Wednesday, 21 December 2011

Tubadili jeshi la polisi kabla ya kutupeleka kuzimu

Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la kuwabambikizia kesi waandishi wa habari hasa wale wanaolikosoa jeshi la polisi au kufichua ufisadi na maovu mengine katika jamii ili ima kuwatisha au kuwanyamazisha au kuwasumbua. Jeshi tulilodhani ni letu, taratibu limegeuka kuwa lao na mlinzi na muhimili wa uovu, uonevu, ufisadi hata rushwa.

Mwaka huu tumeshuhudia waandishi wa habari wawili wa gazeti moja wakibambikiziwa kesi zisizo na kichwa wala miguu. Kabla ya hapo, mwandishi mwingine wa habari wa runinga alibambikiziwa kesi kabla ya mahakama kutomkuta na hatia na jeshi la polisi kuishia kuaibika kimya kimya.

Leo tutajaribu kurudusu hali halisi ya jeshi letu la polisi na nini kifanyike ili kulifanya liwe la wananachi badala ya kuendeshwa na kikundi kidogo cha watu kinachojificha nyuma ya madaraka ambayo nayo pia ni ya wananchi. Kwa mtu anayejua ni kiasi gani jeshi la polisi limechafuka na kupoteza imani kwa wananchi, anashangaa mantiki ya kuwepo kwake. Anashangaa hata hao wakubwa zake wanalipwa kwa lipi iwapo wanashindwa kujenga nidhamu na jeshi la kisasa hasa karne ya 21 ambayo imeshuhudia kuanguka kwa utawala mchafu na wa kikale katika nchi mbali mbali ambapo polisi na vyombo vingine vya dola vilikuwa vikitumiwa na kundi dogo la walevi wa madaraka kuwanyanyasa wananchi huku likishindwa kutambua kuwa kama si kodi za wananchi, hakuna cha jeshi la polisi wala watawala vinavyoweza kuishi.

Historia ya jeshi letu tangu kuingia mfumo wa vyama vingi ni chafu na yenye kukera. Tangu 1992 Tanzania ilipolazimishwa kuingia mfumo wa vyama vingi, chama tawala na jeshi la polisi hawakubadilika. Waliendelea na mawazo mgando ya wakati wa utawala wa chama kimoja. Nani mara hii kasahau mwaka 2000 wakati inspekta jenerali wa polisi wa wakati huo aliyestaafu na kuzamishwa na kashfa ya kutembea na mfanyakazi wake wa ndani, Omar Mahita, alipowaambia wanachama wa chama cha wananchi kuwa kama wao ni ngangari yeye na jeshi lake ni ngunguri? Ajabu Mahita alipojigeuza mwanasiasa kinyume na sheria na kanuni za utumishi wa umma, hakuna aliyekuwa na busara wala ujasiri kumuonya hata kumshauri aache kuvunja sheria. Nani angemuonya wakati aliokuwa akiwakingia kifua ni chama tawala? Nani angemkamata iwapo yeye ndiye alikuwa mkuu wa jeshi la polisi?

Baada ya Mahita kujisahau na kujichafua kiasi hicho, wengi walidhani watawala wangejifunza kufikiri na kukomesha mchezo huo. Lakini wapi! Nani mara hii kasahau mauaji ya Arusha ya Januari 5 ambapo watu watatu waliuawa mmojawapo akiwa raia wa Kenya? Mauaji ya watu wasio na hatia hayakuishia kwenye maandamano ya kisiasa. Nani mara hii kasahau mauaji ya jana ya raia asiye na hatia wilayani Kasulu mnamo Agosti 8 ambapo askari polisi walimuua kinyama Festo Andrea tena kwa kumuingiza vijiti kwenye sehemu za siri mbele ya baba yake marehemu? Mauaji ya raia wasio na hatia nchini ni mengi. Nani mara hii kasahau polisi walivyommiminia risasi raia ambaye walikataa kutaja jina huko Runzewe wilayani Bukombe mwezi huo huo wa Agosti alipouawa Andrea? Nani mara hii kasahau mauaji ya raia huko Ubaruku Mbeya wakati wananchi wakipinga kuingia kwenye eneo lao kwa lori lenye uzito zaidi ya unaoruhusiwa ambapo mtu mmoja aliuawa? Mifano hiyo ni tone kwenye bahari ya mauaji ya kinyama yanayofanywa na jeshi la polisi wale wale tunaowalipa mishahara kwa kodi zetu.

Ukiachia mbali mauaji na kushiriki siasa kwa kubeba chama tawala, polisi wetu wanasifika kwa rushwa kiasi cha kuwa taasisi inayoongoza nchini katika rushwa. Kuhusu hili Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) ilitoa taarifa kuwa jeshi la polisi linaongoza kwa rushwa mwaka huu. Taarifa ilisema, “ Inonesha kuwa asilimia 62.7 ya wananchi hao hawana imani na jeshi hilo kwa kuwa halizingatii maadili, huku asilimia 44.6 wakisema kuwa maofisa wa polisi ndiyo vinara wa kupokea rushwa, asilimia 55 walisema kuna uhusiano mzuri kati ya jeshi la polisi na wao katika kuwakatama wahalifu,” Taarifa hii haina utata. Ni ukweli usiopingika kuwa askari wetu licha ya kuwa wauaji ni wala rushwa wakubwa. Kama ingeundwa tume ya kuchunguza mali zao, wao na wafanyakazi wa mamlaka ya mapato na uhamiaji, wanaongoza kwa kuwa matajiri.

Ukiachia mbali kula rushwa, polisi wetu wana sifa moja kubwa chafu ambayo ni kuwabambikizia watu kesi ili ima watoe rushwa au wawakomoe. Ukienda kila mkoa hiki ndicho kilio cha wananchi. Wananchi wanajiuliza. Kama kweli polisi wetu wangetumia akili ya kawaida biashara ya mihadarati, ujambazi ambao umegundulika kuwa unafanywa na baadhi ya polisi ama kwa kukodisha bunduki au kusindikiza mizigo ya wizi, ufisadi, rushwa na madhambi mengine yasingetamalaki kiasi cha kumlazimisha rais kuunda tume.

Ajabu, waandishi wa habari tunapofichua uchafu kama huu tunaandamwa kwa kubambikiziwa kesi ili kututisha, kutunyamazisha hata kutusumbua kama ilivyotokea hivi karibuni kwa waandishi wa habari wa gazeti hili Mhariri mtendaji Absalom Kibanda na mwandishi Samson Mwigamba. Jamani, kwanini polisi hawataki kukubali ukweli kuwa tatizo si wakosoaji bali wao wenyewe? Kilicho wazi ni kwamba waandishi wa habari ni kama nyuki. Ukiua mmoja wanaibuka wengine wengi. Tunatoa taarifa kwa serikali na jeshi lake la polisi kuacha uonevu, ufisadi, rushwa, ubabaishaji na mauaji ya raia wasio na hatia. Madaraka yana mwisho. Hata hao polisi wanaotumika kama nepi kuna siku watastaafu na kuonja adha ambayo wananchi wenzao wanaonja. Nchi hii ni yetu sote kwa sawa.

Tusidanganywe na madaraka ambayo siku zote hulevya. Wako wapi akina Muammar Gaddafi na wapambe wao? Inatisha kuona tunaposherehekea miaka 50 ya uhuru, bado kuna taasisi tena za umma zinatenda madudu ambayo hata mkoloni hakutenda! Nchi huru lazima iwe na jeshi huru lenye kujua na kutenda haki, kulinda wananchi na si watawala, kuwajibika na kuelimika na siyo jeshi la maguvu na unyanyasaji kama tulivyoonyesha hapo juu. Kama watabishia hili tutakuja na ushahidi mwingine zaidi. Je wahusika wanataka tuanze kuwaripoti Human Rights Watch ndipo wajue wanafanya madudu?
Tumalizie kwa kushauri: tubadili jeshi la polisi kabla ya kutupeleka kuzimu.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 21, 2011.

1 comment:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Kama waandishi wa habari - watu ambao nadhani wanazijua haki zao za kikatiba wanafanyiwa hivi, vipi wananchi wa vijijini wasiojua kitu?