How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 16 November 2011

Ubadhirifu umechukua nafasi ya uadilifu

TULIPOPATA uhuru mwaka 1961 Watanzania wengi walijenga matumaini kuwa tutasonga mbele na kuondokana na matatizo tuliyokuwa tukikabiliwa nayo.

Mara nyingi, watu waliamini kuwa matatizo kama vile ujinga, umaskini, dhuluma na Maradhi vilikuwa vikisababishwa na utawala wa kikoloni. Hivyo ujio wa utawala wa watu weusi wenyewe ulileta matumaini ingawa hayakudumu kwa muda mrefu.

Serikali ya awamu ya kwanza ilijitahidi kupambana kero tajwa hapo juu chini ya dhana ya maadui wakuu wanne wa taifa.

Mwalimu Julius Nyerere, kwa uadilifu na juhudi vya hali ya juu alipambana na vitu hivi kwa dhati. Mwaka 1976 alitangaza Azimio la Arusha ili kuweza kupata mtaji wa kupambana na maadui wetu wakuu wanne.

Alianzisha Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kutaifisha shule zilizokuwa zikiendeshwa na madhehebu ya dini ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu tena bure. Alijenga hospitali na kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapatikana bure na kuwafikia Watanzania.

Kwa kiasi kikubwa alifanikiwa ikizingatiwa kuwa idadi ya wasomi iliongezeka kiasi cha nchi kuanza kujitosheleza kwa wasomi.

Wakati mwalimu Nyerere akihangaika kupambana na maadui wakuu wanne alikabiliwa na vikwazo kutoka kwa wakoloni wa zamani na mataifa ya kibepari. Lakini hakukata tamaa.

Alifanya alichoweza hadi alipong'atuka mwaka 1985 baada ya kugundua kuwa mambo yalikuwa hayaendi kama alivyotegemea. Kimsingi, mwalimu alituachia mtaji hasa raslimali ambazo alizilinda kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Kwa kumbukumbu ni kwamba chini ya Mwalimu, dhahabu tunayochimba na kuuza kwa tani haikuwa imeguswa.

Baada ya mwalimu kuondoka na kuja serikali za shaghalabaghala za ruksa na upuuzi mwingine, ombwe na utapiamlo wa mawazo na sera viliibuka.

Kulianza kuzuka matajiri wa kulala maskini na kuamka wakwasi. Ajabu hakuna aliyeuliza wala kustuka isipokuwa mwalimu aliyehimiza watu kufuata maadili badala ya madili kama ilivyokuja kuzoeleka.

Taratibu taifa letu liliwekwa rehani kwenye mikono ya wezi wa kimataifa walioshirikiana na wale wa nyumbani. Ghafla Watanzania wakajikuta wapweke na wakiwa wasio na wa kuwatetea hasa pale Mwalimu alipoaga dunia.

Taratibu siasa zilianza kutegemea mfuko na uongo wa mtu badala ya sifa na uadilifu. Ubadhilifu ulichukua nafasi ya uadilifu na jinai zikaanza kuhalalishwa chini ya dhana mbali mbali kama vile kukuza uchumi, ubinafsishaji na kasi na ari mpya na mambo mengine kama hayo.

Badala ya wahusika kujenga taifa, walianza kulibomoa kwa kasi ya ajabu kiasi cha taifa letu kuzidi kuwa tegemezi huku uchumi ukiwekwa kwenye mikono ya genge la watu wachache.

Rejea kauli ya aliyekuwa waziri wa viwanda Idd Simba kuwa uchumi wa Tanzania ulikuwa kwenye mikono ya Wahindi wasiozidi kumi. Bahati mbaya tena, Simba alipotoa kauli hii hakuna aliyeshtuka.

Tulianza kuwaona matajiri wakijazana Ikulu hadi mwalimu akaonya kuwa Ikulu ni mahali patakatifu pa patakatifu na si pango la wezi. Nani angemsikiliza wakati alishawapa madaraka?

Mara watawala wakaanza kuuza kila kitu kuanzia rasilimali hadi utu wa watanzania. Ibada za mali na vitu zilianza kushamiri huku uchumia tumbo na utapeli vikahalalishwa kama njia halali za kuupata utajiri.

Mara tukaanza kuona ujio wa marais wadogo watokanao na ukoo wa rais aliyeko madarakani. Mambo yalizidi kuharibika kiasi cha nchi kuwa kama shamba la bibi hadi wafadhili kutuwekea masharti ya kipumbavu kama vile kuridhia ushoga ili tupewe makombo.

Je, hali ikoje? Taifa letu ni kama liko likizoni kiasi cha kila tapeli ajae kuchuma na kuondoka. Rejea wizi kama ule wa Chavda, EPA, Richmond, Dowans, Meremeta, Tangold na mwingine mwingi. Nani anajali iwapo anapata chake cha juu? Je namna hii tutafika au tutalikoroga kama wasemavyo Waswahili kiasi cha kujimbika bila jembe na pakawa hapatoshi? Je, ni kwanini haya hayajatokea?

Sababu kubwa ni utapiamlo wa wananchi kuishi kwa matumaini yasiyokuwepo. Tutoe mifano, ni wapi na lini uliwahi kuona nchi ikikaa kizani kwa zaidi ya mwaka na vurugu za kudai haki hii muhimu zisitokee? Bila shaka ni Tanzania.

Ni wapi sarafu ya nchi iliporomoka kama inaharisha huku gharama za maisha zikipanda na waongo fulani wakaendelea kuhubiri amani waipatayo na kuwawezesha kuhujumu? Bila shaka ni Tanzania pekee.

Ni wapi ambapo watu waliosoma bure walipata madaraka na kuchezea rasilimali za umma huku wakiwauzia watoto wa wananchi waliopigania uhuru na kujenga taifa wanalobomoa kwa kasi ya vichaa na vurugu za kutaka hujuma hii isiendelee zisitokee? Ni Tanzania.

Tanzania Tanzania kila upuuzi na wananchi wanaona na kunyamaza huku wakiishi maisha ya udokozi na jinai nyingine ili bora liende.

Taifa la bora liende ni taifa lenye ombwe na utapiamlo wa kila kitu cha maana.

Wapo wanaosema kuwa taifa letu limechakachuliwa. Karibu kila kitu kimechakachuliwa. Ukweli umechakachuliwa na uongo kuchukua nafasi yake.

Huduma zimechakachuliwa kiasi cha walaji wetu kulishwa uchafu na sumu badala ya huduma. Mfano mdogo ni ulanguzi wa simu ambapo taarifa za hivi karibuni zimeonyesha kuwa ni Tanzania pekee katika Afrika Mashariki kiasi cha kuwalazimisha watanzania waishio nje kupitishia simu zao nchi za jirani hasa Kenya.

Bahati mbaya kuonyesha ombwe na utapiamlo wa sera na mawazo, hili liliporipotiwa si serikali wala mamlaka husika zilitoa maelezo yenye mashiko zaidi ya kunyamaza ama kutupiana mpira.

Kama hamuwezi kutolea maelezo kero za wananchi mnafanya nini madarakani? Kibaya zaidi ni kwamba Watanzania badala ya kukabili matatizo yao ya kutengenezwa na kundi la wezi wachache, wameamua kutumia njia za panya kuendelea kuishi kwa kubangaiza na kusukuma siku.

Mtaishi lini iwapo kila uchao hali inazidi kuwa mbaya? Je, kuna mjomba atakayekuja kuwapigania zaidi ya nyinyi wenyewe?

Ajabu kila siku tunaambiwa kuwa nchi yetu ni shamba la bibi lakini hatuchukii na kuchukua hatua. Badala yake tunanyamaza au kuchekelea. Je, nani alituroga hadi kuwa wa hovyo kiasi hiki na kutendewa mambo ya hovyo na tusichukie. Msemo wangu maarufu ni tuguswe wapi tushituke?

Chanzo: Tanzania Daima Novemba 15, 2011.

No comments: