Mwenzenu nawahabarisha lakini uhai wangu umo hatarini sana. You know what? Si wanakijiwe wamenitolea uvivu na kuniita msukule! Wanadai mimi sina maana wala sababu ya kuendelea kuwa mkuu wao. Kilichonisibu ni vigumu kuelezea hasa baada ya kugundua kuwa walevi wameanza kuzinduka kwenye ulevi na usingizi niliokuwa nikitumia kuwaibia. Sikujua kuwa kumbe walevi nao wana kumbukumbu! Maana, walivyoanza kunizodoa kwa kunipa historia ya jinsi nilivyochaguliwa kwa kishindo cha Tsunami na seiche- (sauti kuu ya Tsunami kwa wale wasiojua seiche). Walinirejesha mwaka 2005 wakati wa uchaguzi ulioniingiza kwenye ulaji wa kijiwe. Walinikumbusha jinsi nilivyoaahidi manywaji na matafunaji ya kahawa na kashata na kunenepeana kama kiti moto au shosti wa kimakonde yule mke wa jamaa yangu anayenenepa kiasi cha kutaka kujaa kwenye ramani ya kaya.
Bado nayakumbuka maneno ya msomi. Alisema, “Nilikuwapo kwenyekampeni ya Mkiti Mpayukaji. Huu ulikuwa ni wakati wa walevi kutwishwa mkenge uliokuwa umetengenezwa na vyombo vya habari vya uchochoron na udaku hasa vya umbea. Vilichonga msukule wetu na kuupa kila aina ya sifa kiasi cha walevi kuuingia mkenge na kuuchagua msukule.” Nilimkata jicho nusu limtoboe ili aache kuniita majina ya ajabu kana kwamba mie ni marehemu.
Yeye hakujali. Aliendelea: “You know what; this msukule did all his flim flams and ended up becoming CEO of walevi.” Mzee Maneno alimkumbusha kwa kuvunja kanuni ya maazimio ya kijiwe. Alisema: “Kimbombo hicho kaka! Hukumbuki tulivyoazimia wiki jana kususia lugha hii hadi jamaa watuombe msamaha?”
Msomi alijitetea haraka na kusema, “Sorry jamani.Lololo! Nimerudia yale yale kama jamaa wa mjengoni wanaobangaiza kimombo na shahada zao za kughushi!”
Alikohoa kidogo na kutupa kipisi chake cha sigara kali na kuendelea: “Samahani jamani. Nilimkumbuka Prince Charles kiasi cha kujikuta naongea kimombo nisijue tumeamua kukisusa hadi watuombe msamaha kwa kutaka kutulazimisha kupitisha sharia za kushikishana ukuta. Si wakawaambie wamanga ambao ni mabingwa wa kamchezo haka au wataliano?”
Kabla ya kumaliza Mbwamwitu alichomekea: “Msikonde wazee. Mei nina mpango wa kwenda kukutana na mama Chazi ili aniombe msamaha kwa niaba yenu au siyo?” Kijiwe hakina mbavu hasa kwa jinsi anavyomtaja mama utadhani ni rahisi kumkaribia kwini! Utani mwingine bwana!
Kuona hivyo Mgosi Machungi alikula mic na kuzoza: “Tinapaswa kurejea kwenye mada ya leo ambayo ni kujadili msukue uliotiingiza mkenge na sasa kuendelea kutitesa bila kutipa kahawa na kashata ulizotuahidi.” Nilimkata jicho Mgosi Machungi hasa nikizingatia kuwa ndiye alikuwa mpamba wangu ambaye alikwenda kuwahonga akina shangingi la Kinshomile Silvia Rweyema, sorry, Rwependekeza kuniandika vizuri.
Baada ya kuona hata wale niliokuwa nikila nao kwa muda mrefu, nilitamani kwenda kwa rafiki yangu Tosh na kuomba aniazime vijana wake wa gesi la kuanzisha fujo liitwalo Fanya Fyoko Ubondwe (FFU) ili liwatie adabu wanywa kahawa kama linavyowafanyia matching guys wanaopinga lisirikali kuwafukuza ili wapishe wale wa kichainizi na kigabacholi. Nilitamani niende mara moja ili wanachopata matching guys wanaoambiwa watafute kwao pa kwenda na kuwaacha wageni wa wateule wanaokula nao kiwapate wanywa kahawa ambao wanaanza kuzibuka kama matching guys na kunikosea adabu kama wanavyokosewa adabu na wale waliowahadaa wakawapa kura za kula.
Nilipokuwa nawaza ni njia gani ya kujinasua na kuhakikisha viherehere wanatia adabu si Mpemba akazidisha maudhi. Alisema: “Si Pemba zama zile kabla ya kufunga ndoa na wabaya wetu tulikuwa na maruhani yakhe. Lakini baada ya maalimu kupata ulaji walahi maruhani yote yametoweka na twaishie raha mstarehe.”
Akiwa anajiandaa kuendelea Mchunguliaji aliingilia kati na kukwanyua mic: “Ami unataka kumdanganya nani? Sema madevu wenu alipowekwa kimada na mafisiahadi kwa kumpa makombo akatulia nanyi mkaingizwa mkenge kama wa Msukule wetu.”
Kabla ya kuendelea nilimuonya. “Mchunguliaji nakuheshimu sana. Chunga ulimi wako ohooooo!” nilimpiga mkwara nisijue kuwa kumbe Mpemba alikuwa na bomu lake!
Maana alikwanyua mic tena na kunena: “Wajua? Heri sie tulipata lau hicho kipande cha ukubwa kuliko huu msukule unokula peke yake nasi tusiambulie hata hicho kipande.”
Nami sikujivunga. Nilizidi kutetea meli yangu isizame. “Msinilaumu bali mjilaumu kwa kuingizwa mkenge. Jilaumuni kwa kupenda hongo. Kwani mie mlinichagua bure? Mara hii mmesahau takrima zangu za kahawa na kashata? Ama kweli hamna adabu wala shukrani.”
Ngonja nitie msisitizo ili mnielewe. Hivi hamkujua kuwa nyie ni watani zangu siyo? Msijeninyotoa roho kama FFU wanavyowanyotoa roho machingas bure.”
Kabla ya kuendelea Msomi aliingilia: Mkiti hatutaki siasa za ki-Njaa Kaya hapa. Ukubali umeshindwa.”
Nami kujiokoa nadandi pwenti ya Msomi na kusema, “ Ni kweli kaya yenu nanyi mnaliwa. Mijitu inaingia kwenye kaya na kujisonda kwenye mabohari na wale watu wa Taasisi ya Kushamirisha Rushwa wanaambiwa. Wakishapata dili wanakwenda kuwatoa upepo na kaya inazidi kujaa mivamizi hadi mjengoni!”
Najifanya hamnazo na kuongea bila kituo: “Mjengoni nako wameishiwa tangu aingie yule mama. Badala ya kujadili maslahi ya walevi wanaonyesha ulevi na ujuha wao! Waulize wadharaulika. Tangu wajifungie mjengoni zaidi ya kulipana marupurupu na posho za makalio wamefanya nini cha maana? FFU inaendelea kunyotoa roho wanywa kahawa wanaoitwa wamachinga wa mawazo na hakuna jamaa wa mjengoni anayelaumu ukiachia wale jamaa wa upingaji ambao wametimiza wajibu wao ingawa wanazidiwa na inzi wa kijani waliojazana huko kutokana na uchafu uliozagaa kila mahali. Yale mainzi yamechana kama malkia wao ambaye amechana kiasi cha kutaka kupasuka!”
Loh! Kumbe kweli nimemix! Basi washikaji mezeeni ilmradi message sent. Ngoja niwahi zangu Idodomya kuona mafisadi wanavyotimuana. See ya guys.
Chanzo:Tanzania Daima Nov. 23, 2011
No comments:
Post a Comment