na ndiyo maana hataki kutetea wananchi dhidi ya ujambazi huu wa mchana.

Hakika Kikwete naye tuseme ni gamba. Anapaswa kujiwajibisha au kuwajibishwa mara moja kutokana na tuhuma hizo.

Hapa ndipo upinzani unapopaswa kuachana na majadiliano na kuingia mitaani ili haki itendeke - kieleweke. Kazi kwetu.

Chanzo: Tanzania Daima Nov. 30, 2011.

No comments: