Monday, 28 November 2011

Mlevi akata rufaa kwa papaBarua kwa mheshimiwa sana papa Benedicto wa 16,
Kwanza nakusalimia kwa jina la Yesu. Naamini hujambo pamoja na watu wako hapo Vatikano. Wenzako huku Uwanja wa Fisi na Bongo kwa ujumla hatuna hali hata hivyo gongo tunapata ingawa polisi wanatusumbua kwa kututoa upepo. Mambo yamezidi kutubana kama mikanda huku wanaotwambia tufunge mikanda wakifungua hata zipu. Wanaitana magamba, mafisi, mafisiahadi na majina mengine ya ajabu ajabu.

Kabla ya kukueleza kilichonisibu na kunisukuma kukuandikia waraka huu, ngoja kwanza nikueleze kuwa mie ni msomi lakini asiye na kazi wala hali bali kujinywea gongo lau nipunguze mateso na mawazo.

Mheshimiwa papa nisamehe. Ngoja kwanza nielezee uzoefu wangu na hali ilivyo kwangu kama kielelezo cha walio wengi katika kiza na mateso yasiyomithalika.

Baada ya kuzisahau na kuzishit shahada zangu nilizopata baada ya kuzisotea siyo kupewa wala kughushi toka chuo kikuu cha Harvard, makufuru yaliyofanywa na kanisa kuu la Kirumi la Mwanza yalinifanya nizikumbuke. Kumbe kila shari ina heri na kila heri yaweza kuwa na shari. Wajua nini? Si nilikuta panya wameishaanza kuzinyea. Kumbe ningechelewa wangeweza hata kutafuna shahada zangu na kuzitumia kutengenezea viota vya kuzaliwa panya wengine. Huu nao ni ufisadi wa mapanya so to speak.

Nasisitiza kuwa sikughushi shahada zangu. Nilizihenyekea kula Harvard na aliyenilipia karo na pesa ya kutanua bia wakati ule na kuotesha kirimba tumbo tena majuu si mwingine ni mzee Mchonga mwenyewe na awamu yake ya kwanza ya kila kitu kwa watanzania. Wakati huo Bongo ilikuwa bongo kweli na siyo Danga ya Nyika kama ilivyo sasa.

Je mheshimiwa sorry ndugu papa unajua kuwa huku Danganyana ya Danganyika kanisa lako limeingia kwenye kashfa ya ajabu? Kashfa yenyewe ni kuanza kuwasafisha mafisadi pale wanapotoa pesa. Kinachoendelea hakina tofauti na kile alichokuwa akikifanya muuza mibaraka wa zama za kiza wa kanisa lako kule Ujerumani aitwaye Johann Tetzel ambaye alisema kuwa kadri sarafu idondokavyo kwenye kishubaka cha kukusanyia pesa mwenye roho ya mwenye dhambi hutoka motoni na kuingia peponi. Nadhani unamkumbuka tapeli huyu ambaye makufuru yake yalichochea watu kama Martin Luther, Menno Simmons, Conrad Grebel, Wycliffe John, Melchior Hoffman, John Hut, Balthazar Hubmeier na wengine kuasi kanisa lako na kuunda madhehebu yaliyogeuka tishio baadaye. Anyways, huko kwenye mambo ya radicals and reformation leo siendi nisije nikakuudhi kama hawa walitenda makufuru huku Mwanza.

Ndugu katika Kristo mheshimiwa Papa,
Kwa niaba ya wanywa kahawa wa Danganyika nakuandika mtukutu sorry mtukufu kuwa hekalu la kanisa lako la Kirumi katika jimbo kuu la Mwanza liligeuzwa kuwa pango la wezi pale lilipomkaribisha Eddie Ewassa ambaye huku huitwa gamba kuu namba mbili eti kulichangishia pesa ya kujenga kanisa jingine. Wajua kanisa lako limeuzwa kwa bei gani? Huwezi kuamini lakini ndiyo ukweli-madafu milioni 200. Najua hujui madafu ambayo si kama Lira. Dola moja ni madafu 1900 kwa bei za kilanguzi ambazo zimeanza kuhalalishwa kutokana na wakubwa kuchota pesa za kigeni zilipo na kuzipitisha mlango wa nyuma kuchuma faida.

Ndugu Papa,
Machukizo haya makuu yaliasisiwa na kufanywa na askofu Rulanchi akisaidiana na wadogo zake katika jimbo lake. Baada ya kufanya makufuru hayo, huwezi kuamini eti alifunga safari kwenda kwenye nchi ya voodoo ulipokuwa kukutana nawe wakati huko nyuma aliacha amechafua hekalu! Najua alipofika huko hakukueleza ukweli. Maana hakujua jinsi umma wa walevi ambavyo ungechukulia haya makufuru ya hekalu la bwana kuchangiwa na wezi huku kanisa lako likiwekwa mifukoni mwa watu wezi waroho na wachafu ambao Rulanchi aliwamwagia sifa ambazo hata hajawahi kukumwagia wewe. Hakuna aliyetegemea kuwa vipande thelathini kama vile alivyopewa Yuda kumsaliti Bwana Yesu vingeweza kutumika tena kipindi hiki cha maendeleo makubwa na utajiri wa kutisha wa kanisa lako tukufu. Inashangaza na kukatisha tamaa hadi wanywa kahawa wameamua kukuandikia waraka. Hii ni baada ya kugundua kuwa mamlaka husika huku zimo kitanda kimoja na mafisi wawalao watu ambao sasa wamejipenyeza kwenye hekalu la Bwana.

Huku Uwanja wa Fisi kwenye kijiwe chetu cha kula gongo nasikia maneno machafu yakipita kila mtaa. Wapo wanaosema eti roho mtakatifu siku hizi amepinduliwa na roho mtakakitu. Wengine wanasema kuwa hekalu la Bwana kwa sasa ni halali kuwa pango la wezi ili mradi watoe mshiko. Wapo wanaosema etiuna mpango wa kuanzisha utaratibu wa ubinafsishaji wa Kanisa ili kuongeza mtaji wa kwendea mbinguni. Hali inatisha. Kama wewe au mdogo wake Porikapu Peng’o hamtamchukulia hatua huyu Rulanchi, msichanganye kujikuta mkivuna magugu badala ya mpunga kwenye shamba la Bwana.

Kwa ufupi habari nilizo nazo ni kwamba kuna waamini wa kanisa lako wengi wanaopanga kujiengua na kujiunga na madhehebu mengine na wengine kujinyonga kama hutamwajibisha Rulanchi na genge lake la mafisadi wa kiroho wanaotumia uroho kama roho mtakatifu wakati ni roho mtakachafu.

Nimalizie kwa kukushauri kuwu umwajibisha yeyote mwenye kuvaa ngozi ya kondoo ili kuwahadaa kondoo wa Bwana. Wengi wanashangaa ni dini gani inayoweza kulala kitanda kimoja na mafisadi? Ningeshauri Vatikano isikubali kurejeshwa kwenye enzi za akina Paul Mackincus yule habithi wa kimarekani aliyechafua benki ya Mungu (Banco Ambrosiano) kwa kushikiana na mafia, “Uomini di fiducia”kama akina Licio Gelli, Michele Sindona, Umberto Ortolani, Roberto Calvi na majambazi wengine waliomuua papa John Paul I (Albino Luciano). Kaka papa, nakuomba usiruhusu akina Edwardo Roberto Calvi Ewassa na Andrea Michele Sindano Chenga wa Danganyika waliteke kanisa.

Kwa vile tulivyoheshimiana na Albino Luciani, nguvu zimeniishia na siwezi kuendelea.

Wabanikiwe walioliuza kanisa kwa mafisadi huku waliolinunua wakilaaniwa milele na milele aaamini.

Chanzo: Dira Novemba, 2011.

No comments: