Wednesday, 14 December 2011

BARUA YA WAZI KWA KIKWETE NA LOWASSA


Waheshimiwa, salamu zenu,
Nitangulize samahani kuwasumbua kutokana na shughuli na yaliyowakuta hivi karibuni hasa kwenye zoezi zima la “kujivua gamba” ambalo hata hivyo halikuvuka zaidi ya kutuna. Maana watani wenu wanasema kuwa badala ya kulivua gamba mmevishana gamba kiasi cha kuchanganyana na kuuchanga nya umma. Wengi hawakuamini kuwa marafiki ambao hawakukutana barabarani wangevuana nguo badala ya gamba kama ambavyo vyombo vya habari vilikuwa vimetangaza.

Haya si maneno yangu; ni ya wengi ninaosikia mitaani, majumbani, kwenye vituo vya daladala, baa hata vijiweni wakisema kuwa kuvuana gamba kumbe kumeishia kwenye kuvuana nguo! Wengi wanasema kuwa hawashangai. Kwani walilitegemea hilo kutokana na kutoka matamshi yanayogongana hasa ikizingatiwa kuwa kila mtu aliweka wasemaji wake kwa chati.

Pia nichukue fursa hii adimu kuwapa pole kwa mfarakano wa mawazo unaoanza kujionyesha kati yenu. Najua hapa wasiojua siri ya siasa kuwa ni mchezo mchafu ambapo hakuna adui au rafiki wa kudumu bali maslahi ya kudumu wamehanikiza kushangaa hili.

Hata hivyo, jambo moja ni dhahiri. Mmetoka mbali na bado mwendako ni mbali hasa legacies zenu hapo baadaye. Good wine needs no bush walisema wazungu. Nanyi mlikuwa mvinyo mzuri kabla ya kuchacha na kuchakachuka kiasi cha kuanza kustukiana. Je tatizo ni nini? Je hamna wasaa wa kukutana kutokana kuwa bize au mnawaongopa wambea wasifichue njama zenu?

Hakuna shaka. Nyinyi ni marafiki na washirika wa muda mrefu mna mengi mliyoshirikiana yawe mazuri mabaya ya wazi na ya kificho. Nakumbuka maneno ya Lowassa kuwa urafiki wenu si wa kukutana barabarani bali mahali fulani tena kupanga mikakati ya kutimiza malengo yenu kwa gharama yoyote bila kujali nani anapinga au kuunga mkono mipango yenu. Hivyo, urafiki huu hauwezi kuvunjwa na wambea au vyombo vya habari wala kuvishana magamba ingawa mnayo tangu enzi za mwalimu. Je nini kimewasibu kiasi cha kuruhusu wambea wa kisiasa wawatenganishe haraka na rahisi vipi? Je ni arobaini ya mwizi au kutimia usemi kuwa kila kilicho na mwanzo sharti kiwa na mwisho? What is the problem?

Kuna maswali ambayo leo ningependa niulize kwa utii na taadhima. Kwanza, kama kumbe hamna ukaribu na siri kiasi hiki, Bwana Kikwete, ni kwanini ulimteua kuwa waziri mkuu wakatiukijua kuwa akizidiwa anaweza kukugeuzia kibao kama alivyofanya hivi karibuni kule Dodoma tena mbele ya vikao ambayo kila jicho la watanzania lilikuwa pale?

Pili, kama jamaa mwenyewe ni gamba kiasi hiki ni kwanini ulimpigia kampeni wakati ukijua kuwa wakati ukifika utamtosa? Una habari kuwa kama asingekung’ang’ania angekuwa historia? Je umekubali kurejesha majeshi au unafanya kile wazungu husema: retreat in order to advance? Je umefanya hivyo baada ya kuona ni zigo zito lisilobebeka au tuseme nanga shingoni mwako? Je alimaanisha nini aliposema kuwa aliachia ulaji kuokoa chama na serikali yake?

Barua hii ni ya watu wawili. Hivyo, tutakuwa tukiuliza mmoja baada ya mwingine. Sasa ni zamu ya bwana Lowassa. Je Bwana Lowassa una uhakika njia uliyotumia ni salama kwako na kwa rafiki yako au ni yale ya kama mbaya mbaya acha wote tukose? Wapo wanaosema kuwa jamaa yako na rafiki yako ni bingwa wa kuvizia na kulipiza visasi kama ilivyotokea kwa akina Samuel Sitta, je umejiandaaje kama hii ni kweli ingawa sisi tunaona kama umbea wa kawaida tu? Je akiamua kutumia shutuma za marehemu baba wa taifa huoni patachimbika bila jembe kutokana ukweli kuwa jamaa anakubalika ingawa alishaondoka zamani?

Nilisahau kusema mapema kuwa mie ni shabiki wenu nyote wawili kufa. Hivyo, siandiki haya ili mniwekee alama ya X halafu mnitumie mifedha kama vyangudoa wa kimaadili na madili wanavyofanya. Nauliza kutokana na mapenzi yangu kwenu hasa nikizingatia kuwa tangu mwaka 1995 nawajua kama mapacha ingawa upacha wenu wakati mwingine hubadilika hasa mnaposhutumiana na kutaka kutoana magamba kabla ya kuvisha hayo magamba.

Bwana Lowassa, je ni kwali kuwa una ndoto ya urais? Je unadhani rafiki yako tena wa chumbani Jakaya anaweza kukusaidia tena iwapo watu wanakusakama na hawakemei ukiachia mbali ukweli kuwa aliwateua wao kwa kazi hiyo maalumu?

Kuna swali jingine ambalo wengi kwenye mabaa na cite kama ile ya Makongoro wamekuwa wakijiuliza: “Kwanini umemgeuka sasa na si wakati wa kushutumiwa na si wakati ule ulipoambiwa upime na kuamua mwenyewe? Halafu kuna swali moja nilitaka kusahau. Nasikia wakikuita waziri mkuu mstaafu, je ni kweli kuwa ulistaafu au uliachia ngazi? Je wanafanya hivyo ili kuepuka umma kujua kuwa ukustaafu halafu kuhoji kama ukustaafu kwanini unalipwa kama mstaafu wakati wewe si mstaafu?

Nimalize kwa kuwauliza wote wawili kama mlivyotajwa hapo juu, je mnaona kuwa mipango yenu ya kukaa madarakani kweli inawezekana hasa wakati huu ambapo mnamalizana wenyewe kwa wenyewe? Je ukweli ni upi, nyote ni Richmonduli au kuna mmoja anampakazia au kumtumia mwenzie? Juzi nilisikia umoja wa vijana ukikoroma kuwa wazee ndiyo wanakwamisha chama chenu. Je nyie bado ni vijana au mmezeeka baada ya 1995?

Nimalizie waraka huu kuzidi kuwahakikishia kuwa nitaendelea kuwaunga mkono katika mabaya na mazuri. Ila naomba kitu kimoja: msome alama za nyakati na mawazo ya watanzania hasa kipindi hiki ambapo wamechoka na usanii. Kwa heshima na taadhima nahitimisha nikiwatakia mapambano mema yak u-survive. Maana tulipofikia hakuna cha rafiki wala nini bali kunusuru sura hata ziwe nzuri au mbaya kiasi gani. Nawatakia mapambano kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya na matokeo mapya.

Chanzo: Tanzania Daima Desemba 14, 2011.

No comments: