Sunday, 18 December 2011

Kafulila asipoacha tamaa na papara atafulia kila aendako


Ingawa kuvuliwa uanachama kwa mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini NCCR-Mageuzi, David Kafulila si haki, kulitarajiwa kutokana na tabia ya mhusika. Kafulila alipoingia kwenye siasa za upinzani alijiwekea malengo makubwa kupita uwezo wake. Kwa wanaokumbuka kilichomtoa CHADEMA, watakubaliana nasi kuwa Kafulila hajatulia.

Bahati mbaya sana kwa Kafulila, anataka kufikia malengo yake kwa njia ya mkato ambayo ni kuanzisha vurugu zisizo na sababu kwenye vyama. Wapo wanaomuona kama mganga njaa na mtu mwenye tamaa. Wengine wanamuona kama Uvuruge wa kawaida wakati wengine wakimshuku kuwa pandikizi la CCM. Yote yawezekana. Je Kafulila atarejea CHADEMA? Je CHADEMA, kwa alivyowachafua, watakuwa dhalili kiasi hiki kumpokea? Je Kafulila yuko tayari kuramba matapishi yake ili angalau apate nyenzo ya kurejea kwenye ulaji? Je Kafulila ni mwanasiasa makini au mleta fujo na mtafuta riziki kwa mgongo wa kisiasa? Je Kafulila atarejesha kiti chake? Je atakwenda CCM?

Kimsingi, pamoja na Kafulila kufukuzwa na mtu mchafu kuliko yeye yaani James Mbatia ambaye anasemekana kuwa pandikizi na kuwadi wa CCM, anapaswa kujiulaumu kwa kutaka kuukata mkono uliokuwa ukimlisha yaani chama. Na hapa ndipo anapoteza umakini na upambanaji aliokuwa akivishwa wakati si mpambanaji kitu. Kama kweli alilia asamehewe na Mbatia tena mbele za watu, basi hana lolote zaidi ya kubangaiza. Kama alikuwa akiamini alichokuwa akisimamia na kupigania, hakupaswa kulialia kama kichanga. Hata hivyo, kutimuliwa kwa Kafulila kuna somo kuwa CHADEMA ni chama makini. Kwani wao hawakumtimua zaidi ya kumvua uongozi kwa faida yake na chama. Bahati mbaya Kafulila hili hakulipata akaamua kufunga virago kumkimbia mjusi na kumkumbatia mamba. Ama kweli wahenga walinena kuwa ngoma ya watoto haikeshi.

Kafulila anapaswa akae ajifue na atulie kama kweli ana ajenda ya maana na yenye mashiko katika siasa zaidi ya kutafuta uheshimiwa ili kuhomola. Wenye akili tieni akilini siasa si lelemama wala nyenzo rahisi ya kutafutia neema miongoni mwa mafisi na mapapa kama ilivyotokea kwa Kafulila. Yetu macho kuona nini kitafuata.

3 comments:

Anonymous said...

Nani kasema wanasiasa wa aina ya kafulila wanamuvuzishwa na agenda? huwa kama zipo basi ni zao na ni undeclared!

,

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mtu unapokuwa huna utashi, ajenda na msimamo basi unageuka mshibisha tumbo tu, mbinafsi, mbishi na LOSER.

Wanasiasa hawa malaya wanaohangaika na kuhamahama kutoka chama kimoja kwenda kingine daima wana matatizo.

Inawezekana Kafulila wa watu Kafulia kweli....
=================>
Mwalimu:

Nilikuwa napita hapa kusema kwamba sasa nimerudi tena rasmi. Tupo pamoja !!!

http://matondo.blogspot.com/2011/12/wanablogu-wenzangu-na-wapenzi-wote-wa.html

NN Mhango said...

Mwalimu Matondo karibu sana na pita tena na tena. Mchango wako unaonyesha unavyochukia uchumia tumbo. We need to tell them bitter truth even when they hate to hear it. Kafulila kwangu hakuwa mwanasiasa bali an accidental one kama rafiki yake Zitto. Tungoje tuone Zitto atatimiza ahadi yake ya kugombea urais 2015 bila chama cha kutaifisha na kudandia.