Saturday, 31 December 2011

Heri ya Mwaka Mpya 2012Wapendwa mashabiki, wasomaji na wageni wa blog hii, tunachukua fursa hii kuwatakieni heri ya Mwaka Mpya 2012. Tunaamini mwaka 2012 utakuwa ni mwaka wa kurekebisha makosa pale tulipokosea na kuongeza bidii pale tulipofanikiwa. Kumaliza mwaka si jambo lililo chini ya uwezo wetu. Ni neema na baraka za Mwenyezi Mungu aliyetujalia kuumaliza mwaka 2011, pamoja na mazonge yake, na kuuona mwaka 2012.

Hata kama kuvuka toka mwaka kwenda mwingine ni suala la kubadili namba na tarakimu, bado kuna haja ya kujiwekea malengo binafsi kama watu binafsi na taifa na kuwa tayari kuyafanikisha. Kimsingi, mwaka 2011, kwa taifa la Tanzania ulikuwa mwaka mgumu. Kwani, licha ya serikali yetu kuendelea kulegalega na kufanya madudu,watanzania wameweza kupambana na kufanya kila walichojaliwa kufanya. Mwaka 2011 ulishuhudia kuongezeka kwa ufisadi hata utapeli. Rejea chama tawala na serikali yake kushindwa kukuza uchumi na kupambana na ufisadi. Rejea kuibuka kwa matapeli wengi wa kidini na kiroho kubwa likiwa ni babu wa Loliondo aliyehadaa ulimwengu kuwa ana dawa ya kutibu kila kitu wakati si kweli bali utapeli wa kitoto. Mwaka 2011 ulishuhudia mauaji ya kinyama yakitekelezwa na polisi huku serikali ikikaa kimya. Rejea mauaji ya Arusha na mengine mengi.
Tukio la mwisho wa mwaka la mafuriko jijini Dar es salaam haliwezi kupita bila kuongelewa. Ingawa waathirika walijitakia kuishi mabondeni kwa kisingizio cha umaskini na ukosefu wa umakini kwa serikali, bado ni pigo kwa taifa kutokana na kupoteza watu wasio na hatia hasa watoto ambao hawana uwezo wa kujipangia wapi wazaliwe au kulelewa.

Kwa upande wa Afrika, mwaka 2011 ulikuwa mwaka wa mapinduzi na kujikomboa hasa kwa wenzetu wa Maghreb ambapo tawala chafu na kandamizi nchini Tunisia Misri na Libya zilianguka huku baadhi ya watawala wakifungasha virago kwenda kuishi ugeni, wengine kufunguliwa mashtaka na wengine kuawa kinyama kama wezi wa kuku kama ilivyototeka kwa Muammar Gaddafi imla wa zamani wa Libya.

Kimataifa mwaka 2011 ulikuwa na mambo mchanganyiko kubwa likiwa ni kuzorota kwa uchumi wa Ulaya ambapo nchi za Ugiriki na Hispania ziliokolewa na mataifa mengine ya Ulaya. Kingine cha mno ni kusakwa na kuawa kwa Osama bin Laden kiongozi wa Al Qaida aliyelingaisha taifa la Marekani kwa muda mrefu hapo Mei 2, 2011.

Si rahisi kuvinjari matukio yote ya 2011. Hivyo, kwa ufupi tumalizie kwa kuwatakieni heri ya Mwaka Mpya 2012.

No comments: