How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 27 December 2011

Helikopta za uokozi hatuna, za kuchungulia waathirika zipo

MWENZENU nina uchungu sana kutokana na mazonge yaliyomkuta mwenzetu mwanakijiwe maarufu mzee mheshimiwa Mgosi Machungi Makambale ambaye ni rafiki mkubwa wa mwenyekiti na rais wa kijiwe alhaji Mpayukaji Msemahovyo mjukukuu wa mtume Waambie yamemfika makubwa.

Si alikumba na zahama ya mafuriko yaliyofurisha jiji la Bandar Salaam ambayo imegeuka Bandar furika kutokana na miundo mbinu ya kishikaji na sheria zinazofuata kura badala ya sheria. Kwa sasa kama siyo kufukuzia riziki hapa kijiweni, Mgosi alipaswa kufikiria kurejea kwao ima Vuga Mashindei au Mtibwa.

Nakumbuka, siku hiyo ambapo mafuriko yalifurisha jiji la Bongo, nilikuwa nimetoka kukutana Mgosi kijiweni.

Tulikuwa tumejadili zahama iliyokuwa imemkuta mchumia tumbo Kafulia na kuandaa mikakati ya kutumia kanuni hizi za chama kuwatia adabu wote wanaoleta mdomo kutaka kuingilia ulaji wetu kijiweni.

Nadhani kwa yaliyomkuta Kafulia baada ya kufulia na kufuliwa, akina Edhard Ruwasha, Sam Sixx, Endelea Chenga na wengine wanaotaka kupimana msuli nami watashika adabu na kutulia kama watoto wazuri kabla hawajanyolewa bila maji.

Mie sitajali kuwa watatoboa siri zangu wala nini. Nitawavua uwanachama. Ingawa alichofanyiwa Kafulia ni kitu mbaya, ni somo kwa jamaa wa magamba wanaoshindwa kuvuana magamba.

Na kama siyo ushikaji na ushirika wa mkuu, Chama Cha Magamba ni hodari wa kutumia karata hizi na zana za maangamizi ya wajivuni na mafisadi. Mambo ya Kafulia na alivyofulia tuyaache.

Baada ya kupokea taarifa toka radioni baada ya mitandao hii ya kishikaji ambapo wawekezaji wanakula na wakubwa na kuweka mimashine mibovu kugoma, niliamua kutumia radio kupata habari kuhusiana na nakama hii. Nilianza kupata wasi wasi na jamaa zangu waliokuwa nje ya nyumba zao kutokana na mibarabara yetu inayojengwa na washirika na washikaji wa mafisadi kubomoka hovyo kutokana na kutokidhi viwango.

Kwanza nilianza kumlaumu Machungi kwa kupanga mabondeni ilhali akijua matokeo yake hata kama kodi alidhani ni nafuu asijue mafuriko yataifanya iwe aghali. Baada ya kufikiri kwa muda mrefu niliachana na lawama baada ya kugundua kuwa na lisirikali lililowanyamazia wakajenga na kuwapa umeme huku likikusanya kodi ya pango nalo ni la kulaumiwa.

Baada ya kuona lawama zangu hazisaidii, niliamua kuomba lau dua ili Mgosi Machungi na mshirika wake wa bedroom, kuku, paka hata panya wapone. Maana sikuwa na jinsi ya kumsaidia wakati ule hasa ikizingatiwa kuwa wagawaji wa kiza walikuwa wamepata sababu ya kuendelea kutukatia umeme.

Nikiwa natafuta jinsi ya kuondoa ngoa niliyokuwa nimeipata kutokana na wenye madaraka kuyatumia vibaya nilijisuta na kuachana na lawama. Maana nilisikia sauti ndani yangu ikisema: Kama si kukiibia kijiwe na kujenga hekalu lako Msa… sorry sana. Sitaji maana majambazi na wachawi wanaweza kunivamia na kuninyotoa roho bure. This is a national top secret after Kagoda and Dowans… nawe si ungekuwa kwenye msambwe kama Mgosi Machungi?

Hivyo niliachana na lawama na kuanza kupanga mikakati ya kutumia janga hili kupata ulaji. Maana kwa kaya za wezi na mafisadi, kila kinachotokea hatukiangalii kwa kuzuia kisitokee huko baadaye wala kujifunza bali kutafuta jinsi ya kuwashawishi wafadhili wamwage mipesa nasi tujifaidie. Upo hapo mshirika? Mezea basi.

Kutesa kwa zamu. Huna haja ya kuwa na nkungukwa. Siku yako ikifika utatesa. Au siyo?

Najua wasomaji walioathirika na mafuriko kwa sasa wananiona kama nawachuria na kuwakoga. Hapana ila bado niseme. Siwezi kuogopa kuuona ukweli hata kama mchungu. You know what?

Hivi unapojenga bondeni kwa kusingizia umaskini unategemea nini hasa usawa huu ambapo kwa mfano hakuna helikopta za kuokoa isipokuwa za kuwachungulia waathirika? Unajenga ukitegemea nini iwapo kuna polisi wengi wa kutwanga watu virungu na wanajeshi wa kuonyesha gwaride lakini si wa uokozi? Shauri yako! Use your bloody brain madala ya kufikiri kwa makario. Hayo ni mambo ya Masumburi, si mimi

Najua masahibu ya umaskini hasa kwa wale wasio na nafasi ya kula bure na kuhomola kama mimi na wapambe zangu.

Najua wengi wajiuliza mantiki ya kuwa Meya hasa yule anayetumia ‘makalio kufikiri’ ambaye siku zote anafukuzia ulaji badala ya kutoa huduma na kutimiza majukumu yake.

Anayesema hivi si mimi. Maana baada ya mitandao feki kurejea angani na kupata fursa ya kuwasiliana na mgosi Machungi kitu cha kwanza nilichosikia ilikuwa ni lawama.

Alisema, “Meya hatikumuona, mbunge hatikumuona. Kwani makosa ya kuishi bondeni yetu peke yetu. Shi ni wao waliotufumbia macho tukaendeea kuishi Jangwani?”

Aliendelea, najua sasa mibaka inaandaa mipango ya kuvuna misaada huku vibaka nao wakitihangaisha kana kwamba hakuna siikai.”
Ingawa sikupenda lugha ya matusi kwa watu wakubwa kama mimi, malalamiko ya Mgosi yalinifumbua macho kuanzisha mfuko wa kuchangia waathirika wa mafuriko ili mimi na bi mkubwa wangu na watu wetu tuvune fweza.

Maana kufa kufaana ati. Hivyo, wewe unayesoma unabii changia mfuko wa wahanga wa mafuriko kupitia akaunti AA 1277890005JK777 TZ000 iliyofunguliwa kwenye benki ya Bank of Tufaane. Onyo, mchango wako unapaswa kuanzia madafu laki moja ili kuonyesha uchungu kwa kaya yako.

Hebu tuache mambo ya ulaji. Mgosi amepoteza magodoro mawili, simu mbili za kiganja, kuku wanne na mkataba wa upangaji huko apangako Luhanga mwisho. Ni mali nyingi hizi hasa kwa mlalanjaa kama Mgosi.

Hata hivyo, tunamshukuru Mungu Mgosi amebaki na pa kushika kwa kubakiwa na mshirika wake wa bedroom bi mkubwa mama Kidume. Magodoro yamekwenda, hata mshirika wa bedroom kama siyo kunasa kwenye mti na Mgosi kuyapiga maji na kumnyofoa, lololo tungekuwa tunaongea mengine! Mgosi angekuwa sasa analiasa kisambaaa, tate nane tate nage kaita mgima mgima sijui angelalia nini yarabi!

Mgosi ana hasira na watawala walioruhusu waroho wachache kujenga nyumba mabondeni na kupangisha wakati wao hawaishi huko. Ingawa alifarijiwa na mkuu pamoja na walaji wenzake kuja kumjulia hali, bado hajawasamehe kwa kupinda sheria kutokana na masilahi yao ya kisiasa ya kutafuta kura ya kula kwa watu wa mabondeni.

Tumalizie kwa kuwapa pole waathirika
wa mafuriko hata kama walijitakia. Sorry walilazimishishwa na ukapa.Chanzo: Tanzania Daima Desemba 28, 2011.

1 comment:

Malkiory Matiya said...

Majanga na mafuriko yamekuwa kama mtaji wa kisiasa!